Featured Post

CHANGAMOTO ZA USAFIRI HAZIKWAMISHI USAMBAZAJI DAWA VISIWANI MULEBA

 Mkazi wa Kata ya Katunguru, Robert Lomwadi, akipakia moja ya boksi la dawa, katika Boti namba BKT 00098 MV BMU Mulumo tayari kupelekwa Zahanati ya Kisiwa cha Mazinga, wilayani Muleba mkoani Kagera leo hii.
 Mganga Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Dkt. Modest Burchard, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali ya afya na upokeaji wa dawa kutoka MSD.
 Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Kisiwa cha Mazinga, Johanes Sweetbert (kulia), akizungumza na waandishi wa habari kuhusu jinsi wanavyopokea dawa kutoka MSD na changamoto zilizopo.
 Afisa Huduma kwa Wateja wa MSD Kanda ya Mwanza, Cornelia Mwillawi (kushoto), akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Afya wa Kisiwa cha Mazinga wakati wa kukabidhi dawa.
 Afisa Huduma kwa Wateja wa MSD Kanda ya Mwanza, Cornelia Mwillawi (kushoto), akiwakabidhi mifuko ya vifaa vya mama vya kujifungulia.
 Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Kisiwa cha Mazinga, Johanes Sweetbert (wa pili kulia), akisaini fomu maalumu baada ya kukabidhiwa vifaa hivyo. Wendine ni wajumbe wa kamati ya afya wa Kisiwa cha Mazinga.
 Mkazi wa Kata ya Katunguru, Robert Lomwadi, akibeba boksi la dawa kuzipeleka tayari kwenda kwenye boti kabla ya kuziingiza kwenye boti.
 Mjumbe wa Kamati ya Afya ya Kisiwa cha Mazinga, Winfrida Itaganisa, akizungumzia jinsi wanavyo pokea dawa kutoka MSD.
Wananchi wa Kata ya Katunguru walioshuhudia makabidhiano ya dawa hizo.

Na Dotto Mwaibale, Muleba Kagera
MGANGA Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Dkt. Modest Burchard amesema licha ya changamoto za kusafirisha dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara kwenda visiwani, Bohari ya Dawa (MSD) imekuwa ikitoa ushirikiano mkubwa kuhakikisha dawa zinafika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwa wakati kwenye visiwa 26 vilivyopo katika wilaya hiyo.

Dkt. Burchard ameyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari ambao wapo ziarani mkoani Kagera kuangalia taratibu za usambazaji dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara pamoja na kuzungumza na wateja wa MSD.

"Tunaishukuru sana MSD kwa kazi kubwa ya kufikisha dawa katika maeneo yote ya visiwa licha ya kuwepo kwa changamoto ya usafiri majini, hasa vipindi vya hali mbaya ya hewa kwenye ziwa victoria".

Alisema katika mkoa wa Kagera, wilaya ya Muleba ndiyo ina visiwa vingi lakini serikali kwa kushirikiana na MSD wamefanikiwa kufikisha dawa katika visiwa hivyo kwa ushirikiano mkubwa wa wananchi.

Aliongeza kuwa Halmshauri ya Wilaya ya Muleba ina boti mbili kwa ajili ya kusafirisha wananchi kutoka mwaloni katika Kijiji cha Katunguru kwenda kisiwa cha Mazinga, ambapo pia ina mpango wa kununua boti jingine kwa ajili ya kuongeza nguvu ya usafirishaji.

Akizungumzia kuhusu upatikanaji wa dawa muhimu wilayani humo, alisema hivi sasa hali ni nzuri kwani upatikanaji wake ni kati ya asilimia 90 hadi 98  na kuwa hali hiyo imetokana na ushirikiano uliopo baina ya Serikali na MSD.

"Kuhusu upatikanaji wa dawa kwa kweli hivi sasa hakuna mtu anayelalamika kwani serikali imeongeza fedha katika bajeti yake  karibia mara 10 kutoka sh.bilioni 30 mwaka 2015/16 hadi kufikia sh.bilioni 260 kwa mwaka wa fedha 2018/2019 ambapo kwa wilaya yetu tunatumia zaidi ya milioni 600 kwa ununuzi wa dawa" alisema Burchard.

Alisema wilaya hiyo ina kata 43, wakazi 750,000 wanaotoka kwenye visiwa ishirini na sita, huku ikiwa na vituo vya afya vitano, zahanati 27 na Hospitali teule moja ya Rubya.

Naye Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Kisiwa cha Mazinga, Johanes Sweetbert alisema licha ya usafiri wa majini kuwa na changamoto zake lakini dawa zote muhimu zimekuwa zikipatika na kuwa zahanati hiyo inahudumia vijiji viwili vya Iramba na Rubili ambavyo vina visiwa tisa ambavyo ni Rubili, Iramba, Mjunwa, Runenke, Magege, Garinzila, Kino, Mazinga na Buyonzi.

Alisema mawasiliano mazuri kati ya MSD na serikali yamewezesha dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara kufika kwa wakati ambapo hutumia boti kusafirisha dawa hizo pamoja na wagonjwa waliopewa rufaa kwenda hospitali ya wilaya.

Mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Afya wa Kisiwa cha Mazinga Winfrida Itaganisa amesema kamati ya afya imekuwa ikivuka kwenda Muleba kwa ajili ya kupokea dawa wanazokuwa wameomba na kufanya makabidhiano kabla ya kuvushwa.

Comments