Featured Post

SERIKALI KUKUZA UTALII KUPITIA MCHEZO WA GOLF – DK. KIGWANGALLA

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akimkabidhi Mcheza Golf mashuhuri zaidi duniani, Jack William Nicklaus wa nchini Marekeni zawadi ya kinyago cha Makonde walipoagana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu J.K Nyerere Jijini Dar es Salaam baada ya kuhitimisha ziara yake ya siku 10 ya kutembelea vivutio vya utalii hapa nchini.
Na Hamza Temba-WMU
........................................................................
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla amesema Serikali itatumia fursa ya ujio wa Mcheza Golf mashuhuri zaidi duniani, Jack William Nicklaus kutoka nchini Marekeni kubuni viwanja vya mchezo huo karibu na maeneo ya vivutio vya utalii nchini ili kuvutia watalii wengi wa kimataifa na hivyo kukuza pato la sekta hiyo.

Dk. Kigwangalla amesema hayo jana mara baada ya kumuaga mchezaji huyo katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu J.K Nyerere Jijini Dar es Salaam alipokuwa akirudi nchini kwao baada ya kumaliza ziara yake ya siku kumi yeye na familia yake katika vivutio mbali mbali vya utalii hapa nchini.

“Tutatumia utaalamu na uzoefu wake kwenye mchezo wa Golf kwa kumtaka aje na kampuni yake atusaidie kutengeneza plan (mpango) ya kujenga viwanja vya golf.

“Amedesign viwanja zaidi ya 300 kwenye nchi zaidi ya 50 duniani na nchi hizo zimefaidika, amesema katika project zake zaidi ya asilimia 90 zinafanya vizuri pamoja na kwamba ni uwekezaji wa gharama kubwa bado imelipa kwa kiasi kikubwa na hakuna hata kiwanja kimoja kimepata hasara na vimekuwa vinasaidia kukuza utalii katika nchi hizo.

“Lengo letu ni kutengeneza ukanda maalum wa viwanja vya golf ambao utakuwa na viwango vya kimataifa na utavutia wacheza Golf kutoka nchi mbalimbali duniani, kwahiyo hii ni aina nyingine ya utalii wa watu wenye uwezo ambao wataleta pesa nyingi kwa wakati mmoja.

 “Tutaendelea kuwa na mawasiliano nae na kampuni yake ili tuweze kuona anawezaje kutusaidia na sisi walau tuwe na hiyo plan (mpango) lakini pia tukapata wawekezaji wakaja kuwekeza kwenye viwanja vya golf vitakavyojengwa karibu na fukwe, karibu na mito au hifadhi za Taifa ambapo tutavutia sio tu watalii ambao wanaokuja  kufanya utalii wa wanyamapori au beach lakini tutavutia watalii wanaokuja mahsusi kwa kwa ajili ya utalii wa golf” alisema Dk. Kigwangalla.

Wakati huo huo Dk. Kigwangalla amesema Serikali itaendelea kuheshimu na kujali maslahi ya wageni mashuhuri wanaokuja nchini ikiwemo ya usiri wa safari zao na kwamba atakayetaka aje kimya kimya na aondoke kimya kimya atapata heshma hiyo na atakayekubali kuwa wazi naye pia atapata heshma hiyo.

Kwa upande wake Jack Nicklaus alisema amefurahishwa sana na vivutio mbalimbali vya utalii alivyovishuhudia katika safari yake hapa nchini pamoja na ushirikiano na ukarimu mzuri kutoka kwa watanzania na ameahidi kuwa balozi wa utalii wa Tanzania huo aendako.

Jack Nicklaus ndiye mchezaji mwenye tuzo nyingi kuliko wachezaji wengine wa mchezo huo hapa duniani kwa sasa, ameweka rekodi ya kushinda mashindano ya kulipwa 117 na mashindano makubwa 18 (major champions). 
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiagana na Mcheza Golf mashuhuri zaidi duniani, Jack William Nicklaus wa nchini Marekeni katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu J.K Nyerere Jijini Dar es Salaam baada ya kuhitimisha ziara yake ya siku 10 ya kutembelea vivutio vya utalii hapa nchini.
  Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiwa na Mcheza Golf mashuhuri zaidi duniani, Jack William Nicklaus wa nchini Marekeni katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu J.K Nyerere Jijini Dar es Salaam muda mfupi kabla ya kuondoka kurudia kwao baada ya kuhitimisha ziara yake ya siku 10 ya kutembelea vivutio vya utalii hapa nchini.
  Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla na Mcheza Golf mashuhuri zaidi duniani, Jack William Nicklaus wa nchini Marekeni wakitumbuizwa na kikundi cha ngoma katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu J.K Nyerere Jijini Dar es Salaam muda mfupi kabla ya kuondoka kurudia kwao baada ya kuhitimisha ziara yake ya siku 10 ya kutembelea vivutio vya utalii hapa nchini.
  Picha ya pamoja ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, Mcheza Golf mashuhuri zaidi duniani, Jack William Nicklaus wa nchini Marekeni na familia yake na uongozi wa Bodi ya Utalii Tanzania ukiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi, Jaji Mst. Thomas Mihayo muda mfupi kabla ya ugeni huo kuondoka na kurudi kwao.

Comments