Featured Post

TUMIA MAJANI YA MAHARAGE KUWAANGAMIZA NA KUNGUNI


NA DANIEL MBEGA
USIOMBEE kulala kwenye kitanda chenye kunguni, maana utatamani bora ulale umesimama.
Kunguni ama kwa Kiingereza Bed Bugs, wanakera sana, kwa kung’ata na pia harufu mbaya ya damu yake.
Ndiyo maana ukisikia mtu anasema; “Yule ana damu ya kunguni”, ujue ni damu inayotoa harufu mbaya kiasi kwamba kila mtu hapendi kuisikia!

Uainishaji wa kisayansi unaonyesha kwamba, Kunguni wanatoka katika Himaya ya Wanyama (Animalia) katika Faila ya Arithropoda, yaani wanyama wenye mwili wa pingili na miguu ya kuunga wasio na ugwe wa mgongo kama wadudu mfano wa nge, buibui na mende.
Kunguni wadudu wadogo wanaotoka katika Nusufaila ya Hexapoda (Arithropodi wenye miguu sita), Ngeli ya Insecta (Wadudu), Familia ya Cimicidae katika Oda ya Hemiptera ya nusungeli Pterygota (yaani wadudu wenye mabawa).
Mara nyingi kunguni wanaishi katika vitanda ambamo hufyonza damu ya wanadamu kama chakula chao kikuu, hasa usiku.
Kunguni hawajathibitika kuwa na uwezo wa kuambukiza ugonjwa wowote kwa binadamu, lakini ni wadudu wasumbufu sana hasa nyakati za usiku ukiwa umelala, kunguni balaa.
Imegundulika pia kuwa wadudu hawa huishi vizuri hata sehemu safi, siyo mahali pachafu pekee.
Ni wachache sana kati yetu wanaoweza kusema hawajawahi kuumwa na kunguni kwani wapo sehemu mbalimbali, mahotelini, kwenye usafiri (daladala, treni), majumbani na maofisini pia.
Kinachoshangaza pia ni uvumilivu wa wadudu hao kuishi hata mwaka mzima bila kunyonya damu huku akisubiri mtu apatikane. Kwahiyo hata kama utawakimbia kwa miezi sita siyo suluhisho, ukirudi tu unao!
Madhara pekee yanayoelezwa kuhusu wadugu hao ni mwasho wa ngozi, kuvimba ngozi baada ya kuumwa, matatizo ya kisaikolojia pamoja na dalili za mizio (allergic symptoms).
Unaweza kung’atwa na kunguni usivimbe, lakini mara kadhaa ngozi huvimba kutokana na kujikuna baada ya kung’atwa.
Kunguni hawaruki, lakini wanakimbia sana hata kwenye sakafu, kuta, paa. Kunguni jike hutaka mamia ya mayai ambayo ni madogo mno.
Kunguni wadogo huongeza ngozi yao kwa awamu tano kabla ya kukomaa ndani ya mwezi mmoja au mitatu.
Ingawa wadudu hao wana vimelea vya magonjwa kama tauni na hepatitis B, hakuna ushahidi wowote wa kitaalamu unaoonyesha kwamba wanaweza kusambaza magonjwa kwa binadamu.
Watafiti nchini Marekani wamesema kwamba wamegundua hhupendelea baadhhi ya rangi hasa nyeusi na rangi nyekundu na huchukizwa na rangi ya manjano na kijani kibichi.
Utafiti mpya umebaini kuwa wadudu hao wanaweza kustahimili siyo tu tanuri ya moto na baridi kali bali pia madawa ya kisasa ya kuua wadudu wanaotambaa.
Kunguni wamegundulika kuwa wanaweza kustahimili kupuliziwa dawa nyingi ya sumu kwa kuimarisha uwezo wake wa kujikinga dhidi ya sumu moja baada ya nyingine.
Wadudu hao ambao huishi kwa kufyonza damu ya wenyeji wake wakiwa usingizini wana uwezo mkubwa wa kibaolojia wa kujikinga dhidi ya sumu kali.
Hii ni kusema kuwa kadiri vizazi vya kunguni vinavyopuliziwa madawa yenye sumu ndivyo wadudu hao wanavyoimarisha uwezo wake wakuzuia maafa miongoni mwa watoto wao.
Aidha, watafiti wanaema kuwa vipimo 1,000 vya sumu kali aina ya (neo-nicotinoid) vinahitajika kuua kunguni mmoja huko Marekani katika majimbo ya Cincinnati na Michigan ikilinganishwa na maeneo mengine duniani.
Watafiti hao sasa wanasema kuwa kuna hatari kubwa ya mdudu huyo kuenea kote duniani kutokana na utandawazi na soko huria ambao umefanya ulimwengu kuwa kitongoji kikubwa tu.
Aidha, wanasayansi hao wanashauri kutafutwa mbinu tofauti na mpya ya kukabiliana na kunguni pasi na kutumia sumu, kama vile kutafuta wadudu wengine wanaoweza kuwala ili kuzuia wadudu hao kuenea kote duniani.
Kumuua kunguni sugu inaweza kuhitaji dawa yenye makali mara elfu moja zaidi ya ile inayohitajika kuua wadudu wasio sugu.
Wanaweza kuishi hadi mwaka mmoja bila kula, na yai moja la kunguni linaweza kuzaa kunguni wengi mno.
Hata hivyo, majani mabichi ya maharage yameonyesha uwezo mkubwa wa kuwanasa kunguni kwa sababu yana vinyweleo ambavyo huwanasa kunguni mara wapitapo juu yake. Pia yana uwezo wa kudhoofisha miguu yao na kuwafanya wasiweze kutembea.
Unaweza kutumia majani hayo kwa kutegesha kwenya chago za vitanda na sehemu nyinginezo ambapo yana uwezo mkubwa wa kupunguza uwepo wa kunguni ingawa shaka bado ipo kama yana uwezo wa kuangamiza na kutokomeza kizazi chote.
Kama njia hii itafanikiwa kwa asilimia 100 inamaanisha kupunguza gharama za kutumia kemikali za viwandani ambazo ni aghali ukilinganisha na majani ya maharage ambayo yanapatikana shambani na kwenye bustani zetu.
Tatizo pekee linaloonekana kwenye njia hii ni muda wa kutokomeza kunguni kama wamevamia nyumba yako, njia hii inahitaji muda kiasi tofauti na kemikali ambazo zingeweza kuwaangamiza wadudu mara upuliziapo.
Tatizo la kemikali nalo ni gharama, uchafuzi wa mazingira na pia usugu wa wadudu kwenye kemikali hizi ambazo wakati mwingine hupoteza uwezo wa kuangamiza wadudu.
Jambo lingine gumu kwenye njia hii ni namna ya kuwafanya kunguni wavutiwe na kupita kwenye majani haya, kwani wasipopita juu yake njia hii haitakuwa na faida yoyote hasa ikizingatiwa kwamba, hawavutiwi na rangi za kijani kibichi.


Comments