Featured Post

TANZANIA YAWEKA MSIMAMO MKALI KWENYE ITIFAKI YA UTALII NA USIMAMIZI WA WANYAMAPORI YA EAC


Waziri wa Maliasili na Utalii wa Tanzania, Dk. Hamisi Kigwangalla (kulia), Waziri wa Utalii, Wanyamapori na Mambo ya Kale wa Uganda, Ephraim Kamuntu (katikati) na wawakilishi wa Mawaziri wa Utalii wa Burundi, Kenya na Rwanda wakisaini Itifaki ya Utalii na Usimamizi wa Wanyamapori ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC) katika ukumbi wa EAC Jijini Arusha. 

Na Hamza Temba-Arusha
..............................................................
Itifaki ya Utalii na Usimamizi wa Wanyamapori katika Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC) imezua mjadala mzito na mabishano makali katika Mkutano wa Nane wa Kisekta wa Baraza la Mawaziri wa jumuiya hiyo uliofanyika Jijini Arusha juzi.

Mvutano huo ulisababishwa na hoja iliyowasilishwa na Tanzania ambayo ilitaka kuboreshwa kwa kifungu cha nne cha itifaki hiyo ambacho kinazitaka nchi wanachama kutangaza eneo lote la jumuiya ya Afrika ya Mashariki kama kituo kimoja cha safari za utalii duniani.

Tanzania ikiongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, ilipinga vikali na hatimaye ikagoma kusaini itifaki hiyo ambayo imejadiliwa kwa zaidi ya miaka saba mpaka pale mapendekezo yake yalipoingizwa kwenye kifungu hicho.

Kifungu hicho kilikuwa kinasema, "Every Partner State shall market and promote the Community as a single tourist destination", (Kila nchi mwanachama itatangaza jumuiya kama kituo kimoja cha safari za utalii (duniani)).

Tanzania ikapendekeza kwenye kifungu hicho uongezwe mstari unaosema, "while maintaining country identites" (huku kila nchi mwanachama ikibaki na utambulisho wake halisi).

Mapendekezo hayo ya Tanzania yaliungwa mkono na Burundi na kupingwa vikali na nchi za Kenya, Uganda na Rwanda ambazo zilisema hakuna madhara yeyote ya kutobadilisha kifungo hicho. Nchi ya Sudan Kusini haikuweza kushiriki mkuatano huo.

Licha ya majadiliano makali yaliyosababisha mkutano huo  kumalizika majira ya saa nne za usiku badala ya saa 12 jioni kwa mujibu wa ratiba ilivyopangwa, wajumbe hao walikubali mapendekezo ya Tanzania na hatimaye itifaki hiyo ikasainiwa.

Awali itifaki hiyo ilijadiliwa kwenye vikao vya wataalam wa jumuiya hiyo na Makatibu Wakuu, siku tatu kabla ya kuwasilishwa kwenye Baraza hilo la Mawaziri.

Akizungumza baada ya mkutano huo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla alisema Tanzania ililazimika kuweka msimamo huo ili kuepuka madhara ya nchi nyingine kutangaza vivutio vyake kuwa viko nchini kwao kama ambavyo nchi ya Kenya imewahi kutangaza mlima Kilimanjaro upo kwao.

Aidha, alisema msimamo huo pia ulilenga kulinda maslahi ya Tanzania kwakuwa ni nchi pekee yenye vivutio vingi na ambayo imehifadhi ardhi yake kwa zaidi ya asilimia 32 ukilinganisha na nchi nyingine wanachama, mfano Kenya ambayo imehifadhi asilimia 7 tu ya ardhi yake.

Mkataba ulioanzisha Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, Ibara ya 115 (1-3) na Ibara ya 116 unaeleza kuwa jumuiya inaweza kuanzisha sera, mikakati na mbinu mbalimbali za kufanya shughuli za utalii na usimamizi wa wanyamapori kwa pamoja, huku kila nchi ikiruhusiwa kubaki na usimamizi, mikakati na sera zake kadri inavyoona inafaa.
 Waziri wa Maliasili na Utalii wa Tanzania, Dk. Hamisi Kigwangalla (kulia), Waziri wa Utalii, Wanyamapori na Mambo ya Kale wa Uganda, Ephraim Kamuntu (katikati) na wawakilishi wa Mawaziri wa Utalii wa Burundi, Kenya na Rwanda wakisaini Itifaki ya Utalii na Usimamizi wa Wanyamapori ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC) katika ukumbi wa EAC Jijini Arusha. 
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiwasilisha mapendekezo ya Tanzania kwenye kifungu cha nne cha Itifaki ya Utalii na Usimamizi wa Wanyamapori ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki katika Mkutano wa Nane wa Kisekta wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya hiyo uliofanyika jijini Arusha. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu, Dk. Aloyce Nzuki.
Baadhi ya wajumbe wa Tanzania walioshiriki mkutano huo.

Comments