Featured Post

RAIS AAGIZA SH. MILIONI 308 ZITUMIKE KUBORESHA BARABARA


*Ni zile zilizotengwa kwa ajili ya maadhimisho ya Mashujaa 

RAIS Dkt. John Magufuli ameagiza sh. milioni 308 zilizotengwa kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa, zitumike kuboresha  miundombinu ya barabara jijini Dodoma.
 
Ametaja miundombinu hiyo ni pamoja na taa za kuongezea magari  katika barabara ya Kisasa na taa za barabarani kwenye barabara mpya ya Emmaus-African Dream yenye urefu wa kilomita 1.4, ambayo kwa sasa inajengwa kwa kiwango cha lami.

Taarifa hiyo imetolewa na Waziri Mkuu leo (Ijumaa, Juni 29, 2018), wakati akizindua kituo cha polisi kinachohamishika katika hafla iliyofanyika eneo la Kisasa, jijini Dodoma. Kila ifikapo Julai 25 ya kila mwaka Tanzania huadhimisha siku ya mashujaa. 

“Sasa kutokana na msongamano uliopo ambao unaweza kusababisha ajali, Mheshimiwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Magufuli ameamua fedha zote zilizoandaliwa kwa ajili ya maadhimisho hayo zitumike kuboresha barabara,” amesema

Waziri Mkuu amesema Rais Dkt Magufuli anawataka  Watanzania wote waadhimishe siku hiyo ya kumbukumbu ya mashujaa kwa kufanya usafi katika  maeneo yaliyo jirani na makazi yao pamoja na yale ambayo wamezikwa mashujaa ikiwa ni njia ya kuwaenzi.

Kufuatia uamuzi huo, Waziri Mkuu amewaagiza Wakuu wa Mkoa waratibu zoezi hilo kwenye maeneo yao.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameliagizaJeshi la Polisi lianze kujikita kwenye matumizi ya mifumo ya kiulinzi ya kielektroniki yaaniCity Surveillance Sytemsili limudu kudhibiti hali ya sasa ya uhalifu. 

Amesema kutokana na kuwepo kwa mapinduzi makubwa ya kiteknolojia duniani, hususani kwenye nyanja mbalimbali ikiwemo eneo la ulinzi wa raia na mali zao, hivyo ni wakati muafaka sasa kwa Jeshi la Polisi lianze kutumia teknolojia za kisasa.

“Usimikaji wa mifumo hiyo si tu utasaidia kupunguza uhalifu na kuongeza usalama wa wananchi na mali zao lakini pia utaongeza imani kwa wafanyabiashara na watalii wanaotembelea nchi yetu,” amesema.

Pia Waziri Mkuu amewasisitiza wakazi wa eneo hilo kukitumia vizuri kituo hicho ni kwa kupeleka taarifa za uhalifu. “Aidha, naomba niwasisitize kituo hiki ni cha muda, hivyo  uongozi wa eneo hili ni lazima uje na mkakati wa kupata kituo cha kudumu,”.

Ufunguzi wa kituo hicho ambacho ni kati ya vituo vitano vilivyogharimu sh. milioni 250 vilivyotolewa na Benki ya Equity mkoani Dodoma; umehudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni.

Wengine ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Vijana, Ajira, Kazi na Wenye Ulemavu, Anthony Mavunde, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Giles Mroto na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Equity, Joseph Iha.

Comments