Featured Post

ALAT TABORA YAIPONGEZA UYUI KWA MATUMIZI MAZURI KWENYE UJENZI WA VYUMBA VYA SHULE YA LOLANGULU


Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Lolangulu Wilaya ya Uyui Mkoani Tabora Mary Zacharia akisoma taarifa jana ya ujenzi wa mradi wa vyumba vitatu vya madarasa na uwekaji wa samani kwa gharama ya milioni 38 kwa wajumbe.

Jengo lenye vyumba vitatu vya madarasa na samani zake lilipo katika Shule ya Msingi Lolalungu wilayani Uyui Mkoani Tabora ambalo limegharimu milioni 38 hadi kukamilika.
Wajumbe wa Jumuiya ya Serikali za mitaa Tanzania ( ALAT) Mkoani Tabora wakikagua na kupata taarifa jana ya mradi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa matatu katika Halmashauri ya Wilaya ya Tabora -Uyui kwenye Shule ya Msingi Lolangulu vilivyogharimu milioni 38.
………………………

NA TIGANYA VINCENT, TABORA
Jumuiya ya Serikali za mitaa Tanzania (ALAT) Mkoani Tabora imeipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Tabora -Uyui kufanikisha ukamishaji wa ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa katika Shule ya Msingi Lolangulu kwa kiasi cha shilingi milioni 38.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Tabora Adam Malunkwi  wakati wajumbe wa Jumuiya hiyo wakiwa katika kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo kwa ajili ya kubadilishana uzoefu.
Alisema juhudi za Kamati ya Shule hiyo kwa kushirikiana na wananchi zimewapa fundisho kuwa miradi mingi inaweza kutekelezwa kwa fedha kidogo na kwa ubora wa hali ya juu.
Mbunge wa Jimbo la Manonga Seif Gulamali alisema Vyumba vipya vya madarasa katika Shule hiyo vinapaswa kutumika kama funzo kwa watu wanaosimamia miradi ya ujenzi katika Mkoa  wa Tabora.
Alisema hali hiyo imeonyesha kuwa wakipewa na Serikali shilingi milioni 64 wanaweza kujenga vyumba zaidi ya vinne vikiwa vimekamilika na samani zake kama walivyoona katika Shule ya Lolangulu.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega Kiwele Bundala alimwagiza Mkurugenzi Mtendaji wake kuhakikisha anatuma wataalamu wake wa ujenzi ili waweze kujifunza mbinu walizotumia wakazi wa pale na Kamati yao kufanikisha mradi huo kwa kiwango cha juu.
Alisema hatua ya wao kuweza kujenga vyumba vitatu vikiwa na samani kwa fedha hizo kimeonyesha jinsi miradi mingi ya maendeleo ya wananchi inaweza kufanyika kwa kiwango kidogo cha fedha.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo Margaret Nakainga alisema wataalamu wa ujenzi katika Halmashauri za Mkoa wa Tabora watakiwa waige mfano wa ujenzi wa vyumba vingi vya madarasa kama vya shule ya Lolangulu ambapo vimewekewa na makinga maji.
Alisema hatua itasaidia kupunguza tatizo la maji katika shule kwa ajili ya shule mbalimbali mkoani Tabora.
Awali akitoa taarifa ya mradi Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Lolangulu Mary Zacharia alisema wakazi wa Kijiji cha Ilolangulu waliweza kufanya kazi hiyo baada ya kuunganisha nguvu zao na kuchangishana na kuweza kufikisha jumla ya milioni 11 ambazo ziliwawezesha kufikisha majengo yao katika lenta.
Alisema Serikali baada ya kuona juhudi zao iliwaunga mkono kwa kuwapatia milioni 24 ambazo zimewezesha kuwamalizia kazi zilizokuwa zimebaki na kuwafanikiwa kuwa na madarasa matatu.
Aidha Mary alisema Shule hiyo bado inakabiliwa upungufu mkubwa wa miundombinu ya matundu ya vyoo kwa ajili ya wanafunzi ambapo mahitaji kwa wavulana ni matundu 23 yaliyopo ni manne na kwa upande wa wasichana ni matundu 31 yaliyopo ni nane.
Alisema hali hiyo inasababisha adha kubwa kwa wananfunzi wa shule hiyo.


Comments