Featured Post

TATIZO LA MJI WA MIMBA LAMSABABISHIA MARADHI YA AKILI



KWA majuma kadhaa kila mwezi, Lucie alionekana kuwa mtu tofauti-alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya kiakili na kimwili na hakujua kwa nini.
Kwa miaka kadhaa alikuwa akimtafuta daktari ambaye angeweza kumpa majibu ya maswali yake, akiwa na miaka 28 alifanyiwa upasuaji na kuondolewa mji wa mimba.

Kabla ya kuvunja ungo, Lucie alikuwa mpole, mwenye furaha na huru. Lakini kuanzia umri wa miaka 13 alianza kusumbuliwa na msongo wa mawazo, kuwa mtu mwenye hofu.
Pia alianza kujiharibu mwili wake na kukumbwa na mabadiliko ya hisia zake mara kwa mara.
Hivyo, akiwa na miaka 14 aliondolewa kwenye shule ya kawaida aliyokuwa akisoma na kupelekwa kwenye taasisi inayoshughulikia masuala ya afya ya akili.
Mambo yalibadilika alipokuwa mjamzito akiwa na umri wa miaka 16, mimba ya mtoto wake wa kiume, Toby.
"Ndani ya miezi michache ya ujauzito niliondoka hospitalini. Dalili za maradhi yangu zilionekana kutoweka, nilikuwa na furaha, nilijisikia vizuri sana, nilijiona niko vizuri kiakili jambo ambalo lilikuwa la kushangaza."
Hali hii ilikuwa wakati wa ujauzito na wakati wa kunyonyesha-lakini hedhi iliporejea, pia matatizo yale yale yalijirudia.
Miaka michache baadaye, Lucie alirejea kwa ajili ya masomo yake chuoni, lakini kwa wiki chache akashindwa kabisa kumudu masomo akaamua kukatisha.
Baadaye akajiunga na mafunzo ili awe mwalimu msaidizi, lakini wakati huo pia dalili za maradhi yake alishindwa kuzivumilia.
Akiwa na miaka 23, Lucie alipata ujauzito tena wa mtoto wake wa kike, Bella, akajisikia vizuri kiakili, ingawa alitakiwa kukaa tena hospitali kwa miezi kadhaa huku akitapika sana.
Baada ya Bella kuzaliwa hali yake ilirejea kuwa mbaya zaidi.
Alikuwa akihisi maumivu ya viungo, misuli, alikuwa anakwazika na vitu kama sauti, harufu na kugusa pia alikuwa na uchovu sana.
Pia alikuwa na matatizo ya kuwa na mawazo sana, usahaulifu, kujisikia hali ya kukata tamaa.
Mara nyingi alikuwa akikumbwa na mawazo ya kutaka kujiua, vilivyomfanya aanze kuhatarisha maisha yake na kuwa tayari kabisa kujikatisha uhai.
Katika hatua hiyo, Lucie aligundua kuwa homoni zake zilikuwa zinamsababishia matatizo ya akili ambayo wataalam waligundua.
Alikuwa akipatiwa sindano za kila mwezi kwa ajili ya kuondokana na usumbufu aliokuwa anaupata, hatimaye sindano zikawa hazifanyi kazi tena.
Baada ya uchunguzi zaidi, madaktari waliamua kuja na suluhu ya kudumu nayo ni kuondoa kabisa mji wa mimba wa Lucie na Ovari, kabla ya hapo Lucie alikuwa na uhakika kabisa kuwa alikuwa anahitaji kupata mtoto wa tatu, lakini haraka sana aliona kabisa ushawishi unafifia.
Mwaka mmoja baada ya upasuaji, alipata ahueni na kuendelea na masomo yake aliyoyakatisha.
Sasa Lucie anafanya kazi ya ualimu, akifanya kazi ile ile aliyofikiri kuwa hataweza kuifanya.


Comments