Featured Post

CCM YANYAKUA KATA 9 KATI YA 20 ARUSHA BILA JASHO, WAPINZANI WAINGIA MITINI


MADIWANI tisa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Arusha wamepita bila kupingwa baada ya wagombea wa vyama vya upinzani kushindwa kuchukua fomu na mgombea mmoja kujitoa dakika za mwisho.
Katibu wa CCM Wilaya ya Ngorongoro, Amos Shimbo, alisema wagombea wa CCM wametangazwa na msimamaizi wa uchaguzi wilayani humo kuwa madiwani wateule na wanasubiri kukabidhiwa barua zao.

Shimbo aliwataja waliopita bila kupingwa kuwa ni pamoja na Daniel Orkeri wa Kata ya Ngorongoro, Lazaro Saitoti wa Kata ya Ng’oile, Sokoine Moil wa Kata ya Aloitole, Boniface Kanjwele wa Kata ya Soitsambu na Kerei Seuri wa Kata ya Pinyinyi.
Naye Katibu wa CCM wilayani Monduli, Kurisha Mfanga, alisema wagombea watatu wa Chama Cha Mapinduzi wamepita bila kupingwa, huku mgombea wa ACT Wazalendo akiamua kujitoa katika Kata ya Engutoto.
Kufuatia kujitoa kwa mgombea wa ACT Wazalendo, mgombea wa CCM, Emmanuel Ambrose ametangazwa na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Monduli, Stevin Ulaya kuwa Diwani wa Kata ya Engutoto, pamoja na Edward Lenanu Laizer wa
Kata ya Naaralami, na Solomon Mollel wa Kata ya Lolkisare.
Baada ya vyama vya upinzani kushindwa kuweka wagombea katika Kata tisa, uchaguzi utafanyika katika Kata 11, huku uchaguzi katika Kata ya Terrati jijini Arusha ukiwa umekumbwa na sintofahamu baada ya mgombea wa Chadema kutekwa na kuporwa fomu.
Tukio hilo lilitokea Julai 14, 2018 ambapo mgombea wa Chadema, Raymond Laizer, alivamiwa na watu wasiojulikana na kuporwa fomu za uchaguzi wakati akizirejesha katika ofisi za Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi wa Kata ya Terrati.
Katibu Mwenezi wa Chadema Wilaya ya Arusha Mjini, Isaya Hari, alisema mgombea wao alivamiwa na kundi la vijana na kuporwa fomu na kuibuka vurugu kubwa zilizosababisha kushindwa kurejesha fomu hizo.
Hari ameongeza kusema kuwa, tayari Chadema wamemundikia barua Msimamizi wa Uchaguzi wakitaka zoezi la kupitisha wagombea lisimamishwe kwa kuwa mgombea wao aliporwa fomu na kushindwa kurejesha kwa wakati.
“Endapo msimamizi atapuuza na kutozingatia mazingira ya tukio hilo tunakusudia kwenda mahakamani kuzuia zoezi zima la uteuzi hadi mgombea wetu atakapopewa haki ya kuongezewa muda wa kujaza upya na kurudisha
fomu,” alisisitiza Hari.
Katika kinyang'anyiro cha Kata ya Terreti waliokuwa wamejitokeza kuchukua fomu ni wagombea wawili tu, Obed  Meng'oriki wa CCM na Raymond Laizer wa Chadema.
Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Ramadhan Ng’anzi, alipotafutwa kuhusu tukio la kutekwa na kuporwa fomu mgombea huyo, simu yake ilipokelwa na msaidizi wake na kudai kuwa yuko katika kikao.
Katika tukio hilo la kutekwa na kuporwa fomu, Katibu Hamasa wa Umoja wa
Vijana wa CCM (UVCCM) aliyefahamika kwa jina la Mutu Marijali alivunjwa mguu huku ikidaiwa wapambe wa mgombea wa Chadema walihusika katika kumshambulia, huku viongozi wa CCM Wilaya wakishikwa kigugumizi kueleza ilikuwaje Katibu hamasa alikuwa katika tukio la kumteka na kumpora fomu mgombea wa Chadema.


Comments