Featured Post

MBEGU ZA NERIKA KUKOMESHA MIGOGORO MABONDE YA MPUNGA

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Kebwe Steven Kebwe, akiongea na wataalam wa kilimo kutoka sehemu mbalimbali  wakati wa siku ya mkulima iliyofanyika katika Kijiji cha Kipenyo wilayani Malinyi. Kulia ni Dkt. Sofia Kashenge, Kaimu mtendaji Mkuu wa ASA.

Na Bashiri Salum, Malinyi
WAKULIMA mkoani Morogoro wametakiwa kutumia mbegu za mpunga aina ya Nerika 1, Nerika 2, Nerika 4 na  Nerika 7 ambazo hustawi maeneo ya milimani ili kuondoa migogoro ya kugombania maeneo ya mabondeni ambayo yanatumika kwa kulima mpunga unaotumia maji mengi.

Rai hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Kebwe Steven Kebwe, wakati akiongea katika uzinduzi wa msimu wa kilimo uliyofanyika katika Kijiji cha Kipenyo, Kata ya Mtimbila wilayani Malinyi hivi karibuni.
Katika uzinduzi huo ulioandaliwa na Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA), Dkt. Kebwe aliwataka wakulima kutumia mbegu hizo ambazo zinalimwa katika maeneo ya miinuko na hazihitaji maji mengi.
"Mbegu hizi huchukua siku kuanzia 95 hadi 110 kupanda hadi kuvunwa na hutoa mavuno ya magunia kati ya 14 hadi 48 kwa ekari moja, hivyo zinaweza kuwasaidia wakulima kupata maeneo ya kulima kibiashara na kuendelea kuchangia asilimia ya chakula kinachopatikana hapa nchini," alisema.
Dkt. Kebwe aliwapongeza Wakala wa Uzalishaji wa Mbegu (ASA) kwa namna ambavyo wameweza kutoa elimu kwa wakulima wengi katika mkoa huo na kusisitiza kwamba, pamoja na uvamizi uliofanywa na wadudu waharibifu wakiwemo viwavi jeshi, panzi, panya na ndege aina ya kwelea kwelea, lakini bado hali ya mavuno ni zuri na mchango wa mkoa bado utaendelea kuwa mkubwa katika usalama wa chakula hapa nchini.
Hata hivyo, Dkt. Kebwe aliwasihi wakulima waliopata elimu hiyo kuendelea kuwafundisha wengine na kutumia fursa hiyo kuanzisha viwanda vingi vya kuongeza thamani ya mazao yao na kuwakumbusha kutumia majina ya maeneo yao katika bidhaa wanazozalisha ili kutangaza kuutanga mkoa.
Msimamizi wa Mradi wa huo wilayani Malinyi, Jonson Tilya, alisema kwamba wakala umetoa elimu ya kilimo bora cha mpunga katika wilaya saba za Mkoa wa Morogoro na wamepanda mashamba darasa 21 ya mpunga wa milimani huku wakulima zaidi ya 1,000 wakifikiwa na mradi huo mwaka huu.
"Mradi wa Kuendeleza zao la Mpunga kwa Kuongeza Tija na Uzalishaji (ERPP) unatekelezwa katika ikolojia tatu za mkoa wa morogoro ambazo ni maeneo ya mpunga wa mabondeni, mpunga wa nchi kavu au milimani na mpunga wa maeneo ya umwagiliaji," alisema Tilya.
Hata hivyo, Tilya alisema katika Wilaya ya Malinyi wamepanda mbegu aina tisa (9) za mpunga ambazo ni Nerika 1, Nerika 2, Nerika 4 na Nerika 7 ambazo zote ni kwa ajili ya maeneo ya mlimani au nchi kavu katika maeneo ya mabondeni wamepanda mbegu aina ya supa, TXD 88, Komboka, Tai na TXD 306 (Saro 5) ambapo wakulima wamepata manufaa makubwa kupitia mbegu hizo.
“Jumla ya vijiji 12 vimeshafikiwa na kupatiwa teknolojia hii ya mbegu bora ambapo jumla ya wakulima 220 wamepatiwa elimu kupitia mashamba darasa ili na wao waweze kuwafundisha wakulima wengine wanne kwa kila moja,” alisisittiza Tilya.
Naye Kaimu Mtendaji wa ASA, Dkt. Sofia Kilenga Kashenge, alisema kuwa Wakala umejipanga kuhakikisha walengwa wanapata mbegu kwa wakati na zenye ubora, lengo ilikiwa kuendelea kuboresha kilimo kiweze kuwa na tija.
“Tuna mashamba 91 ambayo mengi yapo kimkakati  ambapo hutumika kuzalisha mbegu, hata kama ukanda mmoja utakuwa una hali mbaya kiuzalishaji, lakini mengine yataendelea kuzalisha mbegu hizo,” alisema Dkt. Sofia.
Aidha, Dkt. Sofia alitanabahisha kwamba, mahitaji ya mbegu yameongezeka kwa kiasi kikubwa ambapo wakala unashirikiana na makampuni mbalimbali ya uzalishaji wa mbegu ili kuhakikisha mbegu zinakuwepo za kutosha kwa mahitaji ya wakulima wote.
Waziri wa Kilimo, Dkt. Charles Tizeba, wakati akihitimisha Hotuba ya Bajeti katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alisema Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) umezalisha tani 784.155 za mbegu bora zikiwemo za nafaka, mikunde na mbegu za mafuta ambapo kati ya hizo, tani 650.045 wameuziwa wakulima.
Katika msimu ujao wa kilimo, Wizara kupitia ASA imepanga kuzalisha mbegu bora za nafaka na mikunde tani 1,800.

Kwa kushirikiana na Sekta binafsi itazalisha tani 1,500 za mbegu bora katika shamba la Mbozi;  vipando bora vya Muhogo pingili 7,000,000 katika mashamba ya Mwele na Msimba na miche bora ya matunda 50,000 katika mashamba ya Bugaga na Arusha. 

Comments