Featured Post

PANYA WAVAMIA ATM NA 'KUTAFUNA' PESA INDIA



NEW DELHI, INDIA
MAFUNDI waliofika kuukarabati mtambo wa ATM ambao ulikuwa umeharibika katika jimbo moja nchini India walipigwa na butwaa walipoufungua kubaini tatizo lilikuwa wapi.

Noti za thamani ya rupia milioni 1.2 (takriban shilingi 39,851,300) zilikuwa zimechanwa na kuraruliwa na panya katika benki hiyo Jimbo la Assam.
Polisi wanasema, panya hao pengine waliingia ndani ya mtambo huo kwa kupitia kwenye tundu lililokuwa litumiwe kuingizia nyaya, gazeti la Hindustan Times limeripoti.
Picha zinazoonyesha pesa zilizokuwa zimetafunwa na panya hao katika mtambo huo wa Benki ya Dola ya India katika wilaya ya Tinsukia zimesambazwa sana kwenye Twitter.
Moja inaonyesha mzoga wa mmoja wa panya hao kwenye mabaki ya noti hizo.
Ofisa wa Polisi, Prakash Sonowal, alisema kwamba mtambo huo umekuwa haufanyi kazi kwa siku 12 hivi, gazeti la Hindustan Times limeongeza.
Mafundi waliofungua mtambo huo walikuta noti za rupia 2,000 na rupia 500 zikiwa zimeharibiwa.
Walifanikiwa kunusuru noti za jumla ya thamani ya rupia milioni 1.7 (takriban shilingi 56,407,600), maofisa wanasema.


Comments