Featured Post

FADHILA KWA ‘DÉCLASSÉ’ NI MAZINGIRA YENYE TIJA



NA ALOYCE NDELEIO
KUPANUKA kwa pengo kati ya walalahoi na walalahai kumekuwa  kunachangia kukua na kustawi kwa tofauti za hali za maisha baina ya makundi hayo mawili.
Wanaoumia siku zote katika mtazamo huo wamekuwa ni walala hoi ambao kila uchao wamekuwa wakiiona leo yao kuwa ni afadhali ya jana.
Lakini juhudi zinapofanyika kuliinua kundi moja ni dhahiri kuwa hali hiyo  inatarajiwa kuzuia pengo hilo kuendelea kupanuka.

Walala hoi ndio wanaangukia katika kundi la ‘déclassé’ ambalo kihistoria limekuwa likipambana na hata kuchangia sehemu  kubwa ya mendeleo ya nchi  licha ya juhudi zao kutoonekana wazi.
Linapokuja suala la kuiletea jamii maendeleo jukumu hilo linakuwa ni la serikali hata hivyo kutokana na kukithiri kwa mazoea  kundi ambalo limekuwa linaonekana kunufaika na maendeleo hayo ni kundi la walala hai kwa kuwa wao ndiyo wanakuwa wameshikilia mpini.
Yanapokuja masuala ya siasa  kundi la walala hoi limekuwa  na fursa ndogo lakini zikitokea chaguzi  kundi hili linaonekana kuwa na thamani kubwa  kuliko hata rasilimali nyingine ndani ya nchi.
Neno déclassé lilikuwa maarufu miongoni mwa nchi za Ulaya ambako walionekana kuwa ni watu wasio na umuhimu ndani ya jamii.
Hivyo ni kundi linaloundwa na wanajamii wanaoonekana kukosa haiba ndani ya jamii  ambao ni pamoja  wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama machinga, mama lishe, warina asili, wapagazi, wavuvi  na wengine wanaoingia katika mtazamo mzima wa kumenyeka.
Mara nyingine kundi hili linajumuisha hata wale wanaofanya biashara zisizo na staha kama vile machanguadoa.
Dhana ya déclassé ndani ya Afrika ilipata  umaarufu na kufafanuliwa wazi enzi za waasisi wa mataifa ya Afrika katika kupigania uhuru na hususani kutoka kwa Rais wa Kwanza wa Ghana Hayati Dkt. Osagefyo Kwame Nkrumah ambaye alisema kuwa  kundi hili likitumika vizuri huleta mapinduzi ndani ya nchi.
Mapinduzi ambayo aliyazungumzia ni pamoja na kuwapatia fursa zinazoweza kutumika kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya jamii badala ya kuwaacha  wakihangaika  na hata kugeuka kero.
Dhana hiyo imekuwa endelevu hususani linapotokeza suala la uchaguzi kwamba  kundi hili la jamii limekuwa linachukuliwa kama mtaji wa kujipatia kura au wa kufanikisha ushindi wa baadhi ya vyama vya siasa.
Hata hivyo, mara nyingi imekuwa inaonekana kuwa baada ya chaguzi za viongozi katika ngazi mbalimbali kumalizika wamekuwa wakisokomezwa pembezoni na hata ahadi wanazokuwa wameaahidiwa kutotekelezwa jambo ambalo limekuwa likiamsha hasira miongoni mwao.
Lakini baadhi ya wanasiasa wanapotambua umuhimu wa kundi hilo hususani baada ya uchaguzi kwa kutafuta namna ya kulishirikisha katika mkondo wa kupata kipato badala ya kuwasokomeza pembezoni linakuwa ni jambo la busara.
Hili ndilo linalowasibu wafanya biashara  ndogo ndogo maarufu kama wamachinga ambapo mamlaka tawala imeshasema wasibughudhiwe na waachwe wafanye shughuli za kujipatia kipato katikati ya miji.
Ukweli ni kwamba kundi hili linaundwa na walala hoi na kwa kauli hiyo ya mamlaka tawala ni kudhihirisha kuwajali wateja wake wa kisiasa.
Lakini wakati ikiwa hivyo na walala hoi wakikenua  na kuipigia mamlaka  makofi baadhi wanahoji je, wataendelea kufanya shughuli hizo katika maeneo ya katikati miji hadi lini? Je, kuna dalili zozote za kutengeneza mazingira yatakayowawezesha kufanya biashara zao katika mazingira ya ufanisi na tija?
Kauli ya Nkrumah kwamba kundi hili linaweza kuleta mapinduzi ndani ya jamii inafaa kuangaliwa kwamba pamoja na mamlaka tawala  kulipatia kundi hili baraka za kufanya shughuli zao bila bughudha itakuwa ni sahihi zaidi kama mamlaka hiyo italishushia kundi hili neema itakayotoa jibu hoja hizo.
Kwa maana hiyo kama ni kulipa fadhila kwa kura zao wakati wa uchaguzi  basi iwe ni kuwajengea mazingira yenye tija na ufanisi ya kuendesha shughuli zao.
Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani iliweka mkakati wake kwamba imejipanga kuhakikisha kuwa fadhila chanya zinafanyika katika kuwajengea walalahoi mazingira yenye tija ili waweze kuyendesha maisha ya vyema na kuifaidi keki ya taifa.
Hata hivyo, katika mikakati yake ya kuhakikisha hilo linafanikiwa imejikuta ikikumbana na kadhia za kukosekana kwa uaminifu.
Ni neno moja tu ‘uaminifu’ ambalo maana yake ni tabia ya mtu kuweza kuaminika kama vile kupewa amana za watu aziweke mpaka watakapokuja kuzitaka.
Kadhia hiyo imeonesha kwamba wazi kwamba shughuliza kiuchumi na kisiasa zinapofanywa kwa utendaji usio na usawa au watendaji wake  kutoaminika watu hutaka hakikisho la ziada kabla ya kushiriki katika michakato inayokuwa mbele yao.
Kukosekana kwa uaminifu kumebainishwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika maeneo mbalimbali kwa kuzuru na kutoa maagizo na maangalizo ambayo matokeo yake ni kubainika  kuwa usimamizi wa sehemu kubwa ya rasilimali za nchi umekuwa haufanywi kwa uaminifu na hivyo kuikosesha serikali mapato.
Hivyo kukosekana kwa uaminifu ndiko kunawafanya watu  kutokuwa na imani au kushiriki kwa kiwango kidogo katika shughuli za kiuchumi na kisiasa kutokana na imani kwamba hakuna kinachotendeka kwa haki bali kutamalaki kwa ubadhirifu.
Katika kuamini kwamba uaminifu ni gundi ya kijamii na kwamba unawezesha kushirikiana pamoja na kwa ufanisi zaidi katika malengo ambayo jamii imejiwekea  na usimamizi wake ukifanywa na waliopewa dhamana watendaji wengi walitumbuliwa.
Kukosekana kwa uaminifu kumesababisha  kuundwa kwa kamati za kuchunguza mambo mbalimbali ambayo waliopewa dhamana wameingia mikataba na wawekezaji.
Kimsingi kuundwa kwa kamati za uchunguzi ni matokeo ya kuona kuwepo kwa ongezeko  kutowiana kiuchumi  ambayo ni sababu muhimu ya kushuka kwa uaminifu na matokeo yake kushamiri  kutowiana  na kuwepo makundi  yanayotofautiana kijamii na kiuchumi.
Pindi watu wanapoona kuwepo kwa pengo kubwa la kiuchumi miongoni mwa watu kama wao na ambao wanaishi sehemu moja likijumuisha umri, elimu na hata aina ya kazi wanazozifanya uaminifu hupungua, na kupoteza imani kwa watu wengine na serikali.
Uaminifu unaweza kuboresha ushirikiano katika umma na kuondoa matatizo yanayohusu upatikanaji wa huduma za kijamii. Ukweli unabakia kuwa serikali haitamudu kutatua changamoto za kiuchumi na kijamii  katika jamii ambayo haina uaminifu, ambayo haikutulia na iliyogawanyika.
Kukosekana kwa uaminifu kumesababisha kupungua kwa hadhi ya sera za  kuunufaisha umma kwani motisha wa kiuchumi na mtazamo wa tabia za kiuchumi miongoni mwa wananchi na hata biashara zilikuwa zimepuuzwa. Hiyo inamaanisha kukosekana kwa uaminifu kulizuia sera za serikali kutekelezwa kwa ufanisi.
Inasadifu kusema kuwa kwa kutambua hilo serikali imekuwa inachukua hatua na nyingi zimeshawekwa wazi hususani katika rasilimali za madini ili kuhakikisha sio tu kwamba ni kulipa fadhila bali jamii inanufaika na kile ambacho  ni haki yake kukipata na kinanufaisha  watu wake wote.

Comments