Featured Post

KOMBE LA DUNIA 2018: BAO LA JOSE GIMÉNEZ LAIBOMOA MISRI JUA LIKIZAMA



NA JONATHAN WILSON, EKATERINBURG
BAO lililofungwa na José Giménez katika dakika ya 89 liliua ndoto za Misri kuibuka walau na pointi moja baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Uruguay katika mechi ya Kundi A la Kombe la Dunia mjini Yekaterinburg, Urusi.

Huku nyota wa kimataifa wa Misri, Mohammed Salah, akiwa kwenye benchi muda wote, timu hiyo ya Afrika ilionyesha upinzani mkubwa na kukosa mabao kadhaa, lakini jitihada zao zilivurugwa dakika za mwisho wakati Edinson Cavani alipodondoshwa kwenye wingi ya kulia na kusababisha faulo.
Mpira wa adhabu hiyo ndogo uliopigwa na Cavani ulitua katika kichwa cha Giménez (23) na kuifungia Uruguay bao muhimu, ambalo ni bao lake la tano katika mechi 42 ambazo mlinzi huyo wa Atletico Madrid ameichezea timu yake ya taifa.
Hiyo ilikuwa mechi ya kwanza ya ufunguzi kwa Uruguay kushinda kwenye fainali za Kombe la Dunia tangu mwaka 1970.
Lakini sehemu kubwa ya mchezo ilionyesha kandanda la kimataifa kwa timu zote mbili, ambazo ziliweza kulinda, kushambulia na kumiliki mpira kwa kasi tangu mwanzo mpaka mwisho licha ya uwanja huo kujaa maji kiasi.
Mpira ulionekana kunasa mara kadhaa kutokana na maji hayo na kupunguza kasi ya mchezo, hasa katika ushambuliaji.
Wengi walishangazwa kuona Mo Salah, ambaye jana alitimiza miaka 26, licha ya kufanya mazoezi kwa wiki nzima na kupasha na wenzake kabla ya mechi huku akiwemo kwenye orodha ya wachezaji wa akiba, hakuweza kuingizwa uwanjani.
Siyo kwamba Uruguay hawakuwa na washambuliaji wake mahiri, lakini kuna hisia kwamba Cavani na Luis Suárez, ambao wote sasa wana miaka 31, walipaswa kuipa Uruguay Kombe la Dunia.
Cavani, akicheza pembeni daima, hakuweza kuonyesha cheche zozote miaka ya 2010 na 2014 na alijionyesha mwenyewe kama mchezaji asiyeweza kucheza vizuri kwenye mashindano makubwa ikiwemo kadi nyekundu 'aliyozawadiwa' dhidi ya Chile kwenye robo fainali ya Copa America mwaka 2015.
Walau Suárez alifunga mabao matano katika fainali za mwaka 2010 na 2014, lakini kumbukumbu zake mbili zilizobaki kwenye Kombe la Dunia ni kushika mpira na kung'ata.
Ilikuwa vigumu kutabiri nani angeweza kushinda mechi hiyo, lakini Uruguay ilijionyesha kuwa bora.
Suárez alikosa mabao kadhaa ya wazi ambayo atayajutia, kwani yangeweza kuipatia Uruguay ushindi mnono, japokuwa sasa inashika nafasi ya pili nyuma ya wenyeji Russia ambao katika mechi ya ufunguzi waliichabanga Saudi Arabia mabao 5-0.
Bao la jana lilikuwa la kwanza kwa Misri kufungwa katika Kombe la Dunia tangu lile la Mark Wright wa England 1990 ambalo pia lilifungwa kwa kichwa.
Vikosi vilikuwa:
Misri: El Shenawy, Fathi, Gabr, Hegazi, Abdel-Shafy, Warda, Hamed, Elneny, Trezeguet, Said na Mohsen.
Uruguay: Muslera, Varela, Gimenez, Godin, Caceres, Nandez, Vecino, Bentancur, De Arrascaeta, Suarez na Cavani.


Comments