Featured Post

MARADONA: KOCHA USIRUDI ARGENTINA MKITOLEWA MAPEMA KOMBE LA DUNIA



MOSCOW, RUSSIA
KIUNGO wa zamani wa Argentina, Diego Maradona, ameikashifu timu yake ya zamani kwa kutoka sare na Iceland kwenye mechi yao ya kwanza ya Kundi D siku ya Jumamosi.
Maradona ameilaani timu hiyo na kumtahadharisha meneja Jorge Sampaoli kwamba asirejee nchini Argentina iwapo wataendelea kucheza vile.

Lionel Messi alipoteza penalti wakati timu hiyo ilipolazimishwa sare ya bao 1-1 na Iceland wanaoshiriki kombe hilo kwa mara yao ya kwanza.
Maradona, ambaye pia amewani kuinoa timu hiyo, alikuwa uwanjani Spartak kutazama kipute hicho.
"Nahisi kuna hasira kwenye roho ya timu," alisema.
Licha ya Argentina kuongoza kupitia bao la Sergio Aguero dakika ya 19, iliichukua Iceland dakika nne pekee kusawazisha kupitia Alfred Finnbogason.
"Ni aibu kubwa. Kutojiandaa vizuri ukifahamu wachezaji wa Iceland wana urefu wa mita 1.90," mshindi huyo wa kombe la dunia 1986 aliiambia runinga moja ya Venezuela.
Messi alitarajia kuwa na mchango mkubwa kwenye mchuano huo baada ya mpinzani wake Cristiano Ronaldo kuiinua Ureno kwa kufunga het-triki dhidi ya Uhispania siku ya Ijumaa.
Mbali na kuzimwa na mabeki hodari wa Iceland, mkwaju wa Messi wa dakika ya 63 ulidakwa na kipa Hannes Halldorsson.
"Siwalaumu wachezaji. Naweza kulaumu juhudi zao. Kamwe siwalaumu wachezaji, hata Messi ambaye alijituma," aliongeza Maradona.
"Nimepoteza penalti pia nikiwa Diego Armando Maradona. Sidhani Argentina pia wamepoteza alama kwa kuwa Messi alipokosa bao la penalti," alisema nyota huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 57, aliyeisaidia Argentina kufika robo fainali ya Kombe la Dunia 2010 nchini Afrika Kusini.
Argentina sasa inajiandaa kukwatuana na Croatia kwenye mchuano wao ujao uwanjani Saint Petersburg, kesho Juni 21.


Comments