Featured Post

LUKAKU AIPAISHA UBELGIJI, SWEDEN IKIICHAPA KOREA



MOSCOW, RUSSIA
MABAO mawili yaliyofungwa na Mcongoman mwenye uraia wa Ubelgiji, Romelu Menama Lukaku Bolingoli maarufu tu kama Romelu Lukaku, yaliiwezesha Ubelgiji kuibuka na ushindi wa jumla ya mabao 3-0 dhidi ya Panama katika mechi ya Kundi G ya Kombe la Dunia.

Lukaku, mtoto wa mwanandinga wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Roger Lukaku, alifunga mabao hayo ndani ya dakika sita na kuiwezesha Ubelgiji kuongoza kundi hilo.
Mshambuliaji huyo wa Manchester United alifunga bao lake la kwanza katika dakika ya 69 kwa kichwa na kufuatia na bao zuri dakika sita baadaye akiudokoa mpira juu ya kipa Jaime Penedo.
Dries Mertens ndiye aliyeanza kuifungia Ubelgiji katika dakika ya 47 kwenye Uwanja wa Fisht mjini Sochi.
Panama wanashiriki kwa mara ya kwanza Kombe la Dunia na sasa wataweka mkazo kwenye mechi yao ijayo dhidi ya Tunisia siku ya Jumapili, wakipigania kupata pointi yao ya kwanza kwenye mashindano hayo.
Katika mechi iliyotangulia ya Kundi F, Sweden ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Korea Kusini lililofungwa kwa mkwaju wa penalti na nahodha wake Andreas Granqvist.

 Penalti hiyo ilitokana na Kim Min-woo kumkwatua Viktor Claesson na ilihitaji msaada wa video ili kubaini kwamba ilikuwa ni adhabu kubwa.
Mpira huo wa kasi kwa Korea Kusini uliathiriwa na urefu wa wachezaji wa Sweden ambao walihakikisha mipira yote ya juu wanaimiliki.



Comments