Featured Post

ROMAN TORRES: SHUJAA ALIYEIPELEKA PANAMA KOMBE LA DUNIA ANAYEPANGA KUWAHANGAISHA ENGLAND

Roman Torres akifunga bao dhidi ya Costa Rica lililoipa Panama tiketi ya Kombe la Dunia. 

MOSCOW, RUSSIA
ENGLAND watakapoingia uwanjani dhidi ya limbukeni Panama katika michuano ya Kombe la Dunia uwanjani Nizhny Novgorod mnamo Juni 24, itakuwa ni karibu miaka miwili tangu waliponyenyekezwa na taifa jingine linaloibukia katika soka - Iceland.

Iceland walipata ushindi wa mabao 2-1 uwanjani Nice katika michuano ya Euro 2016 kutokana na udhaifu wa England na kuchipuka kwa wachezaji wenye vipaji, hatua iliyomfanya meneja Roy Hodgson kujiuzulu baada ya miaka minne.
Nchini Urusi, England watakutana na taifa jingine lisilofahamika sana katika soka ambalo litakuwa linamtegemea sana mchezaji mkabaji ambaye amejizolea sifa si haba.
Roman Torres ni beki wa kati wa miraba minne ambaye hupendwa sana Panama, kiasi cha kuchukuliwa kama nyota wa filamu.
Panama - na Torres - walifikaje hapa? Ni tishio kiasi gani kwa England?
Mwandishi wa BBC Shamoon Hafez alikaa siku moja katika jiji la Panama City, mji mkuu wa taifa hilo la Amerika ya Kati, akiwa na beki huyo anayechezea klabu ya Seattle Sounders.

Kukumbuka bao la ushindi la kufuzu
"Wakati huo ni muhimu sana kwangu na kwa familia," anasema Torres huku akionekana kutazama mbali, na tabasamu usoni, akikumbuka yaliyotokea usiku wa Oktoba 10, 2017 alipofunga bao la ushindi dhidi ya Costa Rica lililoipa nafasi ya kushiriki fainali za mwaka huu.
"Ni jambo la kihistoria, jambo ambalo daima litakuwemo moyoni mwangu na rohoni. Kamwe sitaisahau siku hiyo."
Ulikuwa bila shaka mwisho wa furaha baada ya mechi za kusisimua za kufuzu kwa Kombe la Dunia kutoka eneo la Concacaf.
Wapinzani wao Costa Rica walikuwa tayari wamefuzu kwa michuano hiyo ya Urusi, lakini majirani zao Panama walihitaji bao kufuzu moja kwa moja, baada ya kusawazisha kupitia bao ambalo lilikuwa na utata kuhusu iwapo mpira hasa ulikuwa umevuka mstari kwenye lango.
Wenyeji walikuwa wanatafuta bao la pili kwa udi na uvumba na nahodha wao Torres alipewa ishara na meneja wao Hernan Dario Gomez.
Dakika chache baadaye, bahati ilimwangukia.
Mpira ulimfikia na akafanikiwa kumzuia mkabaji wa Costa Rica, akauruhusu pira udunde kidogo na kisha akatoa kiki kali na mpira ukatua wavuni.
Uwanja wa Estadio Rommel Fernandez ulijaa shangwe.
Torres alivua shati lake nambari tano na kuliinua juu kusherehekea pamoja na wafuasi wa Panama, ambao waliwasha fataki.
Vurugu zilitokea jukwaani, nje ya uwanja na hata eneo la kuketi wanahabari.
"Roman, Roman, Roman," alisema kwa sauti mmoja wa watangazaji wa mpira ambaye alishindwa kujizuia.
Katika vurugu zilizokuwa zinaendelea, mwanamke mmoja mkongwe alishuka kutoka kwenye kiti chake na kuingia uwanjani na kisha akalala chali na kurusha mikono yake juu hewani.
Walinzi wawili wakisaidiwa na mchezaji wa Panama walifika na kumuondoa.
Hayo yalipokuwa yanajiri, Toress alipewa kadi ya njano kwa kusherehekea kupita kiasi.
Ilichukua dakika tatu kabla ya mchezo kuanza tena - na hakukuwa na wakati kwa Costa Rica kusawazisha.
Filimbi ya mwisho ilipulizwa, na Panama wakafuzu kwa mara ya kwanza fainali za Kombe la Dunia.
Miaka minne iliyotangulia, walikuwa wamekosa fursa hiyo wakati wa mechi ya mwisho.
"Ina maana kubwa sana kwa watu wa Panama," anasema Torres, 32.
"Kwa muda mrefu, tumekuwa tukijaribu kufika Kombe la Dunia.
"Miaka minne tulitokwa na machozi na huzuni baada ya kushindwa na Marekani, wakati huu inaonekana ulikuwa wakati wa furaha tu."
Karol Elizabeth Lara, mwandishi wa habari za michezo wa gazeti la Panama America, aliambia BBC Sport: "Watu walishikwa na wazimu baada ya kufuzu.
"Watu walikuwa wanalia na ulikuwa wakati muhimu sana katika historia yetu. Nchi yetu ina watu karibu milioni nne hivi na watu milioni mbili walijitokeza barabarani kusherehekea usiku huo."
Siku iliyofuata ilitangazwa kuwa siku ya mapumziko ya taifa na rais Juan Carlos Varela, huku watumizi wa umma na wafanyakazi katika kampuni za kibinafsi wakipewa muda kupumzika.
Shule zilifungwa siku hiyo.

'Najihisi kama mwigizaji, kila mtu anataka kupigwa picha'
Tores amechezea timu ya taifa ya Panama mechi 100 na ndiye mchezaji mwenye uzoefu zaidi na anayetambulika zaidi kwenye timu hiyo.
Picha zake zimejaa kila pahali katika mji wa Panama City - kwenye mabango, kwenye maduka ya kuuza mavazi ya michezo ambayo anatumiwa kuyatangaza na pia kwenye kadi za kulipia nauli kwenye mabasi.
Tulikutana katika Amador Causeway, pahala bora zaidi pa kutazama meli kubwa za kusafirisha mizigo zikiingia na kutoka mfereji maarufu wa Panama, pahala ambapo Torres anapiga picha za kusaidia kuvumisha mavazi mapya ya nembo yake.
Baada ya kubadilisha mavazi mara kadha na kupokea maelezo kutoka kwa mpiga picha wake kuhusu wapi kwa kusimama na ni wapi pa kutazama, Torres anamalizia kwa kujipiga 'selfie' kadha na kisha kuweka saini yake kwenye jezi za wafuasi wake ambao walikuwa wamemsubiri kwa muda mrefu.
Mlinzi wake ambaye ana bunduki anasalia kila wakati karibu naye, akisikiliza kila neno linalotamkwa.
"Tangu Oktoba, ni kana kwamba nimekuwa mwigizaji wa filamu," anasema.
"Mambo yamebadilika sana, kila mtu anataka kupigwa picha nami. Halinitatizi kwa sababu nafurahia wakati huu pia wa kihistoria nikiwa na timu ya taifa."
Torres alijiunga na klabu inayocheza Ligi Kuu ya Amerika Kaskazini (MLS) ya Seattle Agosti 2015.
Lakini msimu wake wa kwanza alitatizwa na jeraha la goti Septemba.
Alirejea uwanjani Juni 2016.
Mkufunzi wake Brian Schmetzer aliendelea kumuunga mkono alipokuwa anauguza jeraha hilo na alilipa hisani ya klabu hiyo kwa kuwafungia bao lililowashindia Kombe la MLS 2016 kwenye fainali dhidi ya Toronto.
Torres ana kitu cha kumkumbusha hilo daima - pamoja na kitu cha kumkumbusha bao alilofunga la kufuzu Kombe la Dunia - chale (tattoo) kwenye miguu yake miwili.
"Moja ya malengo yangu ilikuwa kutwaa ubingwa wa MLS na nilifanya hivyo," Torres anasema.
"Nilikuwa bingwa, baada ya yote niliyokuwa nimeyapitia, pamoja na jeraha la goti.
"Kisha, kufunga bao hilo la mwisho, ndio maana nina chale za vikombe vyote viwili."
Panama ni taifa la kupendeza, kuanzia visiwa vya San Blas hadi fukwe zenye mchanga mzuri mweusi za Punta Chame na Coronado, pamoja na jimbo lenye korongo, mito na maporomo ya maji la Boquete, karibu na mpaka wake na Costa Rica.
Panama City ni jiji la kisasa lenye majumba mengi ya ghorofa.
Tunapitia katika mitaa ambayo si ya kifahari kama vile San Miguelito na Santa Ana, ambapo maskini huishi. Ni maeneo ambayo Torres alikulia.
Alirejea katika kijiji alimozaliwa Desemba na akakaribishwa kwa shangwe sana.
Alikutana na jamaa, marafiki na kuwapa watoto zawadi.
Torres anaongeza: "Nafikiri hadhi ya taifa hili imeimarika pakubwa, kwangu hili ni jambo muhimu sana, ni muhimu sana kuliona hili likitendeka.
"Kwa watu wengi, hali kwamba tunaenda kucheza Kombe la Dunia itabadilisha mambo mengi sana kwao. Sisi ni mfano mwema kwa vijana nchini mwetu."
Mwanahabari Lara anaongeza: "Roman Torres ni shujaa wa taifa. Ndiye mchezaji bora zaidi na anayetegemeza zaidi timu ya taifa. Ndiye anayefahamika zaidi na watu humpenda.
"Bondia Roberto Duran ndiye mchezaji nambari moja katika historia ya Panama. Torres ndiye pengine wa pili au wa tatu, juu tuna mchezaji wa baseball Mariano Rivera anayechezea New York Yankees."

Kumuenzi Ferdinand na kujiandaa kukabili England
Torres anajutia zaidi kutohamia England mwaka 2010 na 2011.
Blackpool, waliokuwa wanacheza Ligi Kuu wakati huo, na Swansea walimtaka. Alikaa kwa muda akifanyiwa majaribio Nottingham Forest, lakini uhamisho wake haukukamilishwa kutokana na "sababu za kiuchumi".
Licha ya kutia saini mkataba mpya wa miaka miwili Seattle majuzi, Torres bado hajapoteza matumaini ya kuchezea soka England au Ulaya wakati mmoja.
"Kwa sababu hiyo, lazima nijiandae kucheza vyema zaidi kadiri ya uwezo wangu Kombe la Dunia," anasema.
Katika michuano hiyo hiyo ya Kombe la Dunia, atakutana na kikosi kilichojaa wachezaji nyota cha England.
Atakutana pia na washambuliaji nyota lakini hana wasiwasi.
"Mchambuliaji wa England, Harry Kane, ni mshambuliaji mzuri na anacheza vizuri sana kwa sasa na atatakiwa kuwa amejiandaa vyema kimwili na kiakili," anasema.
"Lakini pia lazima tujifikirie wenyewe. Hatuwezi kuwa na wasiwasi, sisi ni timu iliyo na uwezo wa kukabiliana na timu kubwa na tutajiandaa vilivyo.
"Kama beki, ninamuenzi zaidi Rio Ferdinand. Ni mtu ambaye nilikuwa naangazia sana uchezaji wake uwanjani.
"Ndio, kuna watu wengi wanaosema Panama watatatizika Kombe la Dunia, lakini sisi - wachezaji - hatufikirii hivyo. Tunafikiria tu jinsi ya kwenda Urusi na kuandikisha matokeo mazuri."
Costa Rica walifuzu kwa hatua ya mtoano Kombe la Dunia 2014 kutoka kwenye kundi moja na England lakini England wakaambulia patupu.
Torres na Panama wakifanikiwa kufanya hivyo tena, utakuwa ni ufanisi hata zaidi ya huo wa Costa Rica

Comments