Featured Post

IK, SAYANSI KUDHIBITI MABADILIKO TABIANCHI



NA ALOYCE NDELEIO
Jamii za asili zina utajiri mkubwa wa maarifa kuhusu mazingira yao ambayo yakitumiwa vizuri na kushirikishwa yana mchango mkubwa wa kuboresha juhudi za kisayansi katika kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
Uhifadhi wa kale na kurudiwa kwa vitendo vinavyotumiwa na makundi ya asili kwenye maeneo mbalimbali duniani katika kuendesha maisha yao na umekuwa unajumuishwa katika mikakati ya kisasa ambayo ina ufanisi katika maeneo husika.

Athari za mabadiliko ya tabianchi yamekuwa ni jambo la wazi duniani na  kuongezeka kwake kumekuwa ni kwa kiwango kikubwa kwa kuzingatia mtiririko wa majanga asili katika miaka ya hivi karibuni.
Wakati watafiti, watendaji wa shughuli za maendeleo na wapanga sera wanapokuwa katika hatua za kukabili hali hiyo kunaonesha mkanganyiko, jamii za asili nyingi zimekuwa zinaishi katika mazingira magumu na zimejifunza kuishi na kukabiliana na changamoto  zinazosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.
Kutoka wachungaji  wanaoishi katika mazingira ya ukame  kusini mwa jangwa la Sahara hadi wanavijiji wanaoishi katika mazingira hatarishi katika mataifa ya visiwa wanatumia uelewa na utendaji unahama kutoka uzoefu wa jadi wa wazee wao kwa kuendelea kuyashikilia maisha yao na kuboresha mienendo yao ndani ya  athari za mabadiliko ya tabianchi.
Uthibitisho muhimu wa maarifa  upo katika  jamii nyingi ambao unafahamika kama Maarifa Asilia (IK) ambayo yamewezesha maendeleo ya jamii na kutaka kujumuishwa kwake katika mikakati ya kudhibiti mabadiliko ya tabianchi.
Lakini miongoni mwa swali linaloulizwa na watu wengi  kuhusu IK ni kitu gani cha kujifunza kutoka kwa watumiaji na wakulima  watakaokuwa mstari wa mbele kuhusu madhara ya mabadiliko ya tabianchi wakati wakiendesha maisha yao ya kila siku?

Kupata uzoefu wa asili
Sehemu kubwa ya marifa asilia  imekuwa inaelezwa kwa simulizi za mdomo na hazikuandikwa sawa sawa, jambo ambalo si kwamba linahusisha uhifadhi wake, bali pia kunafanya iwe vigumu kushirikiana maarifa sahihi na wadau muhimu.
Kukabiliana na hali hiyo  yamekuwepo machapisho kadhaa ya vitabu ambayo ni; Mifumo wa Maarifa Asilia na Usimamizi wa Mabadiliko ya Tabianchi na kitabu cha Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco); Hali ya Hewa isiyoeleweka: Maarifa ya asili kwa Tathmini na Udhibiti wa Mabadiliko ya Tabianchi, ambavyo vimekusanya taarifa tofauti za mifumo ya Maarifa Asilia yaliyotumiwa na jamii katika maeneo mbalimbali duniani.
Kuzinduliwa kwa kitabu cha Maarifa Aslia kumechangia katika kuimarisha uelewa wa tabianchi.
Katika kuongezea mwenendo huo, Muundo wa Azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi uliibua kanzidata ya mikakati ya kuendana na uhalisia wake unaotoa mifumo ya rekodi  zilizotumika katika maarifa asilia ya jamii kuendana na athari za hali ya hewa kama vile kubadilika kwa misimu, ukame na mvua  zisizo za kawaida.
Baadhi ya mashirika yanayotafuta taarifa za maarifa hayo  yameanzisha programu za utafiti zinazofanya kazi na jamii za asili kuhamisha uelewa wao katika hali ambayo yanaweza kutumika na watekelezaji wa maendeleo na wapanga sera.
Hiyo ni pamoja na kuanzisha kwa ramani zinazoonesha hali za asili katika maeneo ya kawaida kwa kuwashirikisha watu walio na uelewa wa mazingira ya kawaida na kuyaweka katika mifumo ya kidijitali hivyo kwamba mamlaka ya usambazaji na usimamizi wa vyanzo kufikiwa na maarifa hayo.

Kujumuisha IK, tafiti za kisayansi
Kujumuisha vizuri tabiri za tabianchi na misimu katika maamuzi ya kilimo na ufugaji zinazohusisha kuunga mkono ushirikiano kati ya watabiri wa hali ya hewa na jamii za asili ni hatua sahihi.
Kwa mfano zipo jamii zinazotegemea vidokezo au viashiria vya asili kama vile kuvuma kwa upepo, tabia za wadudu na milio ya ndege kuashiria ni wakati gani wa kulima na kuotesha mbegu katika mashamba.
Wanajamii wengi wanapoangalia wadudu wakiwa wametokeza kwa wingi ardhini na kutembea katika misafara au katika maeneo mengine wakisikia aina fulani ya ndege wakitoa milio mfululizo huwa wanaamini msimu wa mvua umekaribia.
Kutokana na hali hiyo huharakisha kulima na kuziweka mbegu wanazokuwa nazo tayari kuotesha na kwa kiwango kikubwa wanakuwa wapo sahihi.
Hata hivyo mabadiliko ya tabianchi yamebadilisha uhakika wa vidokezo au viashiria na hivyo kushindwa kuwawezesha kuelewa kwa uhakika ni muda gani wanatakiwa kufanya matayarisho ya mashamba yao.
Katika mazingira hayo inakuwa ni vizuri kwa watabiri wa hali ya hewa na wenyeji wanaoelewa hali ya hewa kushirikiana mwanzoni mwa msimu ili kuibua utabiri wa msimu ambao utawawezesha  kutoa taarifa sahihi kwa wanavijiji.
Kwa kuunganisha maarifa asilia na taarifa za kisayansi  kunasaidia kuunda utabiri sahihi unaokubalika na jamii na unaoweza kukubalika na kutumika katika kuangalia hali tofauti za tabianchi.

Kuunda mjadala wa pamoja
Dhana ya kuoanisha IK na sayansi  kumekuwa kunaenda sambamba na  uzinduzi wa programu ya Umoja wa Mataifa unaounda  mitandao ya tafiti za sehemu mbalimbali  ambayo inaziweka pamoja jumuia za wanajamii wa asili katika eneo moja, wanasayansi na maofisa wa serikali katika kuweka taarifa na uelewa wa mifumo ya IK.
Katika mkakati unaoitwa ‘Kuelewa Mabadiliko ya nchi katika Afrika’ umeendesha miradi ya tafiti kijamii katika jamii za wafugaji ambao ni wachungaji wa mifugo za Fulani (Burkina Faso), Fulani Mbororo (Chad), Afar (Ethiopia), Samburu na Laikipia Maasai (Kenya), Maasai (Tanzania), na Bahima na Karamojong (Uganda).
Juni 2017 wanajamii kutoka jumuia ya Bahima na Karamojong  walikutana na wanataaluma na wataalamu wa tabianchi wa serikali mjini Kampala, Uganda katika warsha ya siku mbili kuhusu hali ya hewa  na uelewa wa tabianchi kati ya wafugaji na mifumo ya utabiri wa kisayansi katika Afrika.
Katika kupanga mikakati ya mabadiliko ya tabianchi katika maeneo ya kilimo na maendeleo vijijini, ni muhimu kutoa msukumo  wa kuunda uelewa wa pamoja na wakulima.
Kuwepo kwa mijadala shirikishi kutasaidia kuwa na majadiliano ya kuunganisha mifumo ya maarifa asilia na uelewa wa kisayansi katika kuboresha mbinu za utabiri kukabili athari za mabadiliko ya tabianchi na hivyo kuwezesha utendaji wa jamii katika kuikabili hali hiyo.
CHANZO: TANZANITE

Comments