Featured Post

AFYA YA WATU CHIMBUKO MAMA LA UTAJIRI WA NCHI



NA ALOYCE NDELEIO
MWANAFALSAFA wa Marekani, Ralph Waldo Emerson, mwaka 1860 aliandika kwamba ‘utajiri wa kwanza kwa nchi yoyote ni afya’.
Kauli hiyo haijakosewa na ndio maana serikali zimekuwa zikihakikisha kuwa inakuwepo wizara inayoshughulikia masuala ya afya ya wananchi wake na kubwa zaidi ni kuwaona viongozi waaandamizi wakifanya ziara katika sehemu zinazotoa huduma za afya.

Mfano upo kwamba hivi karibuni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan hivi karibuni alitembelea Hospitali ya CCBRT ambapo aliafiki kuwa shughuli zinazofanywa na hospitali hiyo ikiwa ni pamoja matibabu ya  kinamama walioathiriwa na fistula.
Linapozunguzwa suala la afya katika mtazamo wa jamii na hata kwenye vitabu, dawa huwa zinakanganywa na maana pana ya afya ya binadamu na njia mbalimbali zinazotumiwa katika kufikia au kupata maana yake halisi.
Katika mantiki ya tiba maana ya afya kwa ujumla huchukuliwa kufuatana na mpangilio wa mamlaka, mfumo wa kawaida wa sayansi, kupimwa na  kupatiwa tiba lakini kwa upande mwingine suala la afya linahitaji pamoja na mambo mengine hali halisi kabla ya vipimo vya kawaida vya kisayansi.
Hatua hiyo pia inakuwa ikihusisha ushiriki na utendaji hali ambayo imekuwa inakanganya kwa kuwa suala la ekolojia na masuala mengine ya kijamii huwa linawekwa mbali.
Kwa mfano mara nyingi tafiti zinazohusu dawa hutoa taswira ya kudharau afya kwa kutoziwezesha au kutoshirikisha jamii katika tafiti hizo.
Hata hivyo kwa mujibu wa tafsiri ya Shirika la Afya Duniani (WHO) iliyotolewa mwaka 1946, afya ni hali ya jumla ya kuwa mzima  kimwili, kiakili na hata  uwezo wa kijamii.
Hata hivyo tafsiri hiyo imeboreshwa baada ya kukosolewa na hata kuwepo  mjadala mkubwa na kuongezea kuwa  ni pamoja na kuhusisha uwezo wa watu kumudu kufikia malengo ya kupata au kupatiwa huduma kuendana au kufuatana na mabadiliko ya mazingira na hata misongo mingine inayojitokeza katika mazingira hayo.
Katika mfumo wa kiekolojia afya ya binadamu ni moja ya vidokezo chanya vya jumuiya ikiwa inahusisha vyanzo na namna ya kufikiwa kwa vyanzo hivyo.
Matokeo muhimu na chanya ambayo yanatupiwa macho ni pamoja na uhakika wa chakula, lishe nzuri, kiwango cha chini cha magonjwa na uwezo katika mpangilio wa uzazi ikiwa ni pamoja na uwezo wa kinamama  kupanga muda wa kubeba ujauzito kati ya mtoto mmoja na mwingine na idadi ya watoto atakaozaa, uwezo na kufikia uelewa, mawasiliano na nguvu au kuwa na mamlaka.
Matokeo ya aina hiyo yanaweza kuonekana kama mwangaza katika nyanja za maji, ardhi na matumizi ya nishati na muundo wa kijamii na kiuchumi pamoja sababu nyingine.
Licha ya kwamba mtazamo wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kuwa afya kamili ni pamoja na kukosekana kwa magonjwa, lakini mtazamo wa kitafiti  kuhusu  afya  unaangalia baadhi ya magonjwa  na vyanzo vyake kama moja ya matukio yanayoungana.
Suala la afya ni muhimu kwa sababu watu wanathamini kuishi maisha marefu na hivyo wanataka kuwa huru dhidi ya vikwazo vya kimwili na akili. Wachumi wa masuala ya maendeleo wamekuwa wakijaribu kila mara kuonesha uhusiano kati ya  kipato na afya.
Nchi zilizo na mapato makubwa  huwa zina idadi ya watu walio na afya njema, ambako kwa kawaida huonekana ni matokeo ya lishe nzuri pamoja na kupatikana kwa huduma ya maji salama, mazingira safi na huduma za afya ambazo zinasababishwa na upatikanaji wa mapato makubwa.
Hata hivyo licha ya afya ya mtu binafsi, afya za wengine pia ni muhimu  kutokana na sababu za kimaadili, kiutashi na kuheshimu ubinadamu  na sheria ya haki za binadamu. Afya ya umma pia ni muhimu kwa sababu michango inayotoa unawezesha kujenga  jamii iliyo imara kijamii na kisiasa.
Kwa mfano kushindwa kwa serikali  kuridhisha watu wake, mahitaji ya msingi ya afya huporomoka na huweza kusababisha kujirudia mara kwa mara kwa udhaifu ambao huishia kuanguka.
Hii ndio moja ya sababu  kwamba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Septemba 2014 lilitangaza Ebola kwamba sio tu janga la afya ya umma bali ni tishio la amani na usalama ikiwa ni tathmini ambayo pia ilifanywa  miaka ya nyuma kuhusu VVU/Ukimwi.
Katika miaka ya hivi karibuni wachumi wameukita uelewa wao kuhusu umuhimu wa afya kiuchumi  kwa kuangalia sekta ya afya kama aina ya mtaji wa binadamu ambao unaweza kuwekwa kwenye matumizi ya uzalishaji kama ilivyo weledi na stadi za watu.
Kutokana na hali hiyo kwa kuwa afya ni kipimo cha msingi cha thamani ya kazi, kitu ambacho ni amana kuu ambayo watu maskini wanayo ni muhimu hususani katika kuongeza uwezo wa mtu binafsi au kaya au kubakia juu ya mstari wa umaskini.
Uthibitisho sahihi wa thamani ya afya kiuchumi unatoka kwenye kuchambua uchumi mdogo kwa sababu ndio unaoingia kwa kiwango kikubwa na ukubwa wa kupima utajiri wa kiafya na kipato  na kinachosababisha vimo ndani yake.
Kwenye tafiti ndogo ndogo ambazo zinaangalia masuala ya afya ya mtu binafsi kwa kuangalia majaribio ya udhibiti ambayo yanaonekana kuwa ni ya kiwango cha juu kwenye baadhi ya maeneo baadhi yamekuwa yakionesha mafanikio mazuri.
Kupambana na minyoo miongoni mwa watoto wa shule, kuongeza madini ya chumvi na madini ya iodine ni miongoni mwa mikakati ya kujenga afya za watoto mashuleni.
Hata hivyo, kutokomeza minyoo kwa wanafunzi na mapambano dhidi ya malaria ambako kumekuwa  kizuizi dhidi ya mahudhurio ya watoto mashuleni kunaongeza tija katika kujifunza kwao.
Tafiti za uchumi mkuu ambazo zimekuwa zinaangalia kwa mapana zaidi ni mara chache zimekuwa zinatumiwa, lakini zimekuwa zinapendekeza kuwa  afya kwa ujumla na afya ya uzazi ni miongoni mwa injini za kukua kwa uchumi na imekuwa inaongeza kiwango cha kuishi.
Hali hiyo inatokana na ukweli kwamba kunakuwepo tija kwenye nguvu kazi, mahudhurio mashule upatikanaji wa elimu na mambo mengine mengi  kwa sababu watu wanamudu kufanya kazi kwa bidii na kutumia teknolojia iliyopo kuanzisha fursa nyingine za ajira na hata kuongeza kiwango cha biashara.
Katika familia ambazo zinakuwa na afya nzuri mafanikio ya kijamii yanakuwepo, hivyo kudfhihirisha kuwa suala zina la afya kuwa ndio utajiri wa taifa.
CHANZO: TANZANITE

Comments