Featured Post

KOMBE LA DUNIA 2018: WANAWAKE URUSI WATAKIWA KUTOFANYA MAPENZI NA WAGENI

Tamara Plentyova, Mkuu wa Kamati ya Familia, Wanawake na Masuala ya Watoto bungeni


MOSCOW, RUSSIA
MBUNGE mmoja nchini Urusi anasema wanawake wa Urusi hawapaswi kufanya mapenzi na wageni wakati wa Kombe la Dunia huku akionya kuhusu watoto wanaozaliwa kutoka rangi tofauti.

Tamara Plentyova, Mkuu wa Kamati ya Familia, Wanawake na Masuala ya Watoto bungeni, alisema kuwa hata iwapo uhusiano huo utasababisha kufanyika kwa harusi, wanawake au watoto wao watachukuliwa na mwanamume huyo ambaye atakuwa raia wa kigeni.
Mbunge huyo ni wa chama cha Kikomunisti.
"Hata wakiolewa, watawachukua, halafu watashindwa namna ya kurudi," Bi. Pletnyova alisema katika kituo cha Govorit Moskva.
"Baadaye watakuja kwangu, wasichana wakilia kwamba watoto wao wamechukuliwa."
Alisema kuwa wanawake waliopata watoto na raia wa kigeni wakati wa michezo ya Olimpiki ya 1980 mjini Moscow walisalia kuwa wanawake wasio na wanaume.
"Ni vyema iwapo ni mtu wa rangi inayofanana na yako lakini iwapo ni mtu wa rangi tofauti basi kunakuwa na shida."
"Ni muhimu kuwa na watoto wetu," alisema Bi. Pletnyova.
Warusi wenye rangi tofauti walikuwa wakiitwa 'Watoto wa Olimpiki' ama 'Watoto wa Sherehe' baada ya Muungano wa Sovieti kuwaalika Waafrika, watu wa Mashariki ya Kati na raia wa Marekani Kusini.
Warusi wenye ngozi nyeusi hadi leo hukabiliwa na maswali mengi ya ubaguzi wa rangi katika taifa ambapo chini ya asilimia moja ya idadi ya watu ni watu weusi.
Zaidi ya watalii milioni moja wa kigeni wanatarajiwa kuhudhuria Kombe la Dunia, swala linalozua wasiwasi kuhusu ubaguzi wa rangi na wapenzi wa jinsia moja hususan wakati ambapo wanachama wenye msimamo mkali wa Cossack watazuru mataifa yanayoandaa dimba hilo.

Comments