Featured Post

SENEGAL YAITOA AFRIKA KIMASOMASO RUSSIA, YAITANDIKA POLAND 2-1



MOSCOW, RUSSIA
BAO la M’Baye Niang katika dakika ya 60 na lile la kujifunga la Thiago Cionek katika dakika ya 37 yalitosha kuipa Senegal ushindi wa 2-1 dhidi ya Poland na kuitoa kimasomaso Afrika baada ya timu zake nyingine nne kuanza kwa vipigo katika fainali za Kombe la Dunia.

Kama si bao la kichwa la Grzegorz Krychowiak katika dakika ya 86, Senegal wangeweza kukaa kileleni mwa Kundi H, lakini sasa wako sawa na Japan ambao nao mapema jana walipata ushindi kama huo dhidi ya Colombia.
Mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Spartak Stadium ulikuwa wa kusisimua ambao Senegal iliutawala kwa kiasi kikubwa na kuleta matumaini mapya kwa Waafrika.
Timu zote mbili zinashiriki kwa mara nyingine baada ya muda mrefu, ambapo Senegal ilishiriki mara ya mwisho mwaka 2002 wakati Poland ilishiriki mara ya mwisho mwaka 1996.
Vikosi vya timu hizo vilikuwa hivi:
Poland: Szczesny, Piszczek, Pazdan, Cionek, Rybus, Krychowiak, Zielinski, Blaszczykowski, Milik, Grosicki na Lewandowski.
Senegal: N'Diaye, Wague, Sane, Koulibaly, Sabaly, Sarr, N'Diaye, Gueye, Niang, Mane na Diouf.
Katika mechi ya awali ya kundi hilo, bao la dakika ya 73 lililofungwa kwa kichwa na Yuya Osako lilitosha kuipa Japan ushindi wa 2-1 dhidi ya Colombia iliyocheza pungufu kwa dakika 83.
Matokeo hayo yanaifanya Colombia, ambayo iliishia robo fainali nchini Brazil mwaka 2014, sasa inahitaji kuzishinda Senegal na Poland kama inataka kusonga mbele kwenye hatua ya mtoano.
Ni vigumu kuielezea timu iliyocheza vizuri kama Colombia, lakini kwa bahati mbaya vijana wa José Pékerman walijikuta pagumu huku wakimpoteza mchezaji wake Carlos Sánchez aliyelimwa kadi nyekundu kwa kosa la kuushika mpira kwa makusudi zikiwa zimepita dakika mbili na sekunde 56 tu tangu mchezo kuanza.
Hiyo ilikuwa kadi nyekundu ya pili ya mapema katika historia ya Kombe la Dunia tangu Alberto Batista wa Uruguay alipotolewa katika mechi dhidi ya Scotland mwaka 1986 katika dekunde ya 54.
Shinji Kagawa aliipatia Japan bao la kuongoza kwa mkwaju wa penati.
Ikicheza na watu 10 uwanjani huku nyota wake James Rodríguez akishindwa kuanza kutokana na kutokuwa fiti, Colombia hawakutetereka baada ya tukio hilo la mapema na kuonyesha soka la ushindani.
Mpira wa adhabu ndogo wa Juan Quintero ulipenya ngome ya Japan na kutinga wavuni kuipatia bao la kusawazisha mwishoni mwa kipindi cha kwanza.
Lakini Japan walikuja juu kipindi cha pili na mashambulizi yao yalizaa matunda dakika ya 73 wakati Osako alipopachika bao la ushindi kwa kichwa.
Vikosi vya timu hizo vilikuwa:
Colombia: Ospina, Arias, Sanchez, Murillo, Mojica, Cuadrado, Sanchez, Lerma, Izquierdo, Quintero na Falcao.
Japan: Kawashima, Sakai, Yoshida, Shoji, Nagatomo, Haraguchi, Hasebe, Shibasaki, Inui, Kagawa na Osako.


Comments