Featured Post

RAIS MAGUFULI AWALILIA ASKARI WA JKT WALIOKUFA AJALINI MBEYA



“Kwa masikitiko makubwa nimepokea taarifa ya ajali ya basi la abiria la kampuni ya Igunga Trans iliyosababisha vifo vya vijana wetu 11 Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), askari 1 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na dereva waliopoteza maisha leo tarehe 14 Juni, 2018 majira ya mchana katika mteremko wa Mwansekwa uliopo Mjini Mbeya.

“Vijana wetu wamefariki dunia wakiwa safarini kutoka Tabora kwenda Kikosi cha JKT Itende Mbeya kwa ajili ya kuendelea na mafunzo ya JKT,  tumewapoteza vijana shupavu waliojitolea kulijenga na kulipigania Taifa, nimeumizwa sana na vifo vya vijana hawa na nawapa pole Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini Jen. Venance Salvatory Mabeyo, Mkuu wa JKT Mej Jen. Martin Busungu, familia za marehemu na wote walioguswa na msiba huu.”
Hizi ni salamu za rambirambi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alizozituma kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla, kufuatia vifo vya watu 13 wakiwemo vijana 11 wa JKT waliokuwa wakisafiri kutoka Tabora kwenda Mbeya baada ya basi walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kisha kupinduka katika eneo la Mwansekwa, Mjini Mbeya.
Mhe. Rais Magufuli amewaombea marehemu wote wapumzishwe mahalipe mapeponi, na amewaombea majeruhi wote 25 wa ajali hiyo wapone haraka ili waweze kuungana na familia zao na kuendelea na majukumu ya kila siku.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

Comments