- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Profesa Simon Msanjila akikabidhi zawadi kwa Prosper Gasper na Erick Simon kutoka Shule ya Sekondari St. Jude's jijini Arusha baada ya kuibuka washindi wa jumla wa Mashindano ya Wanasayansi Chipukizi (YST) yaliyofanyika Agosti 8-9, 2017 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Na Daniel Mbega
SHIRIKA la Young
Scientists Tanzania (YST) linaandaa kwa mwaka wa nane sasa Maonyesho ya Sayansi
yanayowahusisha wanafunzi wa shule za sekondari kote nchini ambayo yatafanyika
kuanzia Jumatano, Agosti Mosi hadi 2, 2018 kwenye Kituo cha Mikutano cha
Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Kama ilivyokuwa kwa
miaka mitatu iliyopita, maonyesho ya mwaka 2018 yatawashirikisha jumla ya
wanafunzi 200 na walimu 100 kutoka katika shule 100 za Tanzania nzima - yaani
Bara na Visiwani.
Wanafunzi na walimu wa
shule hizi wamegharimiwa kila kitu - kuanzia nauli za kutoka huko makwao,
malazi na chakula - hali inayotokana na ufadhili kutoka kwenye taasisi
mbalimbali zinazoguswa na ubunifu wa watoto wetu katika kuandaa kizazi cha
wanasayansi.
Haijawekwa wazi ni shule
zipi zitakazoshiriki, lakini kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtandaji wa YST, Dkt.
Gozbert Kamugisha, kunatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa katika kazi za ubunifu
za mwaka huu kutokana na wanafunzi na walimu kila mwaka kuboresha kazi zao kwa
kurekebisha makosa yaliyotokea huko nyuma.
Lengo kubwa la
mashindano ama maonyesho hayo ya sayansi kwa wanafunzi ni kuhamasisha watoto
wetu waweze kuyapenda masomo ya sayansi licha ya ukweli kwamba, mitaala yetu
haitoi nafasi kwa watoto kufanya ubunifu.
Na ubunifu uliopo hapa
kwa wanasayansi hao chipukizi ni kazi zilizo katika nyanja mbalimbali za
sayansi kama Kemia, Fizikia na Hisabati, Baolojia na Mazingira, Sayansi ya
Jamii na Teknolojia.
"Ugunduzi wa
wanasayansi chipukizi umejikita zaidi katika kutafuta mbinu za kukabiliana na
changamoto za maendeleo kwenye afya, kilimo na usalama wa chakula, usalama wa
mawasiliano na uchukuzi, nishati na mazingira, elimu, mahusiano ya kijamii na
matatizo ya kijamii," anasema Dkt. Kamugisha.
Wanasayansi hawa
chipukizi hawaji bure, kwani miongoni mwao watakaoshinda watazawadiwa fedha
taslimu, medali na vifaa vya maabara na wanne kati yao watapewa ufadhili wa
kusomeshwa mpaka elimu ya chuo kikuu, ufadhili ambao hutolewa na taasisi ya
Karimejee Jivanjee Foundation ili waweze kuendelea kuimarisha vipaji vyao vya
ugunduzi wa kisayansi.
"Maonyesho ya
wanasayansi chipukizi ya 2018 yanalenga kuwahamasisha wanafunzi wa sekondari
kupenda sayansi na ugunduzi na kujenga utamaduni wa kisayansi kwa vijana wa
Kitanzania, ni fursa nzuri kwa wanafunzi kuonyesha njia madhubuti za
kukabiliana na changamoto za kijamii na kiuchumi," anasema Dkt. Kamugisha.
Tanzania ya Viwanda
Ukiacha malengo hayo
yanayoelezwa na waandaaji, lakini taswira chanya iliyopo sasa inaonyesha
yanakwenda sambamba na Sera ya Serikali ya kuifanya Tanzania ya Viwanda.
Wakati maonyesho haya
yanaanza mwaka 2011, hakukuwa na mtazamo wowote wa kusema kwamba nchi yetu
inaweza kubadilishwa kuwa ya viwanda zaidi ya wahusika kulenga kutengeneza
kizazi cha wanasayansi.
Hata hivyo, tangu
Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani na kuja na kauli mbiu ya
'Tanzania ya Viwanda', ni dhahiri kwamba maonyesho haya sasa yanafaa kutiliwa
mkazo na kuungwa mkono na wadau wote wapenda maendeleo ili Tanzania ianze sasa
kuwaandaa wataalamu wake ambao ndio watakaoijenga Tanzania ya Viwanda.
Ni wazi kwamba,
wanafunzi waliotangulia miaka nane iliyopita kupata ufadhili, hivi sasa wengine
watakuwa wanasomea shahada za uzamivu kama waliendelea moja kwa moja, japo
walio wengi wamehitimu shahada za kwanza na uzamili.
Hawa wasomi kama
watajengewa mazingira mazuri na wezeshi kwa kuzingatia sera nzuri, hakika
wanaweza kuwa wataalamu tunaowahitaji kwa sababu hatuwezi kuzungumzia Tanzania
ya Viwanda bila kuwa na wataalamu, hata kama tutakuwa na malighafi za kutosha.
Washindi wa mwaka 2017,
kwa mfano, Prosper Gasper na Erick Simon, wanafunzi wa shule ya sekondari ya
St. Jude’s kutoka Arusha, ambao wazo lao la “Kutumia Simu za Mkononi kama Mfumo
wa Kubaini Ajali za Moto” (The Use of Mobile Network as a Fire Alert System)
liliyashinda mawazo mengine 99 yaliyowasilishwa mwaka huo, walifanya vizuri
hata kimataifa baada ya kuibuka washindi wa kwanza katika Mashindano ya Ubinifu
wa Sayansi na Teknolojia barani Afrika yaliyofanyika jijini Johannesburg, Afrika
Kusini 2017, Tanzania ikishiriki kwa mara ya kwanza kabisa.
Vijana hao walibuni mfumo
wa kubaini, kwa kutumia simu za mkononi, uwepo wa moto pamoja na wizi kwa
kuweka ving’amuzi vinavyoweza kubaini mapema hata kama mtu hayuko nyumbani au
akiwa amelala.
YST ni kama jiwe la msingi
katika kukuza vipaji vya wanasayansi nchini, na maonyesho haya yameonyesha ongezeko
kubwa la ushiriki wa shule za sekondari kutoka shule 4 mwaka 2011 hadi 100
mwaka sasa, hatua ambayo imetokana na hamasa ya kuendeleza masomo ya sayansi
kwa shule mbalimbali za sekondari nchini.
Kwa maana hiyo, baada ya
YST kuibua vipaji, serikali na wadau wengine wanapaswa kuunga mkono jitihada hizi
na wanalo jukumu kubwa la kuhakikisha vipaji hivi vinaendelezwa hata baada ya
mashindano.
Lazima serikali na wadau
wengine waweke mazingira mazuri yatakayowapa fursa na hamasa watoto wetu siyo
tu kupenda masomo ya sayansi, bali pia kuonyesha ubunifu na vipaji vyao.
Tunapozungumzia Tanzania
ya Viwanda tunamaanisha kwamba lazima tuwe na wataalamu ambao watabuni na
kuendeleza viwanda vilivyopo.
Comments
Post a Comment