Featured Post

MAREKANI YAJITOA BARAZA LA HAKI ZA BINADAMU LA UMOJA WA MATAIFA



GENEVA, USWISI
MAREKANI imejitoa katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa (UNHRC) na kulitaja kuwa na 'unafiki wa kisiasa na lenye upendeleo'.
"Taasisi hiyo ya "unafiki na upendeleo" inakejeli haki za binadamu," amesema mjumbe wa Marekani katika Umoja huo, Nikki Haley.

Bi Haley mwaka 2017 alilishutumu baraza hilo kwa kuwa na "upendeleo mkali dhidi ya Israel" na kusema Marekani inatafakari uanachama wake.
Baraza hilo lililoundwa mwaka 2006, lililo na makao yake Geneva nchini Uswisi limeshutumiwa kwa kuruhusu mataifa yenye rekodi ya kutiliwa shaka ya haki za binadamu kuwa wanachama.
Lakini wanaharakati wanasema, hatua hiyo ya Marekani huenda ikaathiri jitihada za kuangalia na kushughulikia ukiukaji wa haki za binadamu kote duniani.
Bi Haley alitangaza nia ya Marekani kujitoa katika baraza hilo katika mkutano wa pamoja wa waandishi habari akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo, aliyelitaja baraza hilo kuwa "mtetezi duni wa haki za binadamu".
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, katika taarifa iliyotolewa kupitia msemaji wake, amejibu kwa kusema 'angependelea zaidi' kuona Marekani inasalia katika baraza hilo.
Kamishna wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa, Zeid Ra'ad Al Hussein, ameitaja hatua hiyo ya 'kusikitisha' na habari ya kushangaza mno". Israel, kwa upande wake, imepongeza hatua hiyo.
Hatua hiyo imejiri wakati kukiwa na shutuma kali kuhusu sera ya utawala wa Rais Donald Trump ya kuwatenganisha watoto wahamiaji kutoka kwa wazazi wao katika mpaka wa Marekani na Mexico.

Mshangao zaidi miongoni mwa washirika
Hatua hii ya sasa ya utawala wa Trump huenda ikawasumbua wale wanaoitazama Marekani kulinda na kushinikiza haki za binadamu kote duniani.
Siku zote Marekani imekuwa na mzozano na baraza hilo. Utawala wa George W. Bush uliamua kulisusia baraza hilo lililoundwa mwaka 2006 kwa sababu nyingi kama zinazotajwa na utawala wa Trump.
Balozi wa wakati huo wa Marekani katika Umoja wa Mataifa alikuwa ni John Bolton - ambaye kwa sasa ni mshauri wa kitaifa wa masuala ya usalama wa Rais Trump na mkosoaji mkali wa Umoja wa Mataifa.
Ni mpaka miaka kadhaa baadaye, mnamo 2009, ndipo Marekani ilijiunga upya chini ya utawala wa Rais Obama.
Washirika wengi wamejaribu kuishawishi Marekani isalie katika baraza hilo.
Hata wengi wanaokubaliana na shutuma za muda mrefu za Washington kuhusu taasisi hiyo na wanaamini kuwa Marekani inaweza kuwajibika kuigeuza kutoka ndani, badala ya kujitoa.

Nini UNHRC?
Umoja wa Mataifa uliliunda baraza mnamo mwaka 2006 kuichukua nafasi ya kamisheni iliyokuwepo ya haki za binadamu katika Umoja huo iliyokabiliwa na shutuma kubwa kwa kuruhusu mataifa yenye rekodi duni ya haki za binadamu kuwa wanachama.
Kundi la mataifa 47 yaliyochaguliwa kutoka maeneo tofuati duniani yanahudumu kwa muhula wa miaka mitatu katika baraza hilo.
UNHRC hukutana mara tatu kwa mwaka, na kukagua rekodi ya haki za binadamu ya mataifa yote wanachama wa Umoja wa Mataifa katika mpango maalum ambao baraza hilo husema hutoa nafasi kwa mataifa kusema walichokifanya kuimarisha haki za binaadamu.
Baraza hilo pia hutuma wataalam wa kujitegemea na limeunda tume za uchunguzi kuripoti kuhusu ukiukaji wa haki za binadmu katika nchi kama Syria, Korea Kaskazini, Burundi, Myanmar na Sudan Kusini.

Comments