Featured Post

CAROBON DIOXIDE: HII NI AJALI KUBWA YA BINADAMU



NA CONGES MRAMBA, MWANZA
JUMANNE, Septemba 30, 2014, viongozi wa mataifa 120 duniani walikutana Jijini New York, Marekani, kujadili tishio linaloikabili Sayari ya Dunia, yaani ongezeko la joto na mabadiliko ya tabianchi. Mkutano huu uliitwa UN Climate Summit.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, kabla ya kumaliza muda wake, aliitisha kikao hiki jijini New York, kufuatia tishio kubwa la ongezeko la sumu zinazosababisha majanga makubwa yaletayo maafa yasiyosemeka.
Wanasayansi walisema mwaka  2014, hewa ya ukaa (carbon dioxide) iliongezeka hadi kufikia mzigo wa taka za sumu hewani kiasi cha tani bilioni 40.

Mkutano huu ulitanguliwa na maandamano makubwa katika miji mikuu ya Washington, Marekani na London, Uingereza.
Matokeo ya ukaidi wa kupunguza uchafuzi wa anga na hewa tumeshuhudia majanga kama vimbunga, mafuriko, maporomoko ya ardhi, ukame wa muda mrefu ulioleta vifo vya watu na mifugo hususan Afrika, huku jangwa likikaribia kuimeza Afrika nzima.
Mwaka huu 2018 tunashuhudia tishio hili kwa kiwango cha kutisha. Mafuriko yamezamisha mashamba, kiangazi kimeangamiza kila kitu, hali hii imeleta pia wadudu waharibifu wa mazao, wakulima watavuna haba.
Mabadiliko ya tabia nchi huleta pia athari za kiafya na magonjwa kama Dengue, Malaria na kadhalika.
Siku hizi hata Moshi na Iringa (Makambako) nako kuna Malaria? Barafu ya Mlima Meru na Kilimanjaro imekwisha?
Sababu, zinapoharibu anga la dunia kwa moshi na sumu za viwanda vyao, gesi hizo za sumu huongeza joto la dunia nzima na kusababisha majanga, vifo vya watu na mifugo kufuatia njaa iliyoletwa na ukame wa muda mrefu na huvuruga shughuli za kiuchumi za wakazi wa nchi maskini kama Tanzania.
Ripoti ya Benki ya Dunia, iliyoitwa, ‘World Development Report 2010’, kuhusu mabadiliko ya tabianchi, ilisema ongezeko la joto duniani  liligharimu kipato cha mataifa ya Afrika kushuka kwa asilimia nne; India ni asilimia tano.
Kushuka kwa Pato la nchi maskini ni janga kwa uchumi wa watu hususan wanavijiji.

MKATABA WA KYOTO
Mkataba wa Kyoto, Japan wa mwaka 1997, ulizitaka nchi 38 duniani ambazo ni tajiri zenye viwanda, kupunguza kupeperusha angani moshi wa viwanda vyao (sumu)  kwa asilimia 5.2 hadi mwaka 2012.
Marekani walisaini Mkataba wa Kyoto Novemba 12, 1998, lakini matajiri wa nchi hiyo wakapinga kutekeleza mkataba huo ambao pia hudai kupunguza uzalishaji.
Hata kama Marekani baadaye walisaini itifaki hiyo ya Kyoto kwa shingo upande tu, wameendelea kuchafua anga kwa kiwango cha kutisha.
Mchango wa Marekani pekee katika kuchafua anga la dunia nzima ni asilimia 26.
 Mashariki ya Mbali pamoja na Oceania, huchafua anga la dunia kwa moshi na masizi ya viwanda na migodi yake kwa kiwango cha asilimia 28.9.
Amerika ya Kaskazini huchafua anga la dunia kwa asilimia 28.8. Ulaya Magharibi huchafua anga la dunia kwa asilimia 16.5, wakati Amerika ya Kusini nzima inachafua anga la dunia kwa asilimia 4.3.
Sisi Waafrika, mchango wetu katika kuchafua anga ya dunia haujawahi kuvuka asilimia 3.
Lakini, Ulaya Mashariki na iliyokuwa Jamhuri ya Kisovieti huchangia uchafuzi wa anga la dunia kwa asilimia 12.8, Mashariki ya Kati huchafua anga kwa asilimia 4.7.
Tangu mwaka 1981-85 watu takriban milioni 500 wa nchi maskini duniani ndio wanaohitaji msaada wa kibinadamu majanga makubwa yanayoletwa na ongezeko la joto duniani yanapofika.
Miaka ya 2001-05 watu waliohitaji msaada kufuatia haya majanga walifika bilioni 1.5 wengi wao kutoka nchi maskini.
Mabadiliko ya tabianchi huleta maradhi, ukame na ukosefu wa maji safi na salama.
Mazao huharibika mashambani kwa ukame au mafuriko. Vimbunga kama Mitch kilichoua watu Honduras mwaka 1998 au hata Katrina na majanga mengine ya kiasili huzidi kuua watu kwa makumi ya maelfu hapa duniani.

KANDA YA ZIWA
Mabadiliko ya tabia nchi, licha ya kuangamiza makumi ya mifugo katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, huku yakiongeza magonjwa ya kuambukiza ambayo hayakuwepo zamani, sasa yamesababisha magonjwa ya mazao ya chakula na biashara.
Nilifika nyumbani kwa mwanakijiji cha Saragana, Musoma mkoani Mara, Chikuku Mbogora, mwaka 2017, nikaambiwa kila siku ng’ombe wawili walikuwa wanakufa (asubuhi na jioni) kwa kukosa malisho.
Baadaye, niliambiwa jumla ya ng’ombe 35 walikufa wakati huo wa kiangazi.
Katika wilaya za Bunda na Musoma Vijijini, mifugo walikufa, wakaachwa porini, hata fisi walikataa kula mizoga hiyo ambayo haikuwa na ladha.
Fisi waliacha mizoga porini, wakaenda kurarua mbuzi na kondoo mabandani, maana ng’ombe hawakuwa tena na ladha!

ATHARI ZA KIUCHUMI
Ofisa Kilimo katika Sekretarieti ya Mkoa wa Mwanza, Innocent Keya, alisema mabadiliko ya tabianchi yaliwaletea adha wakulima wa nyanya (zao lingine la biashara), pamba na muhogo.
Keya alieleza namna nzi weupe (White Flies) walioletwa na ongezeko la joto na mabadiliko ya tabianchi, wanavyoshambulia zao la muhogo na kuongeza tishio la njaa na jitihada za serikali ya Tanzania kupambana na magonjwa haya ya zao la muhogo.
“Hapa Kanda ya Ziwa, kabla ya mazao ya nyanya na muhogo kushambuliwa na magonjwa hayo, wakulima hawakuwa fukara kama siku hizi,” anasema Keya.
Ofisa kilimo huyo anasema, magonjwa ya vipepeo katika nyanya huletwa na vipepeo, Tomato Leaf Minor ambao wameletwa na mabadiliko ya tabia nchi kutoka nchi jirani tangu mwaka 2014.
Kulingana na historia, muhogo uliletwa na Wajerumani kutoka Marekani kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa kwa nia ya kupunguza njaa.
Majani ya mihogo ni mboga nzuri iitwayo kisamvu ambacho kina Vitamin A, B na C.
Mizizi yake ndiyo chakula kikuu sasa kwa wakazi wa Ukanda wa Ziwa, na kutetereka kwa zao hilo katika maeneo mengi, kumeleta upungufu mkubwa wa chakula, miti yake ni kuni au nishati muhimu ya kupikia chakula.

PAMBA
Tukiondoka katika zao hili la muhogo, na nyanya sasa tunatazama Pamba (Dhahabu Nyeupe), ambayo kabla ya kuathiriwa na hali ya hewa msimu wa kilimo 20016/2017 na msimu huu  2017/18, ilikuwa tegemeo kwa uchumi wa wakazi wa mikoa takriban 15 hapa Tanzania.
Mvua kubwa mwaka huu imezamisha mashamba, wakulima wamevuna nusu ya mategemeo.
Unapofika mikoa ya Kanda ya Ziwa, unazungumza kuhusu pamba, ambalo ndilo zao kuu la uchumi.
Mara mvua zikatae kunyesha, zao hili linatetereka. Mara zinanyesha nyingi, mashamba yanazama, au wadudu wasumbufu wanaibuka, pamba inaoza.
Tayari kuna wilaya kama Bunda, wakulima walishakata miti ya pamba na kuichoma kwa sababu ya wadudu hawa wanaofyonza majani ya pamba, wenyewe wanadhani tatizo ni mbegu ya UKM 08, kumbe ni wadudu hatari walioletwa na mabadiliko ya tabianchi.
Hawa wadudu ni pamoja na viwavi jeshi vamizi (fall army worms), na utitiri unaovyonza majani ya pamba. Haufi kwa dawa ya aina moja.
Zamani wakulima wakinyunyiza mara moja kwa majuma mawili, leo tunaambiwa kila siku ya pili lazima kunyunyiza dawa za sumu, hili ni ongezeko la gharama za kilimo.
Mihogo inaoza, pamba inashambuliwa, nyanya zimeliwa na vipepeo, mifugo wanaangamia kwa ukame wa kutisha kila mwaka.

BUTIAMA MISITU IMETOWEKA
Juni Mosi hadi 5 mwaka 2017 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo kitaifa yalifanyika kijijini Butiama, mkoani Mara, tulibaini hata misitu ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kamabarage Nyerere iliangamizwa vibaya na tabianchi.
Hapa ndipo nyumbani kwa Baba wa Taifa, ambaye anatajwa kuwa mwana mazingira aliyejali na kuheshimu mimea, ikiwemo miti.
Sherehe hizo zilihudhuriwa na viongozi anuwai akiwemo Waziri katika Ofisi ya Rais (Mazingira) Januari Makamba, wakuu wa wilaya, wa mikoa, wataalam na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan na wengine wengi.
Mwaka huu 2018 pia tumeadhimisha mazingira siku chache zilizopita. Madhara yangalipo.
Miaka 13 iliyopita, Tanzania ilitajwa miongoni mwa nchi 50 zilizokuwa na misitu mikubwa duniani.
Kulingana na Kitabu cha Kalenda, World Almanac, Toleo la 2007, Tanzania katika mwaka wa 2005 ilikuwa na jumla ya hekta za misitu 35,257, na kila mwaka hekta zaidi ya elfu 15 zikifyekwa na kupotea, kufuatia matumizi makubwa ya nishati ya mkaa na upanuzi wa mashamba.
Watu wanalima hadi mtoni, na kusababisha maji ya mvua kusomba tope hadi Ziwa Victoria.

UKOSEFU WA MISITU
Matokeo yake, sote tunajua hivi sasa mvua zimegoma kunyesha mahali pengi nchini na usalama wa chakula uko rehani.
Hata zikinyesha, zinagharikisha mashamba.
Nchi nyingine za Afrika zenye misitu minene ni pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambayo inatajwa kuwa na hekta 133,610 za misitu, Sudan, Zambia, Afrika ya Kati na Angola.
Nchi zinazoongoza kuwa na misitu mikubwa ni zile za Amazonia kama Brazil, Argentina, Venezuela na Mexico, zikitanguliwa na Urusi, Canada, Marekani, Uchina, Japan, na Sweden.
Naam, ufyekaji wa kasi wa misitu na uharibifu mkubwa wa mazingira leo umeleta majanga lukuki kama kupungua kwa kina cha Ziwa Victoria na kukauka kwa mito kunakoletwa na kukosekana mvua za kutosha misimu iliyopita.
Msimu huu mvua imenyesha nyingi, tunalalamikia pamba imezamishwa na wadudu waharibifu wameongezeka, mashamba ya mahindi pia yamegharikishwa na mafuriko.
Barabara na madaraja yamesombwa na maji, serikali itatumia fedha nyingi kurekebisha miundo mbinu!

SAMAKI WAMETOWEKA
Umoja wa wakazi wa Jiji la Mwanza wanaotesha vitalu vya miti mbalimbali ikiwemo ya matunda ufukweni mwa Ziwa Victoria jirani na Barabara ya Makongoro jijini Mwanza.
Hiki ni kikundi cha Omisanya, ambao wamenieleza mafanikio ya kazi hii ya kupanda miti na changamoto zake.
Naam, kikundi hiki cha watunza mazingira wa Mwanza, Omisanya, hakiishii kuotesha miche ya miti, bali pia hufuga samaki katika mabwawa yaliyoko mita chache kutoka Ziwa Victoria, ziwa kubwa hapa Afrika na ni la pili kuwa na maji yenye uhai hapa duniani, nyuma ya Superior la Marekani.
Samaki wanafugwa kandoni mwa ziwa hili, kwa kuwa ziwani kuna magugu maji na uvuvi haramu umesababisha sato na sangara kutoweka!
Hata Ukerewe kisiwani, wanafuga samaki!
Mkoa wa Mwanza pekee kuna visiwa 79 ndani ya ziwa hili ambako kuna makambi ya uvuvi wa samaki.
Asilimia takriban 53 ya ukubwa wa Mkoa wa Mwanza ambao ukubwa wake ni jumla ya kilometa za mraba 25,233 ni maji ya ziwa hili.
Hii ni kusema kilometa za mraba 13,437 ni maji na sehemu iliyobaki ndiyo nchi kavu.
Wilaya ya Ukerewe ina jumla ya visiwa 38, Sengerema kuna visiwa 8, Buchosa 28, wakati Wilaya ya Ilemela ina visiwa vitatu na Magu kuna visiwa viwili.
Asilimia 60 ya visiwa hivi kuna watu wanaishi na asilimia iliyobaki wanakaa wavuvi na kuvua samaki.
Hata hivyo, kulingana na Kaimu Msimamizi wa Rasilimali za Uvuvi mkoani Mwanza, Radhmina Ramadhan Mbilinyi, anasema samaki wanatoweka kasi kufuatia wimbi la uvuvi usio endelevu, na hasa uvuvi haramu.
Kufuatia kupungua kwa samaki, hata Kisiwa cha Ukerewe, kinachozungukwa na maji ya ziwa hili, wanalazimika kufuga samaki mabwawani ili kukabili uhaba wa kitoweo. Samaki mabwawani? Siyo ziwani!
Haikuingia akilini miaka michache iliyopita, wataalam kuwaambia wakazi wa Ukerewe na Jiji la Mwanza kuanza kufuga samaki mabwawani, kandoni tu mwa Ziwa Victoria.
Baharini visiwa vitamezwa na maji yaliyoumuka ya bahari. London utazama!
Zamani, nilisoma makala ya Mwandishi Brown Lenga, kwamba ‘London Can Be Flooded Any Time!’

TABAKA LA OZONE
Ndilo linayolinda tabaka la juu la hewa linaloitwa Ozoni (Ozone Layer).
Kuna kemikali nyingi zinazoharibu tabaka hili.
Ziko kwenye majokofu (refrigerators), viyoyozi, mifuko ya plasiki ikichomwa inaleta sumu hii, na kadhalika.
Tabaka hili ni mlinzi wa maisha ya watu na viumbe hai, lakini huharibiwa hasa na Ulaya, Marekani, Asia na kadhalika na madhara yake hayaishii huko yanakopeleka vimbunga na vifo, hutuletea hata sisi mabadiliko ya
tabianchi, ambayo ni chanzo cha kiangazi na vifo vya mifugo, umaskini, njaa, na magonjwa.
Tabaka hili ni kama blanketi au mwavuli wa kutukinga na miali ya jua mikali na yenye sumu.
Lipo takriban kilomita 10 hadi 50 kati ya jua na uso wa dunia.
Mionzi ya jua ni sumu iitwayo Kiswahili, “Kikiuka-urujuani’ kitaalam wanaita, ‘Ultraviolet-B radiation’.
Nimeita miali sumu ya jua, kwa sababu mionzi hii ya Kikiuka-urujuani isipochujwa na blanketi la ‘ozone’ ambalo  kipenyo chake ni kama meta tatu hivi, hufika kwetu kwa ukali, na kusababisha madhara katika afya ya binadamu na huharibu mazingira.
Sumu hizi huleta madhara ya macho, huleta saratani ya ngozi, huua mifugo, wanyama na binadamu hawawezi tena kubeba mimba na kujifungua.
Sumu mbaya nitakazoeleza hapa ndizo hutoboa utando huu muhimu, kwa hiyo mionzi hii ya ‘kikiuka-urujuani’ hupenya kwenye matundu katika blanketi hili muhimu alilotuwekea Mungu na kuanza kuunguza chochote katika uso wa dunia.
Huunguza miche yote, huleta maradhi mengi na husababisha madhara makubwa hata mafuriko, kiangazi na vifo vya wanyama kama vilivyotokea mkoani Mara na mahali pengine hapa Afrika Mashariki.
Tafiti za kisayansi zimethibitisha kumomonyoka kwa utando wa
Ozoni, kufuatia mataifa ya viwanda kumwaga angani taka hewa (air pollutants), ambazo ni pamoja na kemikali aina ya chloroflourocarbons (CFCs), helons, methl bromide, carbon tertrachroride na nyingi nyinginezo hadi masizi au ukungu angani!
Kemikali hizi nyingine ziko kwenye majokofu yetu ,viyoyozi, vifaa vya kuzimia moto, usafishaji chuma, utengenezaji magodoro, madawa, manukato na kilimo na uhifadhi wa mazao.
Kwa kuwa sasa ni Tanzania ya viwanda, kemikali hizi haziepukiki.
Hata hivyo, Mungu aliweka mimea na hasa miti kuondoa sumu hizo angani.
Mimea mchana hutumia gesi hizi za Carbon Dioxide kutengenezea chakula chake (starch), ndivyo mimea au miti inavyoondoa sumu  hizi adui wa Ozoni.
Sasa tunashuhudia madhara ya kutoboka kwa utando huu, miali ya sumu toka juani, kikiuka-urujuani kinatujia na kuangamiza kila kitu ardhini!
Kikiuka-urujuani pia husababisha upofu, saratani ya ngozi, uharibifu wa macho (mtoto wa jicho), husababisha hata akina mama kutokwa mimba!
Madhara mengine ni kiangazi kinacholeta njaa, umaskini,vifo vya mifugo, jangwa la kutisha na hata mwili hushindwa kukinzana na
maradhi.
Ikolojia huharibiwa sana, samaki hufa, viumbe wa majini hutoweka.
Sasa Mara, chakula chao kikuu ni pamoja na nafaka na samaki, vyote vimetoweka, maji yamepungua, visima na kina cha ziwa kinapungua sana, mwisho maji yatatoweka.
Oktoba 2017, wakazi wa Jimbo la Mwibara, Bunda na Musoma Vijijini, walikuwa wakiamka saa 8 usiku kutafuta maji, lakini wasiyapate!
Haya maji yatatoweka kabisa, yatakayobaki yatakuwa damu,wao wanaita, rugogombwa!
Ufunuo 16:2-9 kuna Mapigo sasa ya mwisho. Haya yanafuatia kiburi cha mwanadamu kutofuata sheria za maadili, ikiwa ni pamoja na uharibifu
mkubwa wa mazingira mkoani Mara.
Maji kugeuka damu, na jua kuanza kuwaunguza wanadamu, jua linawaka hadi nyuzi joto 32 za centigrede.
Mito yote imekauka, Mto Mara unapungua kwa zaidi ya asilimia 60 tangu miaka ya 1970. Mto Simiyu unajaza tope ziwani.
Mizoga ilitapakaa mbuga za Masinono na Bugwema, mkoani Mara, ng’ombe ameuzwa kwa shilingi 30,000 maksai, na wengine wameuzwa hata kwa shilingi 15,000 tu.
Haya ndiyo majanga ya asili yaletwayo na kiburi na ujinga wa mwanadamu (natural disasters).
Naam, yameanzia hata Marekani ambako vimbunga (hurricanes) hufululiza kuua mamilioni, ni kwa sababu ya kudharau mikataba kama ule wa Vienna, Uswisi uitwao Vienna Treaty wa mwaka 1985.
Waliambiwa kuhifadhi tabaka la Ozoni, wakabisha, kuna mikataba kama ya Kyoto, na marekebisho yake.
Hatutajali, lakini hii ni AJALI YA BINADAMU!
CHANZO: FAHARI YETU

Comments