- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Mkuu wa Mkoa wa Tabora
Aggrey Mwanri akifungua warsha ya wanakamati wa Kamati ya kukomesha ukatili wa
kijinsia Mkoani Tabora wakati wakijadiliana jinsi ya kutokemeza vitendo vya
ukatili wa kijinsia kwa watoto, ndoa za utoto, na ukatili kwa wanawake na
baadhi ya waume ikiwa ni njia ya kupunguza maambukizi mapya ya UKIMWI.
NA TIGANYA VINCENT
MKOA wa Tabora ni
miongoni mwa maeneo hapa nchini ambayo bado yakabiliwa na kiwango cha juu cha
ukatili wa kijinsia ikiwemo ndoa na mimba za utotoni, pamoja na vipigo kwa
wanawake kutoka kwa waume zao na baadhi ya wanaume wachache kupigwa na wake
zao.
Hali hiyo imekuwa ikijidhihirisha katika maeneo mbalimbali
kwa mfano mwaka jana kulitokea matukio makubwa na kusikitisha ikiwemo mauaji ya
wanawake watano wilayani Nzega kwa kupigwa na kuchomwa moto na kule Wilayani
Uyui wanawake wanne walinusurika kuwawa lakini wakiwa tayari wamepigwa na
kudhalilishwa kijinsia.
Tukio jingine lilitokea hivi karibuni ambapo Jeshi la Polisi
katika Wilaya ya Kaliua kwa kushirikiana na wananchi wenye huru lilifanikiwa
kuwaokoa wananawake wane ambao walikuwa wachomwe moto kwa imani ya kishirikina
Matukio hayo hayaishi katika mauaji na vipigo kwa wakinamama
bali pia kuna kiwango kikubwa cha mimba za utotoni kwa watoto walio chini ya
miaka 18.
Mgamga Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Gunini Kamba anasema
jumla ya watoto 11,332 walio chini ya miaka 18 mkoani hapa walipata
ujauzito katika kipindi cha
Januari hadi Juni mwaka huu.
Kufuatia matukio hayo na mengine ambayo yanahusu unyanyasaji
wa kijinsia, Mradi wa Sauti unawakutanisha Wadau wa Kamati ya kukomesha ukatili
wa kijinsia Mkoani Tabora ili kujadiliana jinsi ya kutokemeza vitendo vya
ukatili wa kijinsia kwa watoto, ndoa za utoto, na ukatili kwa wanawake na
baadhi ya waume ikiwa ni njia ya kupunguza maambukizi mapya ya UKIMWI.
Akifungua warsha hiyo ya siku moja Mkuu wa Mkoa wa Tabora
Aggrey Mwanri anasema njia ya kwanza ya kutokomeza ukatili kwa wanawake na
watoto ni kuwaelimisha na kuwawezesha kiuchumi ili waweze kuwa na sauti ya
kufanya maamuzi katika masuala mbalimbali yanayowahusu wao na jamii zao.
Anasema kuwa familia ambazo zimepiga hatua kiuchumi na
kielimu hazina tena na mila potofu ya kuwaozesha watoto wao katika umri mdogo
na kuwapiga wanawake.
Mwanri anasema kuwa hali duni ya kiuchumi na maisha duni kwa
akinamama yamekuwa yakisababisha ongezeko la ukatili wanaofanyiwa wanawake na
wenza wao pamoja na unyanyasaji na uyonyaji wa aina nyingine.
“Kipato duni ndio kinawafanya baadhi ya wanawake kupika
chakula kwa kutumia kuni na hivyo kusababisha macho kuwa mekundu na hapo ndio
tatizo linapoanzia kwa wanajamii ambao wana imani potofu ya kudhani kuwa na
macho mekundi ni dalili za uchawi , kumbe yametokana maisha duni
yanayosababisha matumizi ya kuni zaidi kama nishati ya kupikia…imi naona tukiweza
kueleza tatizo hilo la umaskini na kuliondoa kwa akina mama na kuwasaidia
kujikwamua kielimu na kiuchumi tutapunguza ukatili unaosababishwa na mila
potofu zinazotokana na ujinga” anasema.
Anasema pia ni vema jamii ikawapa fursa ya ajira wanawake
ili waweze kuwa na kipato ambacho kitawasaidia wao katika kupunguza utegemezi
kwa wanaume.
Mwanri anasema kuwa
upande wa Serikali inajitahidi kutoa elimu na kutumia sheria zilizopo
katika kuzuia ukatilii wa kijinsia na pia imeweka mazingira ya kuwawezesha
kupitia vikundi watakavyojiunga pamoja katika kujiendeleza kwa kuziagiza
Halmashauri zote hapa nchini kuhakikisha zinatenga asilimia 10 ya mapato ya
ndani kwa ajili ya kuwapa mikopo wanawake, vijana na walemavu.
Afisa Mradi wa Masuala ya kupinga Ukatilii wa Kijinsia
kutoka Shirika la Jhpiego Shangwe Kimathi anasema warsha hiyo ililenga
kuwajengea uwezo wa wadau mbalimbali ili wanaporudi katika maeneo yao wawe na
mbinu mpya za kupambana na ukatilii wa
kijinsia kwa wanawake na watoto ikiwa ni sehemu ya kupunguza maambukizi mapya
ya VVU.
Anasema baadhi ya watoto na wanawake wajikuta wakipata
maambukizi ya VVU kwa sababu ya kubakwa, kulazimishwa kuolewa katika umri
mdogo, kutumikishwa katika biashara ya ukahaba na katika kumbi za starehe.
Mrakibu wa Polisi kutoka Mkoa wa Tabora (SP)Ali Hamad
anawataka watu wote wanaotendewa ukatili kuwa wazi kuwafichua waliowafanyia
vitendo hivyo ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Anasema mara nyingine familia ya wahanga wanapatama na upane
wa familia ya mtuhumiwa na hivyo kupoteza ushahidi ambao ungesaidia kumtia
hatiani mtuhumiwa wa kitendo cha ukatili wa kijinsia.
Naye Koplo Adelina Mgoha kutoka Dawati la Kijinsia Wilaya ya
Tabora anatoa wito kwa wanaume ambao wanafanyiwa vitendo vya kikatili na wenza
kutoona aibu kutoa taarifa ili waweze kusaidia badala ya kukaa nalo moyoni.
Anasema woga wa baadhi ya wanaume ndio umekuwa ukisababisha baadhi ya wanaume
ambao wanafanyiwa vitendo vya kikatili na wake zao kunywa sumu, kujiua na
kufanya mauaji kwa watu ambao wanawadhani ni adui zao.
Adelina anasema hatua hizo zinaacha simanzi kubwa kwa
wanafamilia na wakati mwingine kujenga uadui zaidi kati ya familia ya mwanamke
na ya mwaume na hivyo kusababisha watoto kubaki njia panda.
Kwa upande wa suala la ushahidi anasema kuwa wakati mwingine
inakuwa vigumu kupata ushahidi kutoka kwa wat waliofanyiwa vitendo vya kikatili
kwa sababu wanakuta wameogeshwa na kupoteza ushahidi.
Aidha Mradi wa SAUTI kupitia Shirika la Jhpiego kusaidia
katika ujenzi wa vyumba katika vituo vya Polisi ambavyo vitatoa usiri na kutoa
uhuru kwa mtu aliyefanyiwa ukatili wa kijinsia kuweza kujieleza vizuri na
kutokuwa na wasiwasi wa kusikilizwa na kila mtu hata ambaye hausiki na Dawati.
Naye Mwanasheria kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora
Richard Lugomela anasema ukatilii wa kijinsia unaweza kuwa kimwili,
kisaikolojia, kingono, kiuchumi na unaotokana na mila potofu, mfumo dume, ndoa
za utotoni, ulevi kupindukia, uasherati , matumizi mabaya ya fedha , umaskini,
wivu na matumizi mabaya ya madaraka.
Mwanasheria huyo anasema ukatili wa kijinsia unasababisha
kupotea kwa amani na upendo ndani ya familia, kujenga uhasama,kupoteza nguvu
kazi ya jamii, ongezeko la watoto mitaani, maendeleo duni na kupoteza
rasilimali na kuongezeka kwa umaskini.
Lugomela anasema ni vema yanapojitokeza matendo ya ukatili
wa kijinsia taarifa zitolewe mapema katika vituo vya polisi kupitia dawati la
jinsia, Afisa mtendaji wa Kata, Afisa maendeleo ya jamiii, Afisa ustawi wa
Jamii na kwenye vyombo vya msaada wa kisheria (paralegal)
Anawataka wahanga wa vitengo ukatili wa kijinsia wanatakiwa
kufuata taratibu zote zinazotakiwa wanaporipoti tukio hilo ili kutopoteza
ushahidi ambao ndio utamtia hatiani mtuhumiwa.
Lugomela anasema wahanga wengine wamekuwa wakipelekea hati
maalumu ya Polisi kwa ajili ya kupata matibabu(PF3 ) ikiwa haina mhuri na hivyo
kuonekana kama sio nyaraka halali.
Anaongeza kuwa wengine wamekuwa wakiwacha kutoa taarifa
kwa viongozi walio karibu nao kama vile
Mwenyekiti wa Mtaa au Kitongoji. Kijiji
na Mtendaji wa Kijiji.
Lugomela anatoa wito kwa ndugu wa wahanga wa vitendo vya
ukatili wa kijinsia kufuata taratibu wakati wanapotoa taarifa za tukio la
ukatili waliofanyiwa ili ziweze kumsaidia Hakimu kutoa maamuzi ambayo yanao
ushahidi wa kutosha na usio kuwa na shaka.
Anasema kwenye Ibara ya 12-29 za Katiba ya Jamuhuri ya
Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977
inapinga ukatili wa kijinsia kwani inatoa kwa kuwa inatoa Haki ya kuishi
, Haki ya kutokubaguliwa ,Haki ya kumiliki mali na Haki ya kupata ujira.
Lugomela anaongeza kuwa Sheria ya adhabu sura namba 16 ya
mwaka 2002 kifungu cha 241 inatoa adhabu ya kifungo cha miaka mitano kutokana
na Shambulio la kimwili na kwa mujibu wa kifungu cha 169 A kinalezea kuwa,
ni kosa la jinai kwa mtu yeyote kumtesa au kumtekeleza mtoto na akipatikana na
hatia atawajibika kwa adhabu ya miaka 5 na faini isiyozidi laki tatu.
Anasema kuwa Kifungu cha 131 cha Sheria ya adhabu kikisomwa
pamoja na Sheria ya Makosa ya kujamiana, ubakaji adhabu yake ni miaka 30.
Kwa upande wa Sheria ya Ndoa sura ya 29 ya mwaka 1971 kifungu
cha 66 kinakataza ukatili baina ya wanandoa na Sheria ya Ardhi Na. 4 na 5 za mwaka 1999 kifungu cha 3(2) kinatoa
usawa wa kumiliki ardhi. Pia sheria ya usimamizi wa miradhi sura ya 352 ya
mwaka 2002 ni haki ya mtoto(wakike/wakiume) kurithi mali za wazazi wake pale
watakapokuwa wamefariki.
Pia Sheria ya Mtoto Na.21 ya 2009 kifungu cha 10 kinatamka
kwamba ni haki ya mtoto kufurahi mali iliyoachwa na wazazi wake.
Kwa mujibu wa kifungo cha 62 cha Sheria ya Watu wenye
ulemavu Na. 9 ya mwaka 2010 kinatoa adhabu ya faini isiyopungua milioni mbili
na isiyozidi milioni 20 kwa kusababisha
uelemavu, kuweka mazingira ya
ubaguzi ama kukaidi matakwa ya watu wenye ulemavu.
Lugomela anafafanua kuwa katika Kifungu cha 21 cha Sheria ya
UKIMWI, 2008 kinapiga marufuku ukatili wa kiafya kwa kushindwa kumfahamisha
mwenza wako au yeyote ambae una mahusiano naye ya kimapenzi kuwa una Virusi vya
UKIMWI.
Kifungu cha 22 cha Sheria ya Elimu mwaka 1978
kwa marekebisho ya mwaka 2016kinatoa Adhabu ya miaka 30 kwa mtu
atakaepatikana na kosa la kuoa mwananfunzi au kumpa mimba. Hata hivyo, kifungu
hiki kimezungumzia mtu atakaesaidia kufanikisha kuolewa/kuoa kwa mwanafunzi
adhabu yake ni kifungo cha miaka mitano
au faini isiyo pungua milioni tano au vyote kwa pamoja.
Anasema hakuna sheria ya moja kwa moja ya kukabiliana na
suala la ukatili wa kijinsia Tanzania, kwa kuwa
ukatili wa kijinsia upo wa aina mbalimbali na ni kutoakana na aina hizo, kumepelekea sheria
hizi kuwa nyingi kulingana na aina ya unyanyasaji.
Aidha, Lugomela anasema zipo sheria ambazo bado
zinamapungufu mbali mbali yakiwemo
kupitwa na wakati na kutokuendana na hali halisi ya maisha yetu ya sasa. Mfano,
sheria ya ndoa Na. 29 ya mwaka 1971 bado inatoa wigo wa kwa watoto chini miaka
18 kuolewa kwa idhini ya wazazi.
Naye Meneja wa Mradi wa SAUTI kutoka Shirika la Jhpiego
Flavian Ngeni anasema mradi huo unajitahidia kuhakikisha unashirikiana na wadau
mbalimbali katika kukabiliana na ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto na
pia kupunguza maambukizi ya VVU hapa nchini.
Anasema Mradi huo unaratibiwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za
MItaa(TAMISEMI) na kutekelezwa na Shirika
la jhpiego kwa kushirikiana na mashirika
ya Engender Heath, Pact Tanzania na NIMR
tawi la Mwanza chini ya ufadhili wa
Mfuko wa dharula wa Rais wa Marekani wa kupamana na UKIMWIkupitia Shirika la
Maendeleo la Kimataifa la Watu wa Marekani (USAID) .
Mradi huo ambao ni miaka mitano unatekelezwa katika mikoa 14
na Halmashauri 51 ya Tanzania Bara.
Comments
Post a Comment