Featured Post

WAZIRI AKEMEA WANAUME KUTOA TALAKA KWA SIMU



NA SALUMVUAI, WHUMK
WAZIRI wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Moudline Castico, amekemea tabia ya baadhi ya wanaume kuwataliki wake zao kwa ujumbe wa simu.

Akizungumza na wanachama wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT) wa Chama cha Mapinduzi katika tawi la Kiembesamaki, Waziri Castico amesema kitendo cha kutaliki mke kwa SMS ni dharau na udhalilishaji.
Waziri huyo alieleza masikitiko yake kwamba baadhi ya wanaume wanaofanya hivyo, ni wale waliowezeshwa na wake zao wanaojituma, ambapo hali za waume hao zilikuwa duni wakati wakioana.
Alisema wapo wanaume wanaosaidiwa kujenga nyumba na hata kununuliwa magari na wake zao, lakini hatimaye wanawatoa thamani na kuwanyanyasa baada ya kupata wanawake wanaowaona ni wazuri zaidi.
Alieleza kuwa jambo baya zaidi, ni kuacha kuwashughulikia watoto kwa kuwanyima huduma na matunzo, hali inayowasukuma kuzurura mitaani na kuingia katika ajira mbaya na hatari ya kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji.
Waziri huyo alisema dini zote zinaitambua ndoa kuwa ni kitu cha heshima na ina maadili yanayopaswa kufuatwa na watu wanaoamua kushirikiana kimaisha.
Hata hivyo, alisema iwapo kunatokezea sababu ya wanandoa kutengana, lazima waachane kwa wema, heshima na mafahamiano ili ihsani waliyokuwa nayo wakati wakiwa pamoja iendelee na hasa wanapokuwa wamejaaliwa kupata watoto.
“Kuacha kuna taratibu zake, akinababa mnapowapenda wake zenu muwe na busara, mnapoanza pamoja lazima muende pamoja kama unavyombembeleza siku ya kwanza. Sio keshakuchumia mali zako, ushakuwa na uwezo, kakunulia kigari unampelekea talaka kwenye simu,” alitanabahisha.
Aidha, aliwanasihi akinamama wawe waaminifu kwenye ndoa zao hata pale waume zao wanapokengeuka, badala ya kutaka kulipa kisasi, akisema kufanya hivyo kutawashushia hadhi na kujenga taswira mbaya mbele ya watoto wao na jamii.
Alisema, ikiwa hakuna njia yoyote ya kuinusuru ndoa isivunjike, suala hilo lifanywe kwa taratibu zake, na kutaka wenza wajadiliane na kupanga namna watakavyolea na kuwashughulikia watoto wao, na vipi watanufaika kwa mali walizochuma pamoja.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki, Mahmoud Thabit Kombo, alisema wanawake ni wanaopaswa kuengwaengwa kama mboni ya jicho badala ya kuwanyanyasa kwani daraja yao kwa Mwenyezi Mungu ni kubwa sana.
Alisema, bila ya msaada, nguvu na imani ya mwanamke, wanaume wasingeweza kupata mafanikio wanayojivunia katika maisha yao, hivyo lazima waoneshe shukurani kwao kwa kuwatunza na kuwapa heshima wanayostahiki.
“Wanawake ni mama zetu, na sote tunaujua uzito wa kubeba mimba na uchungu wa uzazi ambapo wakati wa harakati za kujifungua, mama anakuwa baina ya uhai na kifo. Tutafute pepo kwa kuwatunza mama zetu,” alisema.
Thabit ambae pia ni Waziri waHabari, Utalii na Mambo ya Kale, aliwaahidi wanachama wa UWT pamoja na wanawake wengine wa Jimbo la Kiembesamaki, kwa kushirikiana na viongozi wenza kwa jimbo, wataendelea kuyatafutia ufumbuzi matatizo yanayowakabili hatua kwa hatua.
Hata hivyo, aliwashauri kutumia maarifa na taaluma ya kila mmojawao, kubuni miradi ya kimaendeleo yenye tija ili kuwapa moyo viongozi wao kuwasaidia pale wanapokwama.

IMETOLEWA NA WIZARA YA HABARI, UTALII NA MAMBO YA KALE-ZANZIBAR
16 JULAI, 2018

Comments