Featured Post

DC TABORA ATOA ONYO KWA WATAALAMU NA WATENDAJI WA MANISPAA

WATAALAMU na Watendaji wote wa halmashauri ya Manispaa ya Tabora wametakiwa kubadilika kiutendaji na kuacha mazoea ili kufanikisha miradi ya maendeleo ya wananchi vinginevyo watachukuliwa hatua kali za kinidhamu. 

Onyo hilo limetolewa  na Mkuu wa wilaya ya Tabora Komanya Eric Kitwala alipokuwa akiongea na Wataalamu, Watendaji na Madiwani wa halmashauri ya Manispaa hiyo.
Alisema manispaa hiyo ina utajiri mkubwa sana lakini cha ajabu Watendaji wake wanashindwa kuutumia vizuri hivyo kukwamisha utekelezaji shughuli za maendeleo ikiwemo kushindwa kufikia lengo la ukusanyaji mapato yake.
Alisema tatizo ni Watumishi kutofanya kazi kwa kujituma hali inayopelekea baadhi ya miradi ya maendeleo kutotekelezwa ipasavyo.
Alisema baada ya kuripoti katika manispaa hiyo na kuanza kutembelea maeneo mbalimbali amegundua kuwa miradi mingi haiko katika kiwango kinachotakiwa licha ya uwepo wa wataalamu na kueleza wazi kuwa baadhi ya Watumishi hawako makini, wanafanya kazi kwa mazoea.
‘Wataalamu na Watendaji badilikeni, sipo tayari kulea wazembe, kama mlizoea kufanya kazi kwa ulegevu hizi ni zama zingine, nataka kila mmoja awajibike ipasavyo, kama huwezi ondoka’, alisema.
Eric alisisitiza kuwa manispaa hiyo ina vyanzo vingi sana vya mapato ambavyo vikisimamiwa vizuri itapiga hatua kubwa sana kimaendeleo tofauti na hali ilivyo sasa  hivyo liagiza kusimamiwa ipasavyo miradi yote inayotekelezwa katika kata zote za manispaa hiyo ili ubora wake uwe sawa na thamani ya fedha iliyotumika, si vinginevyo.
Alibainisha wazi kuwa kumekuwa na hujuma mbalimbali na vitendo vya ubadhirifu vinavyofanywa na baadhi ya watumishi wasio waaminifu katika manispaa hiyo, na taarifa zao zimeshawafikia viongozi wa ngazi za juu, yeyote atakayebainika kuhusika na vitendo hivyo tutamshughulikia ipasavyo.
Alimtaka Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Bosco Ndunguru kuwa mkali sana kwa watumishi wote wanaofanya kazi kwa mazoea na wasio waaminifu na kuchukua hatua stahiki za kinidhamu kwa mtumishi yeyote atakayebainika kuhusika na ubadhirifu au kukwamisha utekelezaji shughuli za maendeleo.
Ndunguru alimhakikishia kuwa hatasita kuchukua hatua za kinidhamu kwa mtumishi yeyote atakayetenda kinyume, aidha alieleza kuwa tayari ameshaanza kuchukua hatua stahiki kwa baadhi ya watumishi ikiweko kuwakata mishahara wale wanaodaiwa masurufu ya muda mrefu.
Meya wa Manispaa hiyo Leopold Chundu Ulaya aliwataka Wataalamu na Watendaji wa manispaa hiyo kutoa ushirikiano kwa Madiwani ili kuhakikisha miradi yote iliyotengewa fedha inatekelewa kwa kiwango kinachokubalika.
Alisema tatizo linalosababisha miradi mingi ya manispaa hiyo kuwa na mapungufu ni kwa sababu ya ushirikishwaji mdogo wa madiwani.

Comments