- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
NA DEREK MURUSURI, DAR ES SALAAM
USEMI maarufu katika vitabu vifakatifu
kuhusu jiwe lililokataliwa na waashi kuwa jiwe kuu la pembeni, unasadifu uteuzi
wa gwiji la habari nchini, Ernest Samson Sungura, kuongoza mageuzi makubwa ya
vyombo vya habari vya CCM.
Habari zilizopatikana kutoka ndani ya
vyombo vya habari vya CCM zinasema kuwa uteuzi wa Comrade Sungura umetangazwa
leo jijini Dar Es Salaam na Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Bashiru Ali, ambaye
alisema uteuzi huo umeidhinishwa na Kamati Kuu ya CCM.
Comrade Sungura sasa anakuwa Kiongozi
Mkuu wa vyombo vya habari vya CCM, aliyepewa jukumu kubwa la kufanya mageuzi ya
kimuundo na kimfumo (restructuring) ya vyombo hivyo na kuvifanya vitoe
ushindani madhubuti (competitive) katika tasnia ya habari ndani na nje ya nchi.
Kabla ya uteuzi huo, Sungura alikuwa
Mkurugenzi Mtendaji wa Wakfu wa vyombo vya habari Tanzania (TMF) lakini
aliondolewa katika taasisi hiyo na Bodi yake (TMF) muda mfupi baada ya
kutangazwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC).
Sungura ndiye mwasisi wa Tanzania
Media Foundation (TMF), taasisi iliyoleta mageuzi makubwa katika tasnia ya
habari nchini na kuifanya nchi jirani ya Kenya kuja kujifunza nchini kabla ya
kuanzisha taasisi kama hiyo nchini mwao.
Comrade Sungura ndiye anatarajiwa
kuviongoza vyombo vya habari vya CCM katika mageuzi haya makubwa. Vyombo hivyo
ni pamoja na televisheni, redio, magazeti na vile vya mtandaoni ambavyo katika
siku za karibuni vimetokea kuwa na wafuasi wengi duniani.
Pamoja na mafanikio mengine, Sungura
amekuwa na rekodi nzuri na ya kipekee katika kuleta mageuzi ya kimkakati kwa
taasisi za habari nchini.
Baadhi ya mafanikio makubwa
yameonekana katika kuzipatia taasisi hizo uongozi na menejimenti madhubuti,
hivyo kuleta maboresho katika maudhui, miundo na mifumo, ikiwa ni pamoja na
kuimarisha vyanzo vya mapato na kusaidia vyombo vya habari kujiendesha kama
taasisi kamili zinazopata faida.
Sungura ana uzoefu wa zaidi ya miaka
24 (1994-2018) katika tasnia ya habari nchini, hasa katika kuwajengea uwezo
wanahabari vijana huku akibuni program mbalimbali za kuijenga na kuiimarisha
tasnia ya habari.
Amekuwa anajulikana kwa wengi kama
kiongozi mahiri mwenye kujali matokeo, kocha, menta (mentor), mshauri wa
kitaalam na mwalimu.
Desemba 2017, Comrade Sungura
alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na Mwezi Mei mwaka
huu, alikuwa miongoni mwa wajumbe tisa (9) waliopendekezwa na Mwenyekiti wa CCM
Dkt. John Pombe Magufuli kugombea nafasi za ujumbe wa Kamati Kuu ya CCM.
Wakati akichukua uongozi wa Chama,
Mwenyekiti wa CCM, ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.
John Pombe Magufuli, aliahidi kuleta mageuzi katika vyombo vya habari vya chama
hicho ili kuvifanya kuwa mshindani mzuri katika sekta ya habari ikiwa ni pamoja
na kuwa mhimili katika kusaidia mabadiliko ya kiuchumi nchini.
Sekta ya habari na mawasiliano ni
muhimu sana katika siasa za dunia, ikiwemo Tanzania, hasa katika kutoa
ushawishi na uungwaji mkono wa mikakati na sera za Chama cha kisiasa kwa
umma.
Mafanikio makubwa ya tasnia ya habari
katika muongo mmoja uliopita, kwa kiasi kikubwa umetokana na juhudi kubwa
alizozifanya Sungura kupitia taasisi aliyoiongoza ya TMF.
Bodi ya TMF ilimshinikiza Sungura
aondoke katika wadhifa wake kama Mkurugenzi Mtendaji wa TMF baada ya kushinda
katika uchaguzi uliomwingiza katika chombo kikubwa cha maamuzi cha CCM, NEC.
Sungura ni miongoni mwa wanahabari
makini na wenye rekodi ya ufuatiliaji ambao wamepitia mafunzi katika fani zaidi
ya uandishi wa habari.
"Sungura ana uwezo mkubwa,
amebobea katika fani ya habari, usimamizi wa biashara, mafunzo ya wanahabari,
ikiwa ni pamoja na uandaaji wa mikakati na pia ni mtu asiyeshindwa jambo
analokabidhiwa, hakika CCM imefanya uchaguzi sahihi," alisema Flora
Magabe.
Sungura ndiye mwasisi wa mabadiliko
ya maboresho yaliyosaidia kuongeza uwezo na weledi katika sekta ya habari
nchini ndani ya muongo mmoja uliopita (transformation of the media sector
in Tanzania).
Maboresho hayo pia yalilenga katika
kuzifanya taasisi za habari zijitegemee kiuchumi na hivyo kuziwezesha kuwa huru
katika maamuzi ya kiuhariri.
Comrade Sungura amewahi kufanya kazi
na taasisi za kimataifa kama vile shirika la umoja wa mataifa la Elimu, sayansi
na Utamaduni (UNESCO) katika kuboresha matangazo ya vyombo vya habari vya umma
(Public Broadcasting Services) kama vile TBC na ZBC, kazi ambayo aliifanya kwa
ufanisi mkubwa.
Sungura ana Digrii ya Uzamili katika
usimamizi wa biashara kutoka Chuo Kikuu Cha Dar Es Salaam, Digrii ya
Kwanza katika Usimamizi wa Biashara kutoka katika Chuo hicho hicho na Diploma
ya Uandishi wa Habari kutoka Chuo cha Uandishi wa Habari Tanzania, TSJ (sasa
SJMC).
Comments
Post a Comment