- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
NA MWANDISHI MAALUM, DODOMA
WAZIRI
wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ameruhusu uingizaji wa vyavu za
kuvulia samaki na dagaa kutoka nje ya nchi baada ya kubaini kuwa viwanda
vya kuzalisha nyavu hizo vilivyopo nchini kushindwa kuhimili mahitaji
ya soko la ndani na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wavuvi.
Akizungumza
katika kikao cha tathmini ya operesheni Sangara 2018 jijini Dodoma,
Waziri Mpina amemuagiza Katibu Mkuu- Uvuvi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi,
Dk. Rashid Tamatama kuhakikisha kuwa katika kipindi cha siku 14 awe
amekamilisha kupitia maombi na kuruhusu uingizaji wa nyavu hizo kutoka
nje ya nchi. Pia kuweka utaratibu ambao hautaathiri soko la viwanda vya
ndani.
Mbali
na hilo Waziri Mpina ameigiza wizara yake kuandaa mkakati wa kudhibiti
upotevu wa mapato, usimamizi na udhibiti wa rasilimali za uvuvi nchini
ili kuondoa mianya yote ya upotevu wa mapato ya Serikali na kuweka
ulinzi thabiti wa rasilimali za uvuvi.
Pia
ametaka Wizara hiyo kufanya mapitio ya mkakati wa ufugaji wa samaki
kwenye maji, kufufua vituo vya kuzalisha vifaranga na kufanya tathmini
ya uwekezaji wa sekta binafsi na kuainisha mahitaji ya sasa ili kuongeza
uzalishaji utakaochangia kupunguza nguvu ya uvuvi kwenye maziwa na
hivyo kutokomeza uvuvi haramu, kuongeza ajira na upatikanaji wa
malighafi za viwanda nchini.
Akizungumzia
matokeo ya operesheni Sangara 2018, Waziri Mpina alisema jumla ya
watuhumiwa 3,998 walikamatwa kwa makosa mbalimbali na kutozwa faini na
wengine kufikishwa Mahakamani,
nyavu
haramu 575,152, makokoro 11,144 na kamba za kokoro zenye urefu wa mita
859,304 zilikamatwa na kuteketezwa kwa moto.Pia ndoano 1,910, 135
zisizoruhusiwa kisheria ziliharibiwa.
Pia
kilo 359,869 za samaki wasioruhusiwa zilikamatwa na kutaifishwa na
Serikali ambapo kilo 176,780 za samaki wachanga na wazazi ziligawiwa
bure kwenye taasisi mbalimbali zikiwemo shule,magereza,hospitali na watu
wenye mahitaji maalum huku kilo 183,059 za samaki wakavu (kayabo)
pamoja na kilo 5,889 za mabondoziliuzwa kwa njia ya mnada.
Alizungumzia
mafanikio ya operesheni hiyo, Waziri Mpina alisema miezi 6
(Julai-Disemba 2017) kabla ya operesheni Sangara 2018 jumla ya sh.
Bilioni 8.5 zilikusanywa ikilinganisha na jumla ya sh. Bilioni
17.7zilizokusanywa miezi 6 (Januari- Juni 2018) kipindi cha operesheni.
Akitolea
mfano Soko la Samaki la Kirumba jijini Mwanza, Waziri Mpina alisema
mapato yake yameongezeka kutoka sh milioni 206.3 katika kipindi cha
Julai-Dis 2017 kabla ya kuanza operesheni na kufikia sh milioni 848.3
katika kipindi cha Januari hadi Juni 2018 baada ya kuanza operesheni hii
inaonesha kuwa kwa kipindi cha miezi sita mapato katika soko hilo
yameongezeka mara nne.
Alisema
jumla ya makusanyo ya sh.bilioni 26.3 yalikusanywa katika mwaka wa
fedha 2017/2018 ukilinganisha na makusanyo ya jumla ya shilingi bilioni
18.5 yaliyokusanywa katika mwaka wa fedha 2016/2017. Aidha katika
kutekeleza operesheni hiyo jumla ya sh. Bilioni 9.3 zilikusanywa na
Serikali kutokana na tozo,faini na mauzo ya mazao ya uvuvi
yaliyotaifishwa na Serikali.
Pia
mauzo ya sangara nje ya nchi yameongezeka kutoka tani 26,000 mwaka
2016/2017 na kufikia tani 26,700 katika mwaka 2017/2018,urahisi wa
upatikanaji wa samaki wenye ukubwa unaokubalika kisheria, kuongezeka kwa
ukubwa wa samaki wanaochakatwa viwandani huku mahitaji ya vyavu halali
yameongezeka na wananchi kujitokeza kwa wingi kuunga mkono vita ya
uvuvi haramu kwa kuwafichua watu wanaojihusisha na vitendo vya uvuvi
haramu.
Aidha
Waziri Mpina alisema katika operesheni hiyo walibainika baadhi ya
watendaji wa Serikali,Madiwani,Wenyeviti wa Halmshauri,Wabunge
wakihusika kufadhili uvuvi haramu na kwamba tayari majina ya viongozi
hao yameshawasilishwa kwenye vyombo vya dola kwa hatua zaidi huku kwa
upande wa watumishi wa wizara hiyo 12 wakisimamishwa kazi.
Kwa
upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais(TAMISEMI), Suleiman Jafo
aliwaagiza Wakuu wa Mikoa kuwabainisha kwa majina watumishi wote wa
Serikali ngazi ya Serikali za Mitaa waliohusika kushiriki ama kufadhili
uvuvi haramu na kuyafikisha ofisini kwake ili aweze kuwachukulia hatua
kwa mujibu wa sheria.
Waziri
Jafo alisema suala la ulinzi wa rasilimali za Taifa ni watanzania wote
hivyo kama kuna baadhi ya watumishi wanashiriki hujuma katika kipindi
hiki cha Serikali ya awamu ya tano hawatapata nafasi kwani uvuvi ni
miongoni mwa sekta inayotegemewa hasa katika ujenzi wa uchumi wa
viwanda.
‘Kama
Taifa tuna kila sababu ya kuungana katika mapambano ya uvuvi haramu
hasa katika kipindi hiki cha uchumi wa viwanda,ofisi yangu haitasita
kuwachukulia hatua kali za kinidhamu kwa watumishi wote watakaobainika
kutajwa kushiriki uvuvi haramu”alisema Jafo.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge,Kilimo, Mifugo na Maji, Mahmoud Mgimwa
alimtaka Waziri Jafo kusimamia kikamilifu agizo lake kwani baadhi ya
watendaji walioko chini ya wizara yake ndio wafadhili wakubwa wa mtandao
wa uvuvi haramu na kukwamisha juhudi za Serikali za kumaliza tatizo
hilo.
Mgimwa
alisema mapato mengi ya uvuvi yalikuwa yanaishia mifukoni mwa watu
wachache lakini kwa juhudi na ubunifu mpya uliofanywa na Waziri Mpina na
wizara yake umewezesha kukusanya sh. bilioni 9.3 katika kipindi cha
miezi sita na fedha hizo zimeingia mfuko mkuu wa Taifa na kwenda
kusaidia kwenye ununuzi wa ndege,ujenzi wa reli, umeme,maji,elimu bure
na uboreshaji wa sekta ya afya.
Kamanda
Mkuu wa Operesheni Sangara 2018, Emanuel Bulai alisema operesheni hiyo
imebaini kuwepo uvunjifu mkubwa wa sheria ikiwemo matumizi ya zana
haramu za uvuvi, utoroshaji mkubwa wa mazao ya uvuvi na raia wa kigeni
kuingia nchini na kufanya biashara ya samaki na mazao na yake bila
kufuata Sheria za nchi.
Comments
Post a Comment