Featured Post

HUU NDIO UKWELI WA SHAMBULIO LA LISSU



* Mbinu zinazodaiwa kumuondoa Wangwe zatumika
* Kuendelea kubaki na risasi kwenye uti wa mgongo

NA MWANDISHI WETU
UKWELI wa shambulio la risasi la Mbunge wa Singida Kaskazini kupitia Chadema, Tundu Lissu, umeendelea kubainishwa licha ya yeye mwenyewe pamoja na viongozi wa chama chake kuuaminisha umma kwamba kuna mkono wa dola.

Lissu, ambaye anaendelea na matibabu ya nje katika hospitali ya Leuven nchini Ubelgiji anaelezwa kwamba hali yake inaendelea vizuri ingawa sasa hawezi kutolewa risasi pekee iliyopo kwenye uti wa mgongo, huku ndoto za kurejea nchini zikiwa zimeyuka kwa sasa.
Habari za uchunguzi zinaeleza kwamba, ukweli wa shambulio la Lissu lililotokea Septemba 7, 2017 jijini Dodoma anaujua dereva wake Simon Mohamed Bakari na linahusishwa kwa asilimia kubwa na viongozi wa juu wa Chadema.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, shambulio hilo linashabihiana na namna kilivyotokea kifo cha Chacha Zakayo Wangwe, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa, Mbunge wa Tarime na Diwani wa Kata ya Turwa.
Inaelezwa kwamba, ingawa Wangwe alikufa kwa ajali Julai 28, 2008 katika eneo la Pandambili wilayani Kongwa, na Lissu alishambuliwa kwa risasi, lakini matukio hayo mawili yanadaiwa kuwa na dhima moja kutokana na mambo yanayoendelea ndani ya chama hicho.
Vyanzo vya habari kutoka ndani ya Chadema vinaeleza kwamba, licha ya kuwa na mvutano na Serikali katika kipindi hicho, lakini tukio la kushambuliwa kwa Lissu linahusishwa mpango uliokuwepo kwa kutaka kumpendekeza awanie uenyekiti ili kuleta mabadiliko ndani ya chama hicho ambacho demokrasia imefinyangwa.
Ajali ya Wangwe ilitokea wakati mwanasiasa huyo akiwa na mvutano mkubwa na Chadema, hususan Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Freeman Mbowe, ambapo Kamati Kuu ilimsimamisha kwa madai ya utovu wa nidhamu.
Kinachodaiwa kumponza ni hatua yake ya kuhoji masuala ya matumizi ya ruzuku, madeni ya Mbowe aliyodai kuwa alikikopesha chama, upendeleo katika uteuzi wa wabunge wa viti maalum na masuala mengine yakiwemo ya ukabila na ukanda.
"Dereva wa Lissu anao ukweli wote na ndiyo maana alikimbizwa na Mbowe asihojiwe," kilisema chanzo kimoja kutoka ndani ya Chadema.
Inaelezwa kwamba, dereva huyo anaweza akawa analifahamu tukio zima, kwani hata maelezo yake yasiyo rasmi aliyoyatoa akiwa Nairobi, Kenya yanajichanganya na kuacha maswali mengi licha ya kutetewa na Lissu mwenyewe kwamba anamuamini kwa kuwa yeye ndiye aliyemlea.
Lissu alishambuliwa na watu ambao mpaka sasa hawajafahamika ambapo anadaiwa kufyatuliwa risasi 32 akiwa ndani ya gari lake baada ya kuwasili katika makazi yake eneo la Area D, lakini ni risasi tano zilizompata na kumjeruhi vibaya.
Mara baada ya Lissu kushambuliwa na kukimbizwa hospitali, uongozi wa Chadema uliamua kumsafirisha na kumpeleka kwenye Hospitali ya Aga Khan jijini Nairobi, Kenya pamoja na dereva wake ambaye hakupata hata jeraha moja, hali ambayo ilizua sintofahamu.
Dereva huyo, ambaye ndiye hasa shahidi wa kwanza kwenye tukio hilo, hakupewa ruhusa na viongozi wa Chadema ili akatoe maelezo Polisi, na badala yake viongozi wa juu wa chama hicho ndio waliokuwa wakimsemea huku wakiituhumu serikali kwamba ndiyo iliyohusika.
Lakini katika kile ambacho hakikutarajiwa, dereva huyo alitoa maelezo ambayo mpaka sasa yanawalazimu wachunguzi wa masuala ya upelelezi kuamini kwamba kuna vitu anavyovijua, kwani tukio zima limeacha mazonge mengi.
Dereva huyo alidai kwamba ni yeye ndiye aliyemzuia Lissu asishuke
ndani ya gari kabla hata risasi hazijaanza kurushwa na kwamba walikaa ndani ya gari kwa takriban dakika 20 kabla ya kushambuliwa.
Akaeleza kwamba, watu hao walikuwa wakimfuata kila siku nyumbani na siku hiyo walianza kuwafuatilia kuanzia kwenye geti la Bunge hadi nyumbani.
Lissu mwenyewe alidai kwamba, waliomshambulia ambao inadaiwa walitumia magari mawili – Toyota Land Cruiser na Nissan Patrol, “ninawajua. Nimekutana nao mara kadhaa. Nimewatambua kwa kuwa nilikutana nao Dar es Salaam wakati wananifuatilia.”
Dereva wa Lissu alisema; “niliona ile Nissan ambayo ilibeba watu waliompiga risasi Lissu. Tulipoondoka pale eneo la nje ya uzio wa bungeni, lile gari lilitufuata njia nzima hadi nyumbani.”
Simon alisema, siku hiyo ya tukio alimchukua Lissu nje ya geti la Bunge. Akataja namba ya gari ambalo lilibeba “wauaji wa Lissu” kuwa ni Nissan Patrol T 932 AKN.
“Yale magari mawili, moja lilitufuata hadi nyumbani. Liliingia ndani ya geti la nyumba za Area D, ambako Lissu anaishi. Hilo ndilo lililobeba watu waliomshambulia Lissu kwa risasi.”
“Jingine liliishia pale getini. Hili lililotufuata hadi nyumbani, lilikuja kuegeshwa pembeni mwa gari letu. Akajitokeza mtu aliyekuwa ameketi kiti cha mbele cha abiria na kushusha kioo chake ili kutuangalia tuliomo ndani ya gari.
"Baadaye akashuka mtu kutoka kiti cha nyuma cha upande wa kushoto. Akajifanya kama anaongea na mtu kwa njia ya mikono. Lakini ukweli ni kuwa alikuwa anamchungulia Lissu kama yumo ndani ya gari.
"Baada ya muda mfupi akarudi kwenye gari, wakati huo dereva wa gari hilo alikuwa ameshaligeuza na kuliekeleza lilikotoka.
“Ghafla yule bwana akashuka na bunduki aina ya SMG ambayo niliiona wakati anafungua mlango. Akaanza kumimina risasi kwenye gari letu. Nilichokifanya, ni kumlaza Lissu kwenye kiti cha dereva na mimi kuruka nje ya gari na kujificha mvunguni mwa gari jingine lililokuwa limeegeshwa kwenye uwanja wa nyumba za wabunge.”
Mpaka sasa haijafahamika gari hilo alilojificha dereva mvunguni lilikuwa la nani.
Simon akasema: "Kabla ya urushaji risasi kuanza, Lissu alitaka kufungua mlango wa gari lake na kushuka kuelekea ndani ya nyumba yake. Lakini baada ya kumueleza kuwa gari lililopo pembeni limeanza kutufuatilia muda mrefu na hivyo asubiri kwanza, alikubaliana na ushauri huo.
"Mimi na Lissu tulibaki kwenye gari kwa zaidi ya dakika 20 tukiangalia nyendo za watu waliokuwamo kwenye gari lililokuwa linatufuatilia.
“Risasi zilipigwa mfululizo… Wakati nikiwa nimejiangusha kwenye mvungu wa gari, nilisikia yowe la Lissu mara moja, akiashiria kuwa risasi zilizokuwa zikirushwa zimempata,” akasimulia Simon.
“Nilimuona kabisa kabisa. Huyu mtu aliyekuwa anarusha risasi; ninamfahamu. Alikuwa amevaa kapero na miwani myeusi na kizubao… Ni yuleyule niliyekuwa nimekutana naye jijini Dar es Salaam,” akaeleza.
“Baada ya kusikika risasi nyingi zimepigwa kwenye gari la mheshimiwa Lissu, naona waliamini wamemuua na waliondoka kwa kasi kurudi mjini.
“Baada ya kuondoka, mimi nikatoka mvunguni mwa gari na kumkimbilia Lissu. Nikamuona bado anapumua. Nikapiga kelele kuomba msaada. Wakati huo, Lissu alikuwa anavuja damu nyingi mwilini mwake.”
Katika shambulio hilo, Lissu alipata majeraha makubwa kwenye miguu yake miwili, tumbo na mkono mmoja.
 
Kutokana na maelezo hayo, kuna maswali mengi ambayo yameachwa bila majibu:
Mosi, anasema watu hao walikuwa wakimfuata kila siku hadi nyumbani. Na kama siku hiyo pekee walimfuata hadi anaanza kuelekea nyumbani, dereva hakuona hali ni tofauti na kuamua kupeleka gari sehemu salama au kutumia mbinu ambayo ingemthibitishia kuwepo kwa nia ovu?
Pili, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema shambulio hilo ni la kisiasa kwa kuwa Lissu hana adui nje ya siasa. Hao maadui ndani ya siasa ni nani? Ni wanasiasa wa chama kingine au walio ndani ya Chadema? Ni maadui katika ngazi gani ya kisiasa ambayo inaweza kufikia kiwango cha kutaka kumuua Lissu?
Tatu, dereva anasema alimzuia Lissu asishuke, na kwamba walikaa ndani ya gari kwa zaidi ya dakika 20. Ni kwa nini katika muda huo wasichukue hatua hata ya kupiga simu kwa watu wengine kuwajulisha mashaka yao, japo hata kwa familia tu?
Nne, kuna sababu gani ambazo zilimfanya dereva huyo amzuie Lissu asishuke kwenye gari kwa kipindi chote hicho? Kama alihisi hatari, ni kwa nini hakuliondoa gari mahali hapo na ikiwezekana kurudi alikotoka? Alikuwa anasubiri nini kama siyo kujua ambacho kingetokea?
Tano, dereva anasema, mmoja wa watu hao alitoka na bunduki aina ya SMG. Aliitambuaje aina bunduki?
Tano, anasema watu hao walifyatua risasi mfululizo, je, yeye amepitia mafunzo ya jeshi kiasi cha kufanikiwa kukwepa risasi hizo mfululizo? Aliwezaje kupata ujasiri wa kumhamishia Lissu kwenye kiti chake (cha dereva) na yeye akafanikiwa kutoka nje na kwenda kujificha uvunguni kwa gari nyingine (ambayo haijulikani ni ya nani)?
Sita, inawezekana kweli katika purukushani kama hizo yeye hakuweza hata kujeruhiwa? Ni kweli Lissu ndiye alikuwa mlengwa na ndiyo maana yeye akaachwa au aliachwa kwa sababu naye alikuwa sehemu ya mpango huo ndiyo maana hakuweza hata kujeruhiwa?
Yako maswali mengi yasiyo na majibu, kama ilivyokuwa katika tukio la ajali ya Wangwe, ambayo wengi walidai huenda mwanasiasa huyo aliauwa kabla ya ajali hiyo huku dereva wake, Deus Mallya, akitoka salama salimini.
CHANZO: FAHARI YETU

Comments