Featured Post

AFRIKA TAJIRI WA MIGOGORO NA RASILIMALI



NA ALOYCE NDELEIO
Mchambuzi mmoja wa masuala ya siasa kuhusu  hali  ya Afrika aliwahi kusema kuwa hili ni bara lililojaliwa utajiri wa rasilimali lakini pia likiwa na utajiri wa migogoro.

Mtazamo wa mchambuzi huyo uliangalia hali ya maeneo mbalimbali ya Afrika ambayo  yamejaliwa kuwa na rasilimali za maliasili na hususan madini, mafuta na gesi asilia kuwa  zilikuwa zimeishia kutonufaika na rasilimali hizo kwa muda mrefu kutokana na kujiingiza kwenye migogoro ya wenyewe kwa wenyewe.
Aidha ni katika hatua hiyo hitimisho linalotolewa kuhusu rasilimali hizo ni kwamba zimegeuka kuwa laana badala ya neema kwani sehemu kubwa ya mapato yaliyotokana  na rasilimali hizo ilitumika au imekuwa inatumika kwenye vita.
Hali kama hiyo nusura  ingeingia Tanzania hususn baada ya kutangazwa kuwa  kiasi kikubwa cha rasilimali ya gesi asilia  kimegundulika kusini mwa Tanzania na kuibua mgogoro kupinga kusafirishwa kwa gesi hiyo kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.
Hali hiyo ilisababisha kuwepo kwa maandamano ambayo yalisababisha hasara za mali pamoja na watu kuumia na kama si kudhibitiwa kwa kutumia vyombo vya dola  hali ingekuwa kama ilivyo kwa nchi nyingine zilizo na migogoro inayotokana na rasilimali hizo.
Hali kadhalika jitihada za kuelimisha jamii kuhusu mikakati iliyowekwa na serikali katika kusafirisha gesi hiyo kulichangia utulivu na jamii kuelewa.
Lakini jambo la kusikitisha ni matokeo ya tume iliyoundwa na Spika wa Bunge Job Ndugai na kubaini kuwepo kwa matumizi mabaya katika mikataba iliyosainiwa katika ya serikali na wawekezaji katika uchimbaji wa gesi hiyo. Hali hiyo nayo inaweza kuwa ni aina fulani ya mgogoro.
Hata hivyo mbali na hali hiyo ambayo ilionesha  taswira ya jinsi ambavyo rasilimali hugeuka kuwa laana jambo ambalo limekuwa likielezwa kutokea kwenye maeneo mengine ya Afrika lakini kwa wakati huu lilionesha taswira yake kwa mara ya kwanza na kwa uwazi.
Lakini licha ya kwamba  lilikuwa halijajitokeza, udadisi ambao umekuwa unafanywa kwenye maeneo  ambayo umefanyika uwekezaji mkubwa wa rasilimali za maliasili umekuwa unaonesha mdororo wa kimaisha miongoni mwa jamii zinazozunguka maeneo hayo ya uwekezaji.
Kwanini  hali inakuwa hivyo  ni kwa kuwa  sehemu kubwa ya mapato imekuwa inaelezwa kuchukuliwa na wawekezaji hao na kujengeka dhana  kuwa  huenda siku zijazo wakaja kuambulia mahandaki yasiyo na kitu.
Aidha taswira nyingine inayojengekea kwenye mazingira hayo ni kwamba pamoja na kuachiwa mahandaki yasiyo na kitu ndani yake mazingira nayo yanakuwa yameharibiwa kupita kiasi na hivyo kubakiwa na kazi nyingine kubwa ya kutunza mazingira.
Lakini hali hiyo yote inatokana na kukubali kirahisi kuingia kwenye mfumo wa uliberali ambao umejengeka katika misingi ya kukomba  rasilimali ambazo  nyingi zimo ndani ya Afrika.
Ndani ya mifumo ya kiliberali  taswira yake huwa ni kuimarisha sera za  kiporaji. Aidha kwa upande mwingine ni dhahiri mazingira yalikuwa yameandaliwa na ambayo yalizilazimisha serikali kujitoa kwenye usimamizi wa uchumi.
Ukweli unabakia kuwa hayo ndiyo mazingira yanayozifanya nchi nyingi za Afrika licha ya kufikisha umri wa zaidi ya  miaka 50 ya uhuru kuendelea  na utegemezi wa kutisha kwa upande mmoja wakati upande wa pili mfumo ukiendelea kuwameza  zaidi   wazalishaji wadogo ndani ya mfumo wa ubepari ambao kwa sasa umepakwa mafuta na kupewa sura ya utandawazi.
Uzoefu wa zaidi ya miaka 25 ya utekelezaji wa sera za uliberali mambo-leo umekuwa unadhihirisha kuwa ni mfumo katili zaidi pengine kuliko hata biashara ya utumwa na ukoloni.
Rasilimali za wanyonge zinaporwa, na wanyonge wanapojaribu kupinga hutumiwa majeshi na serikali zao au za mabeberu. Hayo yapo na kauli za kuwakataza watu au kuwaweka watu mbali na wawekezaji zimekuwa zinatolewa na mara nyingine vyombo vya dola kutumika kuwanyamazisha.
Haya ni mambo ambayo yamekuwa yakitokea barani Afrika na pindi kiongozi anapokuwa hakubaliani na mitazamo ya mababa wa utandawazi ni lazima ataundiwa mizengwe  kwa  kisingizio cha kujenga demokrasia na kubwagwa kutoka kwenye mamlaka kikatili pia.
Mbinu zinazotumika  zilishaonekana nchini mwetu. Pia tumeyaona barani kwetu na duniani kote mifano ikiwa ni uvamizi wa Libya na Iraq uliosababisha kuchinjwa kwa viongozi wa nchi hizo, na mamilioni ya wanyonge kuuawa.
Katika Hotuba ya Mei Mosi iliyotolewa na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1995, aliziita sera za ubinafsishaji na uwekezaji kuwa ni za kinyang’anyi. Akasema kuwa zitazalisha mabilionea, lakini watakuwa wachache. Lakini pia zitazalisha maskini, na hao watakuwa wengi sana. Hayo ndiyo yanayotokea hivi sasa na maeneo mengine duniani.
Lakini kwa upnde mwingine kugundulika kwa rasilimali kama vile za gesi asilia  kunawafumba watawala macho kwa kushindwa kuyaona yaliyopo hivi sasa kwa dhana kwamba ndani ya kipindi kifupi shida hiyo itaisha. Je, mikakati ya mababa wa utandawazi juu ya rasilimali hizo itakubali kunyoosha mikono?
Kimsingi maamuzi tata yasiyojumuisha na ambayo si shirikishi kwa maana ya kuwashirikisha wadau wa aina zote ili nao waweze kushiriki kwa kutoa maoni yao ndio husababisha baadhi ya majanga ambao yanaweza kuelezwa kuwa ni misiba ya kujitakia.
Kwa mfano kama jamii ikielimishwa kuwa kuchakata gesi ambayo inapatakana katika eneo fulani kunahitaji miundombinu ya aina fulani  ili kuwezesha mgawanyo wake  kuwa sawa kwa jamii yote ndani ya nchi kabla ya kuanza kwa zoezi lenyewe mitafaruku inaweza kuepukwa.
Kwa kiwango kikubwa  maamuzi yasiyo ya kidemokrasia  ndio yamesababisha Afrika kuwa na utajiri mkubwa wa migogoro. Tanzania inalijua hilo kwani imekuwa ndio kimbilio la wakimbizi kutokan akatika nchi zilizo na migogoro.
Kitendo au maamuzi tata ya kisiasa na ung’ang’anizi wa madaraka ndio nyenzo kubwa  inayozalisha migogoro na mara nyingine kuishia katika  mapigano ya wenyewe kwa wenyewe  miongoni mwa nchi nyingi.
Ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) utajiri wa migogoro ni moja ya sifa zake.
Pamoja na utajiri mkubwa wa maliasili uliopo ndani ya DRC bado utajiri huo umekuwa hauoneshi kuwanufaisha wananchi zaidi ya mababa wa utandawazi na kuibua utajiri mwingine wa migogoro.
Wakati ikiwepo mikakati ya kufanya chaguzi   za marais na wabunge/wawakilishi  halitakuwa jambo geni  tena kuona  kuwa kauli kwamba Afrika ni tajiri wa rasilimali  na hapo hapo ni tajiri wa migogoro pindi kanuni zinazosimamia chaguzi hizo zitakapokiukwa.
CHANZO: TANZANITE

Comments