Featured Post

KISA MAJI, MAMBA WAACHWA WAKITAFUNA VIUNGO VYA WATU



NA MWANDISHI WETU, IRINGA
HAUZIDI umbali wa kilometa moja kutoka nyumbani kwenda shuleni, lakini kwa Iddi Nosa (19), mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Lukosi katika Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, huo ni umbali mrefu.
Pengine akichelewa kudamka anaweza kuchelewa masomo.
Siyo kwamba Iddi ni mzembe. Hapana. Mwanafunzi huyo anatumia magongo mawili kutoka nyumbani kwenda shuleni kila Jumatatu hadi Ijumaa. Ulemavu alionao siyo wa kuzaliwa, bali ni mazingira yaliyomfanya hata ndoto zake nyingine, kama kuwa mchezaji wa mpira wa miguu, kutoweka ghafla.

Sababu ya Nosa kutumia magongo ni kwamba, hana mguu wa kushoto.
Lakini alizaliwa na miguu yote miwili, lakini alipofika darasa la nne, huku akiwa mchezaji hodari wa mpira wa miguu, mamba wa Mto Lukosi aliizima ghafla ndoto yake baada ya kuung'ata mguu wake wa kushoto.
Licha ya kwamba hayakidhi haja, magongo ndiyo yanayokamilisha mguu wake ulioliwa.
Uhaba wa maji kijijini Mtandika, Kata ya Ruaha Mbuyuni, wilayani Kilolo ndiyo sababu kuu iliyosababisha mwanafunzi huyo kukatwa mguu wake.
Kijiji hicho kinategemea maji ya kunywa na ya kumwagilia kutoka katika mto.
Akikumbuka tukio hilo lililompa kilema cha maisha, Iddi anasema: “Baada ya kucheza na muda wa kuoga kufika, nilikwenda mtoni na mdogo wangu kuoga. Ndipo nilipohisi kitu kimekamata mguu wangu, kumbe alikuwa mamba alikuwa ameuuma mguu. Mdogo wangu alipiga kelele ndipo nilipookolewa. Tayari mguu ulikuwa umeshang’atwa ikabidi ukatwe.”
Hali yake aliyonayo, anashauri wanakijiji wa Mtandika na serikali, kukaa pamoja na wadau wengine kwa ajili ya kuleta ufumbuzi wa tatizo la maji. Aidha, amewaomba wasamaria wema wamsaidia baiskeli maalum kwa watu wenye ulemavu ili aweze kuwahi shuleni na kushiriki shughuli nyingine anazoweza kuzifanya katika jamii.
Athuman Nosa, baba wa Iddi, anasema mwanaye alipopatwa na tukio hilo na kutibiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa, matibabu yake yalimgharimu jumla ya Shs. 300,000. Licha ya Iddi kuzowea magongo, baba yake anakiri kwamba yanampa taabu hasa wakati wa kuvuka barabara kuu kuelekea shuleni.
Mbali na Idd, wapo wengi waliokumbwa na zahama hiyo akiwamo Zaituni Ngecha, mama wa watoto wawili, huyu hana mguu wa kulia. Umekatwa wote na ule wa bandia anaoutumia ni mzito kiasi cha kumfanya asiweze kutembea umbali mrefu. Naye amepata kilema cha maisha baada ya kwenda Mto Lukosi kufua nguo na kisha kuoga, huko alikumbana na mamba aliyemsababishia ulemevu huo.
Akielezea mkasa uliomkuta hadi kumfanya kuwa tegemezi maishani yake, Zaituni amesema siku ya tukio, Desemba 19, 2003 alipomaliza kufua nguo, alimweka mtoto kando na kutumbukia ndani ya maji tayari kwa kuoga. Alichukua uamuzi huo kwa kuwa nyumbani hakuna maji na itamgharimu muda kurudi kwa ajili ya kuchota maji akaogee nyumbani.
“Nilipoanza kuoga nilisikia mguu ukivutwa, sikupiga kelele, niliogopa angenimaliza. Alianza kunivuta na kuniingiza kwenye maji na kuninyanyua na kunirudisha kwenye maji hadi nikafanikiwa kujisaidia kwa kushikilia matete huku akiwa anakula mguu wangu…nilipiga kelele ndipo kaka (Rashid) alipokuja kuniokoa kwa kumpiga,” huku machozi yakimlengalenga, Zaituni alieleza.
Kutokana na namna mnyama huyo alivyomjeruhi, mama huyo alipofikishwa kwenye Hospitali ya Mkoa wa Iringa, mguu wote ulikatwa na sasa mguu wa bandia alioupata kwa msaada wa aliyekuwa Mbunge wa Kilolo, Venance Mwamoto pamoja na ndugu zake (wa Zaituni) hawezi kuutumia na kuwaomba wasamaria wema kumchangia baiskeli ili aweze kuendesha maisha yake.
“Kwa sasa mimi ndiye baba, ndiye mama, mwanangu wa pili yuko darasa la nne, malezi ni magumu hasa ikizingatiwa sina kipato, nategemea ndugu ambao nao hawana uhakika wa kunisaidia. Pigo la zaidi ni pale alipofariki mama yangu ambaye alikuwa akinisaidia kulea,” anasema Zaituni ambaye pamoja na kilema alichonacho, anakabiliwa na shinikizo la damu.
Hata hivyo, takribani mita 500 kutoka kwa Ngecha, ni nyumbani kwa Zaituni Nosa, aliyekatika dole gumba baada ya kung’atwa na mamba katika Mto Lukosi.
Kwa mujibu wa mama huyo, Novemba 24, 2008, alikwenda mtoni kuchota maji akiwa na mwanaye lakini alishtuliwa na kitu kilichokamata kidole gumba chake na alipogundua ni mamba, alipambana hadi akaweza kujiokoa.
Nosa (55), anasema, mwezi uliofuata baada ya kupatwa na mkasa huo, mwanaye aliyekwenda mtoni hapo kumsaidia kuchota maji alishambuliwa na mamba maeneo ya ubavu, mkono na mguu lakini hakudhurika kwa kiwango cha kumfanya asiweze kufanya shughuli zake za kila siku.
“Tatizo hapa hapa kijijini hatuna chanzo kingine cha maji ni huu mto pekee japokuwa una mamba. Mabomba hapa ni suluhisho kwetu sisi, tusikwenda mtoni,” anasema mama huyo ambaye pamoja na matibabu ya mwanaye, ilimgharimu si chini ya Shs. 300,000.
Mkuu wa Sekondari ya Lukosi, Naboth Mulimuka, pamoja na shule hiyo kuwa mwanafunzi alipata kilema kutokana na uhaba wa maji, tukio kama hilo limeshawihi kutokea kwa mwanafunzi mwingine kujeruhiwa na mamba na kuhamia mkoani Tanga.
Wanafunzi wa shule hiyo iliyopo takriban meta 750 (robo tatu kilometa) kutoka Mto Lukosi, wanategemea mto huo ambapo Mulimuka ameeleza ni changamoto kitaaluma kwani wasichana waoishi shuleni wanahitaji maji kwa wingi huku mengine yakihitajika kwa ajili ya shughuli za usafi.
“Mwanzoni tulikuwa na wazo hili la bweni kwa ajili ya wasichana kukwepa watu wa mitaani na ujauzito lakini haisaidii kwani lazima wachanganyike huko mtaani wakati wakiwa wanakwenda kuchota maji,” anasema Mkuu huyo wa shule.
Mamba wa Lukosi hawajamdhuru Iddi, Zaituni Nosa na Zaituni Ngecha pekee. Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Mtandika, Rashid Mzemela anasema, hadi sasa jumla ya watu nane wamejeruhiwa na mamba na wengine, wakiwemo Iddi na Zaituni wamepata vilema vya maisha na kuwafanya kuwa tegemezi huku mmoja akiwa ameuawa na wanyama hao wa majini.
Hata hivyo, pamoja na uwepo wa tatizo sugu la maji lililopo Mtandika, bado kijiji hicho hakina kamati ya maji kwa ajili ya maji ya matumizi ya nyumbani. Iliyopo inahusika na umwagiliaji pekee. Kijiji hicho awali kilitegemea zaidi wafadhili lakini maji lakini visima vilivyochimbwa havitumiwi/havifanyi kazi kwa sasa kwani maji yake si salama kwa binadamu. Yana chumvi kali inayodhuru hata mimea.
Mtendaji anasema tatizo hilo limekuwa likimuumiza husani kwa wanafunzi wa sekondari ya Lukosi ambao ili wapate maji, lazima wavuke barabara kuu. Pamoja na kuwashirika hata viongozi wa makanisa na misikiti, bado hakuna ufumbuzi uliopatikana.
Mtendaji huyo anasema, jambo pekee ambalo kijiji kimelifanya ni kuwaelimisha wananchi namna ya kujilinda na mamba ikiwa ni kuaacha tabia ya kuoga mtoni na kuwa waangalifu wakati wakienda kuchota maji katika mto huo.

Sera ya Maji
Kijiji hiki kimepitiwa na chanzo cha kuaminika, mto Lukosi, bado maji yamekuwa ni tatizo la muda mrefu na pengine lililoacha simanzi kuu maishani mwa wakazi wake. Laiti uongozi na wananchi wangeijua na kutekeleza Sera ya Maji ya mwaka 2002, tatizo hilo lingebaki historia.
Kwa mujibu wa sera hiyo, wananchi wanapaswa kuwa wasimamizi na waendeshaji wa miradi ya maji. Kupitia Sheria ya Maji namba 12 ya mwaka 2009, watumia maji wanapaswa kuunda Vyombo vya Watumia Maji ili kusimamia miradi hiyo kwa niaba ya wananchi ikiwemo kukusanya fedha za mradi, kuendesha ama kusimamia vituo vya maji.
Halmashauri ya wilaya katika hili ni kushauri na kusaidia mahitaji makubwa ambayo yameshindikana katika ngazi ya kijiji. Hata hivyo walioathiriwa na hali hiyo wameisihi serikali kukisaidia kijiji hicho kuibua mradi wa kusambaza maji kutokea mto Lukosi kwani kijiji hicho kimeshindwa jukumu hilo.
Mtandika, siyo wananchi wa kawaida pekee bali hata viongozi hawaijui wala kuitekeleza sera hiyo. Hakuna taarifa ambayo imepelekwa katika mamlaka za juu kwa ajili ya kutatua tatizo hilo. Hivyo elimu juu ya yaliyomo kwenye sera na sheria ya maji inapaswa kutolewa  hivi sasa kwa umma.


Comments