- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
NA CONGES MRAMBA, MWANZA
JIJI la Mwanza, Juni 5, liliadhimisha
siku ya Mazingira Duniani huku likiendelea kuacha kiasi kikubwa cha
plastiki kuingia Ziwa Victoria.
Plastiki hizi zinaharibu ubora wa
maji na kuhatarisha uhai wa rasilimali za ziwa hili, wakiwemo samaki.
Kwa mujibu wa Ofsisi ya Uhusiano, Halmashauri ya Jiji miaka
michache iliyopita, ilikuwa ikizalisha kiasi cha tani 357 za taka ngumu kila
siku, na walikuwa wakihifadhi tani 265 tu za taka kila siku, kiasi ambacho
ni takriban asilimia 80 ya taka zote.
Asilimia 20 ya taka hizi zilikuwa hazihifadhiwi, zingine
huingia ziwa Victoria, ambamo hutishia uhai wa viumbe hai wakiwemo samaki.
Jiji la Mwanza lina Halmashauri mbili, Halmashauri ya
Jiji na Manispaa ya Ilemela, ambayo pia inasemwa kushindwa kukusanya taka zote
zinazozalishwa kila siku.
Halmashauri ya jiji la Mwanza imesema imekuwa ikizalisha
tani nyingi za taka za plastiki, huku tani 30 zikiachwa kuingia Ziwa
Victoria kila mwezi, kitu ambacho ni hatari kwa mazingira.
Afisa Uhusiano wa Jiji la Mwanza, Martin Sawema, amesema
juzi kwamba hivi sasa Halmashauri yake imepata wabia ambao hurejereza kiasi
kikubwa cha taka za plastiki, lengo likiwa kuondoa uwezekano wa taka hizo
kuathiri ziwa Victoria na rasilimali zilizomo.
Tayari baadhi ya nchi zimepiga marufuku matumizi ya mifuko
ya plastiki, ikiwemo Rwanda na Kenya ambazo zilipiga marufuku matumizi ya
plastiki mwaka 2014.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Uhusiano ya Jiji, kabla ya wabia
hawa kuja, zaidi ya tani 300 za plastiki zilikuwa zikiingia ziwa Victoria kila
mwaka, na kwamba wanafanya jitihada kurejereza plastikiili zitengeneze bidhaa
nyingine na kupunguza uzalishaji wa plastiki katika maji ya ziwa Victoria.
Sawema anasema, Mwanza ni Jiji ambalo idadi ya watu
huongezeka maradufu kila mwaka, na mwingiliano wa wageni ni mikubwa
unaosababisha biashara kuongezeka huku zikisababisha pia uharibifu wa kutisha
wa mazingira hususan ziwa Victoria ambalo ni chanzo kikubwa cha pato na
chakula cha takriban watu milioni 10 wanaoishi kuzunguka ziwa hili muhimu.
Kulingana na Afisa Uhusiano huyo, jijini Mwanza wakati wa
mchana,kuna kuwa na jumla ya watu milioni moja ambao Ofisa Uhusiano huyo, Sawema,
anasema wanasababisha uharibifu wa mazingira, lakini hadi sasa kuna kila juhudi
kuhakikisha taka za plastiki zinasombwa na kuhifadhiwa ili zitengeneza mbolea
na bidhaa nyingine.
Ziwa Victoria pia huzungukwa na idadi kubwa ya migodi
ambayo uchenjuaji wa madini katika miji na vijiji huhatarisha usalama wa ziwa
hili.
Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) liliwahi kusema,
asilimia 86 ya miradi iliyokuwa inayotekelezwa miaka ya nyuma, ikiwemo
migodi ya madini, Kanda ya Ziwa, ilitekelezwa kinyume cha Sheria,
mingi ilikuwa haina hata vyeti vya ithibati ya mazingira.
Miaka michache iliyopita, Taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa
Baraza la Ulinzi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC), Injinia Bonaventure Baya,
iliyotolewa kwa Wakuu wa Mikoa sita ya Kanda ya Ziwa mwaka jana,
ilisema licha ya miradi mingi kuendeshwa kwa ukiukwaji mkubwa wa sheria za
Ulinzi na Uhifadhi wa Mazingira, asilimia 12 ya miradi hiyo huendeshwa pasipo
kuzingatia sheria, licha ya kuahidi kila mara kwamba kuna mipango ya utunzaji
wa mazingira.
Kulingana na Mkurugenzi huyo wa NEMC, Taarifa yake imetokana
na zoezi la Ukaguzi uliofanywa na Baraza hilo tangu mwezi Mei hadi Julai mwaka
juzi 2016 nchi nzima ikiwemo mikoa ya Mara, Mwanza, Kagera, Geita, Simiyu
na Shinyanga.
Wakaguzi wa NEMC pia walizunguka katika mikoa hiyo ya
Kanda ya Ziwa yenye idadi kubwa ya migodi ya madini, Ujenzi wa Mahoteli makubwa
yanayotiririsha maji taka yenye kemikali, na yenye kuhatarisha usalama wa maji
na viumbe hai katika Ziwa Victoria.
NEMC walisema zoezi la ukaguzi lilifanyika kwa umakini
mkubwa kwa siku 80, wakabaini kwamba asilimia 86 ya miradi mikubwa hapa
nchini, huchafua mazingira.
Zoezi la ukaguzi la NEMC liliendeshwa na Timu ya wataalam
walioongozwa na Dkt. Yohana Mtoni, ndilo Mkurugenzi huyo wa NEMC analosema
lilibaini miradi mingi ukanda wa Ziwa Victoria inakiuka sheria ya Mazingira
Sura 191 EMA, ya mwaka 2004, iliyoanza kutekelezwa rasmi hapa nchini Julai Mosi
mwaka 2005.
Kulingana na Mkurugenzi huyo wa NEMC, Injinia Bonaventure
Baya, zaidi ya miaka 10 imepita tangu sheria hiyo itungwe na Bunge na kuanza
kutumika hapa nchini, lakini hadi sasa miradi inayoendeshwa kwa kuitii, ni
asilima mbili tu.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘PAMBANA NA TAKA ZA PLASTIKI’
kuokoa mazingira.
CHANZO: TANZANITE
Comments
Post a Comment