Featured Post

INASADIFU KUPENDA BOGA NA UA LAKE



NA ALOYCE NDELEIO
“Ukipenda boga penda na ua lake” Huu ni usemi maarufu wa Kiswahili wenye maana nzito. Usemi huu unakumbusha Waswahili umuhimu wa kujali na kuenzi watu wanaoweza kuwa ni mhimili wa vitu muhimu wanavyopenda sana.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alianza kuendesha mapambano ya kiuchumi nab ado anaendelea nayo na hakuna ubishi kuwa yapo mafanikio  makubwa.

Kuna wanachama na wasio wanachama wa CCM wanaomsifia Rais Magufuli kutokana na kasi yake ya utendaji lakini pia wapo wanaokosoa kwa sababu mbalimbali zinazoeleweka na hali kadhalika zisizoeleweka.
Wakati Serikali ya Awamu ya Tano inakaribia kutimiza miaka mitatu  tangu iingie madarakani wale waliokuwa wanaimba pambio la ‘kuisoma namba’ wakiwa na imani ya kuendelea kuvuna jasho sasa wanasoma kozi ya kuishi kwa jasho kutoka kwa wavuja jasho.
Kama watakuwa ni wazito kuelewa somo watapata tabu sana kufikia hatua ya kuihitimu kozi hiyo ambayo ni endelevu. Walio na wepesi wa kuelewa wapo katika mkondo unaoendana na muhtasari wa somo lenyewe.
Hata hivyo kama raia halali wa taifa hili, watu hao wana haki ya kisheria na kikatiba ya kukosoa ili mradi hawavunji sheria. Lakini wakati huo huo raia wenye kufikiri vizuri wanatakiwa kutoa maoni yao juu ya suala hili pia.
Lakini pia katika utendaji huo Rais Magufuli pamoja na Waziri wake Mkuu, Kassim Majaliwa kwa pamoja wanaonekana kuwajibika kwa jamii kama  uwajibikaji huo ulivyokuwa  unanadiwa wakati wa kampeni za uchaguzi.
Kwa mtu mwenye busara hawezi kumsifia rubani wa ndege ya abiria kwa kazi nzuri na wakati huo huo akasahau kuwasifia wahandisi wa ndege wanaoruka na rubani huyo kila mara.
Kwa mujibu wa mfumo wa kisiasa, kikatiba na kisheria unaoongoza Serikali ya Muungano wa Tanzania, Rais Magufuli ni kama rubani mkuu na Waziri Mkuu Majaliwa ni mhandisi mkuu wa ndege ya abiria. Hivyo kwa chochote kitakachotokea au kufanywa  na mmoja wao lazima kukubaliana nalo kwa kuwa “Ukipenda boga penda na ua lake”.
Kuna usemi mwingine wa Kiswahili unaotumika kama swali. “Kuku na yai nani katangulia ?” Mara nyingi usemi huu unatumika kuhoji watu wanaotathmini mambo mazito kirahisi na kutoa kauli mbovu. Unakumbusha pia Waswahili umuhimu wa kuenzi vitu fulani pamoja na mihimili  inayowezesha vitu hivyo kudumu na kuendelea kuwepo duniani.
Ni wazi kwamba bila kuku kuwepo, dunia haiwezi kupata mayai na hali kadhalika bila kuwepo kwa mayai kiumbe aitwaye kuku kitatoweka duniani kwa kushindwa kuongezeka idadi.
Kwa mtazamo wa kisiasa hapa nchini ni wazi kwamba Rais mwenye uwezo mkubwa kiutendaji anaweza kushindwa kazi na kuonekana hafai iwapo chini yake atakuwa na Waziri Mkuu asiyefaa.
Pengine waasisi wa taifa hili kwa kutumia busara zao walilitambua hilo mapema na ndio maana wakapendekeza na hatimaye kupitishwa kikatiba kwamba Waziri Mkuu ateuliwe na Rais na kisha ndio apitishwe na Wabunge wote kwa kura za siri.
Waziri Mkuu ndiye anayeongoza shughuli zote za serikali Bungeni na ndio msemaji mkuu wa mwisho wa serikali. Hili si suala jepesi kwani Waziri Mkuu anawajibika kutetea maamuzi yote magumu ya serikali na kuwahakikishia  wabunge kwamba serikali inafanya kazi kuridhisha wapiga kura na walipa kodi wa nchi hii.
Nje ya Bunge, Waziri Mkuu anawajibika kuwahakikishia wananchi, wanachama wa chama chake, mabalozi na wafadhili wa nje na ndani kwamba serikali inawajibika kikamilifu kwa raia walioiweka madarakani.
Hakuna watu wagumu kuridhishwa na serikali za nchi zinazoendelea kama wafadhili wa nje hususan watoa mikopo ya kimataifa kama Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).
Hiyo si kazi nyepesi na asiyeiona basi hataweza pia kutambua umuhimu wa ua la boga au yai la kuku katika maendeleo endelevu ya viumbe hai hapa duniani.
Kwa hakika Waziri Mkuu anakalia kiti cha moto kuliko vyote katika vyeo vya kisiasa hapa Tanzania na hakuna Waziri Mkuu miongoni wa wote waliopitia wadhifa huo aliyewahi kukalia kiti hicho akathubutu kusema kwamba cheo hicho kimempa nafasi ya kufurahia maisha na familia yake, kwani ni kazi ngumu.
Hali hiyo inatokana na sababu kuwa familia yake inakuwa imepanuka na kuwa ni familia ya Watanzania wote na katika mazingira kama hayo fikra na mawazo ni kuhakikisha kuwa mahitaji ya watu hao yanapatikana kwa ufanisi. 
Waziri Mkuu wa kwanza alikuwa Mwalimu Julius Nyerere Desemba 1961 baada ya Tanganyika kupata uhuru na kabla ya muungano na Zanzibar.
Mwalimu alijiuzulu uwaziri mkuu na kumwachia Mzee Rashid Kawawa kabla ya kutwa urais wa Jamhuri ya Tanganyika 1962 na hatimaye urais wa Muungano wa Tanzania Aprili 1964.
Mzee Kawawa alishashika tena nafasi hiyo baada ya cheo cha umakamu wa pili wa rais alichokuwa nacho kufutwa rasmi kikatiba.
Wanasiasa wengine waliokwisha shika cheo hicho ni Hayati Edward Moringe Sokoine, Dk. Salim A. Salim, Jaji Joseph Warioba, Cleopa Msuya, John Malecela, Frederick Sumaye, Edward Lowassa na Mizengo Pinda.
Kwa hakika hakuna mmoja miongoni mwa wanasiasa hao atakuambia kwamba cheo hicho kimempa nafasi ya kufurahia maisha na familia yake kwani ni kazi ngumu sana.
Hali kadhalika katika kipindi ambacho jamii ilikuwa imezongwa na ubadhirifu wa rasilimali za nchi  hususani katika madini, uvuvi, nishati ya gesi asilia ni dhahiri kuwa mzigo umo kichwani kwake kuhakikisha kuwa unakuwepo ufanisi ili kuondoa hulka ya ukuwadi wa rasilimali uliokuwa unamea kwa kasi.
Aidha wakati mkakati na malengo ya serikali ni kuelekea katika uchumi wa kati na hususan kuinyanyua sekta ya viwanda iliyokuwa imepooza lazima unakuwepo umakini wa ziada kuhakikisha hilo linafanikiwa.
Hilo linatokana na kigezo muhimu ambacho ni kuwepo kwa boga na ua lake na vyote viwili na hivyo kulipenda boga peke yake haiwezekani ni lazima pia kulipenda ua lake.
CHANZO: TANZANITE

Comments