- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
NA CONGES MRAMBA, MWANZA
TAKRIBAN familia 100 huko Malemve, Tarafa ya Ngudu wilayani
Kwimba, mkoani Mwanza, zilihofiwa kupoteza maisha na makazi miaka michache tu
iliyopita.
Upepo mkali ulivuma kijijini Malemve, ukaezua nyumba 73.
Wamiliki wa nyumba hizo walikosa makazi, wakabaki
wanaomboleza. Kuku, mbuzi bila shaka walipoteza maisha.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo ya Kwimba, Pendo
Malebeju, akatuma wataalam kutathmini uharibifu huo wa kimbunga hicho kilichoandamana
na mvua kali, bila shaka nyakati za jioni.
Pepo kama hizi ni nyingi na huua mamilioni ya watu na
kusababisha hasara ya mali za mamilioni.
Wataalam wa hali ya hewa wanaonya kuwa majanga haya huletwa
na mabadiliko ya tabianchi kufuatia uharibifu mkubwa wa mazingira tunaofanya
hapa sayari ya dunia.
Mabadiliko ya tabianchi (Climate Change) chanzo chake ni
uharibifu mkubwa wa mazingira.
Ufyekaji wa misitu umefanya nchi kuenea jangwa. Misitu ya
Savannah haipo tena, ndiyo maana tunapata El-Nino,
La Nina au hata vimbunga vinavyoleta
mafuriko na hasara kubwa kiuchumi.
Mkurugenzi wa Wilaya ya Kwimba, Pendo Malebeju, aliteua Tume
kuchunguza kimbunga hiki ili kutafuta ufumbuzi.
Hata hivyo, niseme hapa kwamba, ni vigumu mno ‘Tume Teule’
kama hii ya Kwimba miaka michache iliyopita kutambua pepo hizo na madhara yake.
Badala yake, hupitia juu juu tu pasipo hata kujua ‘Kimbunga’
ni nini? Huletwa na nini? Jamii ifanyeje kuepukana na majanga haya?
KIMBUNGA
NI NINI?
Taasisi ya Hali ya Hewa Marekani, The United States Weather
Bureau, imewahi kufafanua maana ya vimbunga.
Kimbunga hutambuliwa kwa kupimwa mwendo wake, yaani maili
kinavyotembea kwa saa.
Siyo kila upepo ni kimbunga. Kuna vimbunga, chamchela, pepo
kali, Omusoke (Jina la Kikerewe) na vingine vingi.
Upepo mwanana (calm) huvuma kwa mwendo wa chini ya maili
moja kwa saa, kuna ‘light air’, light breeze, gentle na moderate breeze ambazo
huvuma kwa mwendo wa maili kati ya 3-18 kwa saa.
Kuna ‘strong breeze’ hadi gale huanza kuleta madhara. Gale
hukimbia maili kati ya 39-46 kwa saa, na huweza kung’oa miti.
Bado haujafikia strong gale wala storm. Storm (kimbunga)
hukimbia maili kati ya 55 hadi 63 kwa saa, na violet storm huvuma maili
63 hadi 73 kwa saa.
Hurricane kama Katrina na Mitch huvuma kwa mwendo wa zaidi
ya maili 74 ambazo ni kilometa 118.4 kwa saa moja tu.
Upepo mkali unaoweza kukimbia kutoka Mwanza hadi Shinyanga
kwa muda wa saa moja na nusu tu.
Naam, kuna haya ma-hurricanes, tornadoes, cyclones na
typhoons, yanayoweza kuezua nyumba, kutifua tope baharini na ziwani hadi kuua
samaki na viumbe hai.
Yanaweza kusomba maji ziwani au baharini na kuigharikisha
nchi kavu kwa kasi kubwa hata watu wasiweze kujiokoa.
‘Omusoke’ (tornadoes) ni upepo mkali unaoweza kutokea
ziwani, ukapindua kila kitu kichwa chini-miguu juu, hadi samaki wanakufa na
kuelea!
Mawimbi yake yanaweza kuwa na kipenyo cha mamia ya maili.
‘Omusoke’ huweza kujizungusha kwa kasi ya maili 200 kwa saa
au zaidi, hupindua kila kitu-ole wako ukutwe na upepo huu mkali.
Pepo hizi kali zote ni hatari kabisa, madhara yake
hayasemeki.
Haya ni majanga ya asili ambayo ukiyachunguza yanaletwa na
kiburi cha nchi zilizoendelea kama Marekani na washirika wake, kwa kuchafua
sana anga la dunia, kukataa kusaini mikataba kama ule wa Kyoto (Kyoto
Protocol), ili maji yachafuke, viumbe wafe kwa ongezeko la joto na mabadiliko
ya tabianchi, mafuriko kila mahali.
Vifo viletwavyo na majanga, kansa, ukimwi, vyanzo vya
maji kuwa damu, kutoboka kwa utando wa Ozone na kadhalika vimetajwa na Biblia
kama ‘MAPIGO SABA YA MWISHO’.
Miongoni mwa shughuli za kiuchumi za binadamu zinazoharibiwa
sana na uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi ni pamoja na kilimo,
ufugaji, uvuvi na kadhalika.
Mkutano wa New York wa Septemba 22, 2009, ulifanyika
takriban miaka 12 kamili tangu mkutano wa Kyoto, Japan ufanyike Desemba 1997.
Katika mkutano wa Kyoto, viongozi wa mataifa zaidi ya 150
duniani waliweka itifaki ambayo ingewezesha kupunguza hewani kiwango
kikubwa cha sumu zinazoletwa na hewa ya ukaa (C02) na gesi nyingine
kama CH4, N20, HFC8, PFC8 na SF6.
Mkataba huo ulikusudia kupunguza gesi za sumu duniani kwa
silimia 5.2 kabla ya kufika mwaka 2012.
Mataifa yaliyoshurutishwa kusaini mkataba huo wa Kyoto ni
nchi zote 38 zenye viwanda duniani.
Mataifa yote 15 ya Umoja wa Ulaya (EU) yakakubali kupunguza
asilimia nane ya taka hewa zake duniani. Marekani ilitakiwa kupunguza asilimia
saba ya gesi zake inazotupa angani.
Japan, ilitakiwa kupunguza asilimia sita ya taka sumu
inazotupa angani, na nchi zinazoendelea zilitakiwa kupunguza kiwango chochote
kwa uhuru wake.
Marekani ilisaini mkataba huo Novemba 12, 1998, lakini
kutokana na kitisho kutoka kwa matajiri wenye viwanda nchini humo, serikali ya
Rais Bill Clinton ilichelea kupeleka ajenda hiyo katika Bunge la Seneti.
Kusaini Mkataba wa Kyoto na kuutekeleza, maana yake ni
kwamba viwanda vya Marekani vingelazimika kupunguza uzalishaji, ili kupunguza
kiasi cha gesi za sumu angani.
Ni kwa sababu hii, serikali ya Clinton iliufyata.
Mkutano mwingine wa kujadili upunguzaji wa taka za sumu
hewani ulifanyika Bonn, Ujerumani Julai 2001.
Utawala wa George W. Bush ulitangaza kujitoa katika Mkataba
wa Kyoto kwa madai kwamba uliweka zigo kubwa katika nchi zilizoendelea bila
kuzingatia usawa.
Marekani waligeuka wapinzani wakubwa katika ajenda za
kupunguza hewa za sumu duniani, tangu huko mjini Bonn na mahali pengine, kwa
sababu ya maslahi yake na ya viwanda vyake, bila kujali madhara makubwa
yaliyotokana na wingi wa viwanda vyake kutupa angani hewa chafu zenye
kusababisha majanga makubwa ulimwenguni.
Kwa shingo upande, walikubali baadaye kupunguza hewa hizo za
sumu ili kutekeleza huo Mkataba wa Kyoto.
Katika makubaliano ya mjini Bonn, mataifa makubwa yenye
viwanda yanayomwaga kwa wingi hewa za sumu angani, yalishauriwa kufuata malengo
waliyowekewa ya kupunguza hewa ya ukaa katika anga.
Kulingana na Shirika la Kudhibiti Uharibifu wa Mazingira,
hewa ya ukaa (carbon dioxide) imeongezeka sana angani kutoka mwaka 1990 hadi
sasa; na hii ni kutokana na shughuli za binadamu, ikiwa ni pamoja na
viwanda na migodi.
FAIDA
ZA MISITU
Wakati hewa za sumu zinapoongezeka, misitu ama miti
inayopunguza kwa kiwango kikubwa hewa ya ukaa kwa kutengenezea chakula chake (starch)
inatoweka kwa kasi na kwa kiwango cha kutisha sana.
Mashariki ya Mbali pamoja na Oceania wanachafua anga kwa
kiwango cha asilimia 28.9.
Amerika ya Kaskazini huchafua anga kwa kiwango cha asilimia
28.8.
Marekani pekee inachafua anga la
dunia nzima kwa moshi wa magari na viwanda vyake kwa asilimia 24.7.
Ulaya Magharibi, kwa pamoja huchafua anga la dunia kwa
asilimia 16.5, wakati Amerika ya Kusini nzima na Kati huchafua anga la dunia
kwa kiwango cha asilimia 4.3.
Ulaya Mashariki, na iliyokuwa Jamhuri ya Kisovieti (USSR)
huchafua anga la dunia kwa kiwango cha asilimia 12.8. Mashariki ya Kati
huchafua anga kwa kiwango cha asilimia 4.7.
Afrika, inachangia katika uchafuzi
wa anga la dunia kwa asilimia 3.9 tu.
Hii ni kwa mujibu wa Ripoti za
Energy Information Administration, kuanzia mwaka
1999.
Afrika inayochangia kwa kiwango kidogo sana katika uchafuzi
wa hewa angani ndiyo inayoathiriwa na madhara makubwa ya uchafuzi wa hewa
angani unaoleta mabadiliko ya tabianchi.
Mifugo ya Afrika, hususan Kenya, Somalia, Uhabeshi na mwaka
juzi hapa kwetu Tanzania hususan Kanda ya Ziwa hufa kwa ukame unaoletwa na
uchafuzi wa mazingira ya anga kunakoleta ukame.
Ukame huu uliokita katika mbuga za Bugwema mkoani Mara ndiyo
unaochangia jangwa kuongezeka na njaa na vifo vya watu pia.
Benki ya Dunia (WB) ilishasema mwaka 2001 kwamba kila mwaka
watoto wachanga wapatao 500,000 wangepoteza maisha duniani kote kwa sababu ya
uharibifu huu mkubwa wa anga.
MVUA
ZA SUMU
Kunatokea mvua za sumu (acid rains) zitakazosababisha
uharibifu mkubwa wa misitu hasa ya Afrika, na wala mvua za sumu hizi za viwanda
vya mataifa makubwa haziharibu huko kwao peke yake.
Marekani inaongoza duniani kwa uchafuzi wa anga, lakini
athari zake tunapata sisi huku; tunakufa kwa njaa na matokeo ya ukame.
Ni kwa sababu hii, ubeberu wa Marekani wa kukataa kutia
saini mikataba ya upunguzaji wa hewa na taka za sumu, kama huo wa Kyoto, ni
hatari kwa maisha ya watu, hasa tuishio nchi maskini.
Ingekuwa heri kama Mikutano ya New York na Afrika ya Kusini
ingeipa kibano kikali Marekani kwa kiburi chake na kuweka mbele maslahi binafsi
ya viwanda vyao, huku ng’ombe wa maskini wakifa kwa maelfu pasipo fidia.
Marekani hukimbilia kuliburuza Baraza la Usalama la Umoja wa
Mataifa kuzitenga nchi nyingine kaidi kutekeleza mikata kama ya nyuklia.
Imesahau kwamba, mabadiliko ya tabianchi ni janga la kutisha
katika nchi zinazoendelea kama Tanzania.
NI
HATARI KULIKO UGAIDI
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Makerere Uganda, Alphonce Nkusi,
aliwahi kusema majanga ya kiasili yanayotokea leo Marekani, kufuatia uharibifu
wa mazingira, ni mabaya kuliko ugaidi.
Amesema, utunzaji wa mazingira haupewi umuhimu kama
vita dhidi ya ugaidi duniani, lakini hasara zinazotokana na majanga haya ni
kitisho maradufu duniani.
“Marekani sasa haishambuliwi na magaidi wa Al-Qaeda, inashambuliwa
na majanga ya kiasili, Katrina na Rita, kiasi cha kuwaua maelfu, na kuwafanya
wengine wakimbizi,” Nkusi alisema.
Alikuwa akihutubia waandishi wa habari waliohitimu kozi ya
wiki mbili ya mazingira, iliyofanyika katika Chuo Kikuu cha SAUT, Nyegezi
jijini hapa mwaka 2007.
Nkusi, ambaye alikuwa Mratibu wa mafunzo ya habari za mazingira
katika nchi tano za Bonde la Ziwa Victoria (Victoria Basin), Kenya,
Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi, aliwataka waandishi waliohitimu mafunzo
hayo kuitaarifu jamii ya watu zaidi milioni 100 wa nchi hizo kuhifadhi
mazingira, hususan Ziwa Victoria, linalotoa raslimali nyingi ambazo ni chanzo
kikuu cha uchumi, na ni uhai wa watu hao.
“Wanaovunja sheria za ulinzi wa mazingira, kwa kufanya uvuvi
haramu au kukata miti, kuchoma mkaa, kwa nia ya kujipatia fedha, wanafanya
nini? Wanapata faida gani, kulinganisha na hasara wanayosababisha?”alihoji.
Alishauri sheria kali zinazolinda mazingira kutungwa
sambamba na zile za kuzuia ugaidi, kwa kuwa majanga ya kimazingira ni kitisho
kikubwa kuzidi ugaidi hapa duniani.
Alishauri waandishi wa habari kufichua uovu mwingi na uzembe
dhidi ya mazigira, ili kuiepusha dunia katika maangamizi kama vimbunga
vinavyotokea Marekani.
Kwa kuharibu mazingira ya dunia tunamoishi, kutokana na
moshi wa viwanda, magari (daladala), kufyeka na kuchoma misitu; tunachezea
maisha yetu kamari, na tunajiletea mustakabali wa kifo.
Kila kunapokucha, viwanda, magari, na mitambo
mbalimbali duniani hurusha angani mamilioni ya taka za sumu, ambazo huongeza
joto duniani, na ufyekaji wa misitu unatisha.
TANI
MILIONI 400 ZA SUMU ANGANI
Kituo cha Marekani cha Udhibiti wa Uchafuzi wa Hewa,
kiliwahi kutabiri kuwa kuanzia mwaka 2000, tani milioni 404 za hewa ya sumu
zitakuwa zikirushwa angani kila mwaka.
Uchafu huo unaolemea dunia, unakisiwa kujumuisha tani milioni76
za Sulphur dioxide, tani milioni 207 za carbon monoxide, tani milioni 53
za Hydrocarbons, tani milioni 30 za Nitrogen Oxides, na tani milioni
28 za vumbi, ukungu na masizi.
Mwandishi Henry Schroeder, katika kitabu chake, THE POISON
AROUND US, kilichochapwa mwaka 1974 na Chuo Kikuu cha Indiana, alisema kama
kiasi hiki hakitadhibitiwa, basi dunia itakumbwa na majanga ya kutisha, kama
Tsunami, vimbunga kama Mitch, Katrina, na vingine vingi ambavyo vitaujia
ulimwengu.
Wanasayansi wamesema kuwa joto linapozidi duniani, kufuatia
uchafuzi huu wa hewa angani, katika Ncha za Kaskazini (North Pole) na Kusini (South
Pole), maji huchemshwa hadi barafu kuyeyuka na kuifanya bahari kuumuka urefu wa
futi 250 za usawa wa bahari na kugharikisha visiwa na Pwani.
Kutokana na nguvu za asili kuchochewa na joto lililotokana
na hewa za sumu, maji ya bahari hupeperushwa kwa nguvu za vimbunga au tufani
hadi nchi kavu na kugharikisha watu.
Ndivyo ilivyotokea New Orleans; kimbunga Katrina kikasomba
maji baharini kwa mawimbi yenye urefu wa futi 30, yakavunja kingo za Mto
Mississippi, na kugharikisha mji mzima wenye wakazi nusu Milioni.
Uliwahi kugharikishwa mwaka 1927 kabla ya mwaka huo 2005.
Kuna uhusiano kati ya vimbunga, matetemeko, tufani na
majanga yote ya asili.
Miti inayopunguza hewa chafu hii inapokatwa na kutoa mwanya
kwa joto kuongezeka,ndipo majanga ya asili yanapotokea na kuua watu.
GAIDI
ANAYEHARIBU UCHUMI
Majanga haya huvuruga kila kitu, hususan uchumi, na
kuwafanya waathirika kurejea maisha ya mamia ya miaka nyuma.
Kwa mfano, janga la Katrina, liliharibu uchumi wa New
Orleans, hadi pakiti ya sigara za kawaida iliuzwa Dola 10 (sawa na Shs. 10,000).
Mafuta yamepanda, na kila bidhaa ziko juu kupindukia.
Katika maeneo yanakotokea majanga, dola hushindwa kudhibiti
uhalifu.
Janga la Katrina lilifanya wafungwa kutoroka, na mafaili ya
kesi zao kusombwa na mafuriko.
Polisi waligeuka majambazi,na raia wa kawaida wamegeuka
waporaji (looters) ili kujinusuru na njaa na shida ya mahitaji, ambayo ni nadra
kuyapata wakati wa majanga haya.
Hii ni kusema kwamba, uharibifu wa mazingira ni zaidi ya
ugaidi na maangamizi ya mabomu kama yale ya Hiroshima; hivyo lazima kukabiliwa
sambamba na ugaidi, au silaha za sumu.
Kwa mfano huu wa Katrina, ni vema tangu sasa jumuia za
Kimataifa zikatazama upya namna ya kupambana na majanga haya ya asili, kama
siyo kuyaondoa kabisa.
Katika Tanzania, uharibifu wa mazingira haujawa mkubwa
kulinganisha na Marekani, tunasogea sana.
Lakini, misitu inafyekwa bila serikali kuchukua hatua
zinazostahili. Haifahamiki ni kwa nini jamii hailichukulii uzito mkubwa suala
la mazingira.
Je, wananchi wa kawaida wametambua kwamba ardhi ikihifadhiwa
ipasavyo itatupa kila kitutukitakacho?
Ardhini tunapata chakula, vifaa vya ujenzi, malisho ya
mifugo, vyombo vya usafiri na kadhalika.
Hali za uchumi wa watu hutegemea uoto wa asili. Ukitaka
kujua hali za watu, tazama uoto wa asili.
Mahali pasipo na miti au nyasi za kutosha, watu ni fukara
kupindukia. Pasipo na miti hapana uhai; ndiyo maana Mungu akamuumba mwanadamu
baada ya miti kuwepo.
Miti hii ndiyo chakula chetu, dawa yetu, nyumba zetu, vyombo
vyetu vya usafiri baharini na nchi kavu, ndiyo vitanda vyetu, kabati zetu,
magazeti yetu, redio zetu.
Miti husaidia kuleta mvua, huondoa joto duniani, hutunza
ardhi yetu, kwa nini hatuitunzi wakati ni wakala wa Mungu wa uhai wetu?
Janga la Tsunami na Katrina yawe somo kwetu ili tuhifadhi
mazingira.
Tusipotunza mazingira tunajichagulia mustakabali wa kifo,
kama si umaskini, majanga na dhiki za milele.
CHANZO: TANZANITE
Comments
Post a Comment