Featured Post

MPINA AITAKA SEKTA BINAFSI ZINAZOSHUGHULIKA NA BIASHARA YA MIFUGO KUCHANGIA KWENYE UCHUMI WA VIWANDA NCHINI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Joelson Mpina (aliyesimama) akizungumza kwenye kikao cha wadau wa maziwa na ngozi kulia ni Naibu wake Mheshimiwa Abdallah Ulega kushoto ni Katibu Mkuu Mifugo Mstaafu Dkt. Maria Mashingo. Picha na John Mapepele
Na John Mapepele, Dodoma
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ameitaka Sekta Binafsi nchini inayojishughulisha na biashara ya mifugo na mazao yake kujitathmini na kurekebisha kasoro zilizopo miongoni mwao ili kuiwezesha sekta hiyo kutoa mchango unaostahili katika uchumi wa nchi hasa katika kipindi hiki cha Tanzania ya Viwanda.

Amesema Serikali ya awamu ya tano inathamini na kutambua mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya nchi na ndio maana iko tayari wakati wowote kushughulikia changamoto zilizopo ili kuweka mazingira wezeshi ya kufanya biashara nchini.
Akizungumza katika kikao cha wadau wa tasnia ya Nyama, Maziwa na Ngozi jijini Dodoma, Waziri Mpina ameelezea kusikitishwa kwake na kitendo cha wadau wa sekta binafsi kutopendana na kuhujumiana na ndio sababu ya Serikali kushindwa kutatua kwa wakati changamoto zinazoikabili sekta hiyo.
Waziri Mpina amesema baadhi ya wadau wa sekta binafsi wamekuwa wakiwayumbisha watendaji wa Serikali na watunga sera na sheria kwa kila mmoja kuvutia upande wake huku wakiwa na mitazamo tofauti hata kama wako kwenye tasnia moja huku baadhi yao wakipenda njia za mkato na kushindwa kufuata taratibu na sheria zilizowekwa jambo ambalo limekuwa likisababisha ucheleweshaji wa maamuzi serikalini.
Pia ameeleza kuchukizwa na kitendo cha wenye viwanda vya mazao ya mifugo kuwanyonya wafugaji kwa kununua bei ndogo mazao yao akitolea mfano maziwa na ngozi ambapo kwa upande wa maziwa wenye viwanda hununua lita moja kwa sh 700 na baada ya kusindika wanauza sh 3,500 kwa lita, huku wenye viwanda vya ngozi nao wakinunua kwa mfugaji kipande cha ngozi kwa sh 1,000 na baada ya kuichakata wao wanauza kwa zaidi ya sh 60,000 jambo ambalo Serikali haiwezi kukubali liendelee.
Mpina alisema wako baadhi ya wenye viwanda vya maziwa,nyama na ngozi ambao hawana hata shamba la mifugo wala maeneo ya kuhifadhia hali inayoifanya Serikali kuamini kuwa bado sekta binafsi nchini haijaweza kujipanga vya kutosha kuwekeza katika sekta hiyo.
Alisema ni lazima sekta binafsi na yenyewe ifanye mageuzi ya kiuendeshaji na kimfumo ili kwenda sambamba na mabadiliko yanayofanywa na Serikali ili kuiwezesha sekta hiyo kukua kwa haraka na kutoa mchango unaostahili kwa maendeleo ya Taifa.
Mpina alisema tayari Serikali iko kwenye hatua za mwisho za kupitia upya changamoto zote zinazoikabili sekta binafsi ikiwemo za utitiri wa kodi na tozo mbalimbali zinazotozwa kutoka kwenye taasisi mbalimbali za Serikali ili kuharakisha ufanyaji kazi kwenye sekta hiyo.
Kuhusu suala mikopo na mitaji kwa wawekezaji wa mazao ya mifugo amesema Serikali itahakikisha Benki ya Maendeleo Kilimo nchini inakopesha wadau hao ili kuongeza mnyororo wa thamani wa bidhaa wanazozalisha na kukuza uchumi kwa haraka kwani kwa muda mrefu taasisi nyingi za kifedha zimekuwa zikiwabagua wafugaji na wavuvi.
Mpina alisisitiza kuwa ni mategemeo ya Serikali kuona baada ya miaka mitano Tanzania iweze kushindana na dunia katika uzalishaji wa ya maziwa na bidhaa nyingine za mifugo kutokana na fursa kubwa zilizopo nchini.
Aidha Waziri Mpina alisema hatua zinazochukuliwa na Serikali kuzuia biashara holela ya mazao ya mifugo nchini hazilengi kumkomoa mtu bali kuiwezesha sekta binafsi nchini iweze kufanya biashara vizuri na kwa ushindani sawa na waingizaji bidhaa hizo kutoka nje nchi.
Pia Waziri Mpina amesema kutokana na kuripotiwa kuwepo mlundikano wa ngozi katika maghala yaliyopo nchini na kukosa soko la kimataifa amelazimika kuunda kamati ndogo ili kupitia na kufanya tathmini ya kina kuhusu kasoro zilizopo kwenye tasnia hiyo ili kuwepo uelewa wa pamoja baina ya Serikali na wadau wa ngozi, Kamati hiyo itahusisha Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji pamoja na Wizara ya Fedha.
Hivyo aliwahakikishia wawekezaji hao kuwa pamoja na changamoto zote zilizopo kwenye sekta binafsi nchini Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Pombe Magufuli iko pamoja nao katika kutatua shida zote na ndio maana Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeitisha mkutano huo ili kuwasikiliza na itaendelea kufanya hivyo mara kwa mara.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Mifugo, Dk. Maria Mashingo alisema lengo la mkutano huo ni kutambua changamoto zilizopo kwenye mnyororo wa thamani katika sekta ya mifugo ili kuweiwezesha sekta hiyo kuzalisha bidhaa zenye ubora na kukuza pato la Taifa
Pia aliwataka wadau wa sekta ya maziwa kwenda kujifunza katika Kiwanda cha Maziwa cha Tanga Fresh ili kuwezesha kuanzisha vikundi vya wafugaji wadogo ili kuwa na uhakika wa ukusanyaji wa maziwa.
Naye Meneja Mkuu wa Tanga Fresh, Michael Karata aliomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuondoa kodi ya ongezeko la thamani VAT ili kuiwezesha sekta hiyo kukuwa kwa haraka na kuweza kushindana na mataifa mengine.
Alisema Serikali ikiweka kiwango cha kodi sifuri gharama za uzalishaji zitapungua na kuweza kuuza bidhaa zao kwa bei nafuu tofauti na sasa ambapo huuza lita moja ya maziwa ya muda mrefu kwa sh 3,500.

Comments