- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
NA DANIEL MBEGA, DODOMA
LICHA ya msimu wa masika kwa mwaka huu
2017 kukumbwa na hali ya ukame, lakini upatikanaji wa pembejeo za kilimo
umekumbwa na changamoto kubwa inayoashiria uzalishaji duni wa mazao ya chakula
na biashara.
Safari hii siyo changamoto ya ubadhirifu
na ucheleweshaji wa pembejeo hizo, bali ni wakulima wenye dhamana tu ndio
wanaoruhusiwa kupatiwa vocha za pembejeo.
Uchunguzi uliofanyika mkoani Dodoma
umebaini kwamba, ingawa wakulima wengi mkoani humo siyo wanufaika wakubwa wa
pembejeo hizo, lakini wale wanaostahili kupata safari hii wameshindwa baada ya
kuwepo kwa sharti la dhamana ya kuwa na shamba lisilopungua ukubwa wa ekari
moja.
Aidha, wakulima wengi ambao mara nyingi
huhitaji pembejeo hizo, hususan mbegu na mbolea, na wale wanaojihusisha na
kilimo cha mpunga, mahindi na vitunguu, wengi wao wakiwa katika maeneo ya
mabonde ambayo yanahusisha kilimo cha umwagiliaji.
Zuberi Saidi Mlinji, Ofisa Ugani wa Kata
ya Malolo, anasema, utaratibu wa ugawaji wa vocha za pembejeo umebadilika
ambapo sasa si wote watakaonufaika kama ilivyokuwa zamani bali ni wale tu
watakaokidhi masharti.
“Kwa mfano, katika Kijiji cha Malolo
vocha zitakazokuja ni 100 tu na zitatolewa kwa wakulima ambao wanakidhi vigezo
vya kuwa na shamba lisilopungua ekari moja,” anasema ofisa huyo.
Anasema serikali imefanya hivyo baada ya
kugundua kwamba, baadhi ya wakulima waliokuwa wakipata vocha za pembejeo
hawakuwa pia na uwezo wa kulipia hata nusu ya gharama na wengine hawakuwa
kabisa na mashamba, hatua ambayo iliwafanya baadhi yao kuzigeuza mtaji kwa
kuuza kwa wenye uwezo.
“Wengi walikuwa wakiziuza tena vocha
hizo kwa sababu ama hawakumudu gharama, hawakuwa na mashamba na wengine
waliamua tu kutotumia na kugeukia kwenye kilimo cha asili walichokizowea kwa
kutumia mbegu za asili na hawakutumia mbolea kabisa,” anabainisha ofisa ugani
huyo wakati akizungumza na mwandishi wa makala haya kijijini Malolo.
Anasema hivi sasa wameamua kutoa
pembejeo hizo kwa wakulima baada ya kujiridhisha kwamba wana uhitaji na wanayo
mashamba yanayokidhi vigezo.
Aidha, anasema kwamba, kupungua kwa
idadi ya vocha hizo za pembejeo ni jambo la kawaida, kwani mpango huo wa
serikali ulilenga kuwawezesha wakulima kupata mbegu bora pamoja na mbolea ili
kukuza uzalishaji na kuongeza kipato.
Kupitia mpango huo wa ruzuku ya pembejeo
ulioanza mwaka 2008, serikali ililenga kuwapunguzia mzigo wakulima kwa kubeba
nusu ya gharama za pembejeo hizo wakati kiasi kingine kilipaswa kulipwa na
wakulima wenyewe.
Kwa mujibu wa maelezo ya maofisa kutoka
wizara ya kilimo, idadi ya vocha hizo ilikuwa ipungue kila mwaka kwa kuamini
kwamba, walau katika kipindi cha miaka mitatu wakulima hao wangekuwa na uwezo
wa kujinunulia wenyewe pembejeo.
“Watu wanakosea, ni kwamba, mpango huu
ulipanga kuwawezesha wakulima wote walau kwa miaka mitatu, na baada ya hapo
vocha zisingeweza kuja kwa idadi sawa, bali zingeendelea kupungua kwa kuwa
serikali iliamini katika kipindi hicho tayari wakulima wangeweza kumudu kununua
pembejeo wenyewe, jambo ambalo linaonekana kama limeshindikana,” anasema ofisa
mmoja wa wizara hiyo anayeshughulikia masuala ya pembejeo, ambaye aliomba
hifadhi ya jina lake.
Lakini kupungua kwa vocha hizo za ruzuku,
na kwa utaratibu wa sasa wa kuhakikisha wakulima wanakuwa na dhamana, kutaleta changamoto
kubwa ya mpango wa serikali kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya kilimo.
Licha ya kupungua kwa idadi hiyo, lakini
mara kadhaa pembejeo zimekuwa zikichelewa kuwafikia wananchi na mpango huo
umekumbwa na ufisadi mkubwa kwa watendaji pamoja na mawakala, ambapo inaelezwa
kwamba, baadhi yao walishtakiwa katika mahakama za kisheria.
Kila mwaka, bajeti kuhusu pembejeo za
kilimo imekuwa ikipungua na wakulima, ambao wanaamini ni haki yao kupata vocha
hizo bila kujali idadi yao, wanaona kwamba serikali imewatelekeza.
Kwa mfano, katika bajeti ya kilimo ya
2015/2016, makadirio ya mahitaji
ya pembejeo yalikuwa tani 485,000 za mbolea, tani 60,000 za mbegu bora, miche
ya chai 1,700,000, miche ya kahawa 5,000,000, viuatilifu vya korosho tani
25,000 na viuatilifu vya pamba ekapaki 1,500,000.
Aidha,
kwa mwaka
2015/2016 Serikali ilitoa ruzuku ya pembejeo za kilimo kwa mfumo wa vocha
ambapo kaya za wakulima 999,926 zilinufaika kwa kutumia tani 99,993 za mbolea,
tani 10,270.86 za mbegu bora za mahindi na mpunga vyote vikiwa na thamani ya
Shs. 78 bilioni.
Idadi hiyo ilipungua kwa mwaka 2016/17, serikali
ilisema ingewezesha upatikanaji wa pembejeo za kilimo kwa kuhakikisha
upatikanaji wa tani 400,000 za mbolea, tani 40,000 za mbegu bora, miche bora ya
kahawa na chai pamoja na kuwezesha upatikanaji wa viuatilifu vya zao la
korosho, pamba na mazao mengine.
Licha ya sekta ya kilimo kuchangia
asilimia 29 ya Pato la Taifa kwa mwaka 2015, lakini ukuaji wake ulipungua
ulipungua kwa asilimia 2.3 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 3.4 katika
mwaka 2014 kwa shughuli za kiuchumi za kilimo zinazojumuisha mazao, ufugaji,
uvuvi na misitu.
Wakati ambapo mahitaji ya pembejeo
yanaongezeka kila mwaka kutokana na wananchi kuhamasika kujishughulisha na
kilimo, serikali imeshindwa kuongeza nguvu katika utoaji wa vocha za ruzuku
hasa kwa kuzingatia kipato halisi ya mwananchi wa kawaida, hususan mkulima,
ambaye hana uhakika na soko la mazao yake huku hali ya mabadiliko ya tabia nchi
nayo ikimuathiri kutokana na uhaba wa mvua.
Comments
Post a Comment