- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Patricia Mhondo, Meneja Uhusiano wa Nje wa Kampuni ya Shell ambao ni moja ya wadhamini wakuu, akifafanua jambo kwenye mkutano na waandishi (hawapo pichani). Kushoto kwake ni Mkurugenzi Mtendaji wa YST, Dkt. Gozibert Kamugisha.
NA DANIEL MBEGA
TAASISI ya Karimjee Jivanjee
(KJF) imeingia mkataba wa miaka mitano na shirika la Young Scientists Tanzania
(YST) kuanzia mwaka huu hadi 2022 kufadhili maonyesho ya wanafunzi ya kazi za
kisayansi na ubunifu.
Devota Rubama, Meneja wa KJF,
aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kwamba, taasisi yake
inaunga mkono jitihada za YST katika kukuza vipaji vya wanafunzi na kuchochea
ubunifu wa kisayansi.
Kwa mujibu wa Rubama, taasisi
hiyo imetenga kiasi cha Dola 100,000 za Kimarekani kila mwaka (sawa na Shs.
milioni 226) ambapo kwa miaka mitano itatoa jumla ya Dola 500,000 kuhakikisha
maonyesho hayo ya kila mwaka yanafanikiwa.
Maonyesho ya mwaka huu
yanatarajiwa kuanza Agosti Mosi hadi 2, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano
cha Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, ambapo jumla ya
wanafunzi 200 kutoka shule 100 nchini kote, watashiriki.
Mkurugenzi Mtendaji wa YST,
Dkt. Gozbert Kamugisha, aliwaeleza wanahabari kwamba, maonyesho ya mwaka huu
yanatarajiwa kuwa na ushindani zaidi kutokana na ubora wa kazi zitakazoshindanishwa.
Kila mwaka, KJF hutoa ufadhili
wa masomo ya elimu ya juu kwa washindi wanne wanaoibuka kwenye maonyesho hayo.
“Kazi za miradi mingi
zimejikita kutafuta suluhisho kuhusu matatizo katika sekta ya afya, kilimo na
usalama wa chakula, mawasiliano, usafirishaji, nishati, elimu, mazingira na
mabadiliko ya tabia nchi,” alisema Dkt. Kamugisha na kuongeza kuwa shule zote
za binafsi na serikali nchini zinaruhusiwa kushiriki bila kutoa fedha yoyote.
Kamugisha alisema kwamba, awali
walipokea mawazo 400 ambayo yalichujwa na kubakia 100 pekee, lakini akaongeza
kwamba washiriki wanatokea katika mikoa yote ya Tanzania - Bara na Visiwani.
Alisema wanasayansi chipukizi
watakaoshiriki katika maonyesho hayo ya YST 2018, ambayo ni ya nane tangu mwaka
2011, wataonyesha kazi zao katika nyanja mbalimbali za kisayansi kama kemia,
fizikia na hesabu, baolojia na ekolojia, sayansi ya jamii na teknolojia.
Wanafunzi watakaojituma na
kufanya ugunduzi mzuri watazawadiwa fedha taslimu, medali, vikombe na
uimarishaji wa maktaba ya shule zao.
Mbali ya KJF, wadhamini wengine
wakuu ni kampuni ya Shell inayojihusisha na utafiti na uchimbaji wa gesi asilia
nchini, ambayo imekuwa ikidhamini mashindano hayo kwa miaka minne sasa tangu
ikiitwa BG.
Patricia Mhondo, Meneja
Uhusiano wa Nje wa Shell, alisema kwamba kwamba, udhamini wa maonyesho hayo umo
kwenye program yao ya miradi ya jamii na kwamba wanaona fahari kuunga mkono
jitihada za kuwaibua wanasayansi wapya.
Washindi wa jumla wa mashindano
hayo watakwenda Johannesburg, Afrika Kusini kushiriki Mashindano ya Sayansi na
Teknolojia, ambapo washindi wa mwaka 2017 walishiriki mwaka jana na kuibuka
mabingwa.
Comments
Post a Comment