Featured Post

DC KOMANYA AAGIZA KUONDOLEWA WAKUU WA IDARA WASIO NA TIJA

MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa  ya Tabora, Bosco Ndunguru na Meya wa manispaa hiyo Leopold Chundu Ulaya wameagizwa kuwaondoa mara moja Wakuu wa Idara za Mipango Miji na Ardhi kwa kushindwa kuzisimamia ipasavyo.

Agizo hilo limetolewa  na Mkuu wa wilaya ya Tabora mjini Komanya Eric Kitwala katika kikao cha Madiwani na Wataalamu mjini hapa.
Alisema idara hizo mbili zimejaa malalamiko mengi sana tena ya mara kwa mara kutoka kwa wananchi lakini chakusikitisha Maofisa Wanaozisimamia wapo na hakuna hatua yoyote inayochukuliwa kumaliza hali hiyo.
Alisema Mkuu wa idara yeyote anayeshindwa kumaliza kero au kushughulikia malalamiko ya wananchi katika idara yake ameshindwa kazi na hafai kuendelea kuwepo katika Idara hiyo, anapaswa kuondolewa haraka kwa manufaa ya wananchi.
‘Mkurugenzi Mtendaji na Meya, ondoeni Wakuu wa Idara wote wasio na tija katika idara zao, anzeni na hawa wa Mipango Miji na Ardhi, hizo ni idara muhimu, tafuteni wenye uwezo wa kuziongoza, hawa wameshindwa siwataki’, alisema.
Alisema manispaaa hiyo imechafuka kwa sababu ya idara zisizotekeleza wajibu wao ipasavyo, hivyo akaagiza mchakato wa kuwaondoa uanze haraka iwezekanavyo na kuweka wengine, na wasipofanya hivyo atawaondoa yeye.
Alibainisha kuwa Wakuu hao hawafai kwa kuwa wamekuwa chanzo cha migogoro ya ardhi katika manispaa hiyo ndiyo maana malalamiko yamejaa kila kona.
Kitwala alisisitiza kuwa kuchafuka kwa manispaa hiyo kunachangiwa na viongozi waliopewa dhamana ya wananchi kushindwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo, huku akieleza wazi kuwa hata madiwani wanahusika kuchafua manispaa.
‘Nataka tubadilike ili halmashauri yetu ipige hatua kubwa ya kimaendeleo, sitaki uzembe wa aina yoyote ile, iwe kwa Madiwani, Wakuu wa idara au Watendaji, kila mmoja asimamie kwenye zamu yake’, alisema.
Aidha alimtaka Mkurugenzi, Meya na Naibu Meya kutofumbia macho uzembe wa wakuu wa idara, aliwataka kutathmini utendaji wa kila Mkuu wa Idara na kuchukua hatua mara moja ili kuharakisha maendeleo ya manispaa hiyo.
Alionya madiwani kutotumia nafasi zao kwa manufaa binafsi badala ya kusimamia shughuli za maendeleo katika halmashauri hiyo, alikemea tabia ya kujimilikisha viwanja lukuki, kutosimamia ukusanyaji mapato na kutochukua hatua kwa wakuu wa idara au watendaji wazembe.
Madiwani wa CCM Ramadhan Kapela (kata ya Isevya), Zinduna Kisamba (Tambuka reli), Seleman Juma (Ndevelwa) na Martin Mussa (Mwinyi-CHADEMA) walibainisha wazi kuwa sasa manispaa yao itabadilika, kwa kuwa wamepata DC makini sana.
Walimhakikishia kuwa watamwunga mkono kwa asilimia zote na kumpa ushirikiano unaotakiwa ili anyooshe watumishi wazembe na kukomesha vitendo vya ubadhirifu katika halmashauri hiyo.

Comments