Featured Post

TANZANIA YAIELEZA UNESCO UMUHIMU WA UTEKELEZAJI WA MRADI WA KUFUA UMEME KATIKA BONDE LA MTO RUFIJI (STIEGLER’S GORGE)



Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yaeleza umuhimu wa kuendelea na mradi wa kufua umeme katika Bonde la Mto Rufiji (Stiegler’s Gorge) ndani ya Pori la Akiba Selous kwenye Mkutano wa 42 wa Kamati ya Urithi wa Dunia unaoendelea Manama, Bahrain, kuanzia tarehe 24 Juni hadi 4 Julai 2018.
Pamoja na mambo mengine, Mkutano huu unajadili hali ya uhifadhi wa maeneo ya Urithi wa Dunia na kutoa mapendekezo kwa nchi wanachama juu ya namna kuboresha uhifadhi wa maeneo hayo.
Kupitia Mkutano huu, Tanzania imeendelea kusisitiza msimamo wake kwenye Kamati ya Urithi wa Dunia juu ya umuhimu wa utekelezaji wa mradi huo. Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano huo umesisitiza hayo, kufuatia msimamo uliowasilishwa na Maj. Jen. Gaudence Milanzi, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii kwenye Mkutano wa 41 wa Kamati ya Urithi wa Dunia uliofanyika Krakow, Poland, Julai 2017.
Umuhimu wa ujenzi wa mradi huo, uliwasilishwa pia kwenye kikao maalum kati ya wajumbe wa Kituo cha Urithi wa Dunia, Bodi ya Ushauri kwa UNESCO - International Union for Conservation of Nature (IUCN) na Wataalam wa Uhifadhi kutoka Tanzania kilichofanyika tarehe 25 Juni, 2018 Manama, Bahrain. Katika kikao hiki, UNESCO imekubali kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha mradi huu hauleti madhara ya kimazingira.
Aidha, wakati wa majadiliano ya ajenda ya hali ya ya uhifadhi ya Selous, Tanzania ilieleza kuwa, kukamilika kwa mradi huo kutaongeza shughuli za kiuchumi kutokana na kiwango kikubwa cha nishati ya umeme cha Megawati 2100 kitakachozalishwa. Ujumbe wa Tanzania ulifafanua kuwa tayari tathmini ya athari za kimazingira kwenye mradi wa Stiegler’s Gorge imekamilika na kuwasilishwa UNESCO kwa ajili ya upembuzi na kutumia fursa hiyo kulisisitiza Shirika la UNESCO juu ya umuhimu wa maendeleo endelevu kwenye maeneo ya Urithi wa Dunia.
Kwa nyakati tofauti, Tanzania ilipongezwa na Bodi ya Ushauri ya IUCN, pamoja na Nchi Wanachama wa Kamati ya Urithi wa Dunia kutoka kundi la Afrika ambazo ni; Angola, Zimbabwe na Uganda juu ya hatua kubwa iliyopigwa katika kupiga vita ujangili na kuongezeka kwa idadi ya tembo na faru katika Pori la Akiba la Selous. Sambamba na hilo, Serikali za Ujerumani na China zilipewa shukrani kwa kusaidia Tanzania katika kuimarisha ulinzi na uhifadhi katika Pori hilo.
Vilevile, nchi za Afrika ziliunga mkono jitihada za Serikali ya Tanzania katika utekelezaji wa mradi huo na kupendekeza ushirikiano baina ya wataaalam wa UNESCO na Serikali ya Tanzania. Mwisho, nchi hizo zilitoa mkazo juu ya utekelezaji wa ajenda ya maendeleo endelevu yenye kuzingatia uhifadhi wa maeneo ya Urithi wa Dunia.
Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano huo uliongozwa na Maj. Jen. Gaudence S. Milanzi, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii na kuhudhuriwa na Bw. Joseph Kizitto, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira; Bw. Ali Khalil, Katibu Mkuu Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira - Zanzibar; Dkt. Amina Amir, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari,Utalii na Mambo ya Kale – Zanzibar; Mhe. Samwel W. Shelukindo, Balozi na Mwakilishi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Shirika la UNESCO; na Wataalam wa uhifadhi na Urithi wa Dunia kutoka Tanzania Bara na Zanzibar. 

Imetolewa na:
KATIBU MKUU
Maj. Gen. Gaudence Milanzi
28 Juni 2018






Comments