Featured Post

KINANA ATOA SIRI TATU KWA CCM KUBAKI MADARAKANI



NA MWANDISHI WETU, DODOMA
ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, ameagwa rasmi na wabunge wa chama hicho huku akiwaachia siri tatu ambazo zitaifanya CCM iendelee kubaki madarakani.

Siri hizo ni pamoja na kutimiza ahadi kwa Watanzania, kujiandaa kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwakani na kujitayarisha kwa uchaguzi mkuu wa 2020.
"Tunafaa kutekeleza ahadi tulizotoa kwa wananchi kwa kuwa ziko katika Ilani yetu ya Uchaguzi, kujiandaa kwa chaguzi ndogo na kujiandaa kwa uchaguzi mkubwa.
"Iwapo serikali itatekeleza ahadi ilizotoa kwa wananchi, wananchi wataendelea kuiamini. Na iwapo serikali itatatua matatizo yanayowakumba wananchi, watahisi kufarijiwa na mtaendelea kuchaguliwa kwa idadi kubwa. Na mwisho wa siku CCM itaendelea kuongoza," alisema.
Kauli hiyo aliitoa jana wakati akiagwa na wabunge hao jijini Dodoma ambayo iliambatana na kumkaribisha Katibu Mpya wa chama hicho, Dkt. Bashiru Ally.
“Hatuna budi kutambua kuwa ili chama kiendelee kupata ushindi, wajibu wetu ni kuendeleza sera zetu nzuri, kuwa karibu na wananchi, kuwasikiliza na kutimiza matarajio yao.
"Pia tutambue wapi tuchukue hatua kutatua matatizo yanayowakabili, yanayowasumbua na yanayowaudhi ili kuwafanya wasipoteze mapenzi na imani na chama chetu na kwa serikali zetu.
"Wametuamini na kutuchagua kwa imani kubwa na kwa matarajio makubwa tuwasikilize na tufanye hivyo kwa unyeyekevu na kwa wakati wote,” alisisitiza.
Kinana aliwaambia wabunge hao kuwa chama hicho kipo madhubuti, kinakubalika na kinaheshimika ndani na nje ya nchi ni bora kwa muundo wake na sera zake.
Alisema miezi sita iliyopita wamehitimisha chaguzi ndani ya chama na katika jumuiya na kwamba safu zote za uongozi na watendaji ndani ya chama zimekamilika.
Kinana alisema kwa kiasi kikubwa anatambua kuwa wabunge wa CCM ni kiungo kikubwa ndani ya chama kwakuwa wamekuwa wakijituma hususani kuwasemea wananchi bungeni na kuishari serikali.
"Bila shaka sitakuwa nawapamba nikitamka kwamba ninyi ndio kiungo muhimu na madhubuti kati ya chama, serikali na wananchi mna nafasi ya kipekee.
"Mnashiriki vikao vyote vya CCM vinavyobuni na kundaa sera na kusimamia uendeshaji wa shughuli zake, mnaishauri, mnaihoji na kuisimamia serikali kuu na za mitaa ili kutekeleza ilani ya uchaguzi.
"Mnawasikiliza na kuwasemea wananchi mnaowawakilisha bungeni na katika vikao mbalimbali. Kazi hii ni nzito na inahitaji kujiandaa, kujiamini, kujituma na kujitolea,” alisema.
Alisema serikali inawategemea wabunge hao katika kutekeleza ahadi za CCM, kuidhinisha bajeti, kupitisha miswada, kutunga sheria, kuridhia taarifa mbalimbali na kutimiza majukumu yake kwa wananchi.
Kinana alisema, CCM ikitimiza wajibu wake kwa ufanisi na wananchi wakaridhika hapana shaka itaendelea kuchaguliwa na kwamba serikali itaendelea kupokea hoja na kero za wananchi wanazoziwakilisha na kufanyiwa kazi ipasavyo.
"Wabunge na serikali mna mpango mmoja na nyote mnategemeana, wabunge wanawawakilisha na kuwatumikia wananchi," alisema.
Alisema kila upande ukielewa hivyo watafanya kazi kwa ushirikiano na kwa umoja na kusisitiza ni lazima kila upande uzingatie na kudumisha kanuni ya kuheshimiana, kuthaminiana na kushauriana.
Aidha, alisema, kwa kiasi kikubwa ushirikiano wa aina hiyo utaleta maendeleo ya haraka kwa wananchi hivyo wakati wote lazima kuepuka kushindana na kuvutana kusiko na tija kwani kwa kufanya hivyo watakaoathirika ni wananchi.
Aliongeza kwamba, kama mijadala itakuwa mikali iwe kwa nguvu ya hoja na kamwe isitawaliwe na kejeli wala vitoisho kutoka upande wowote.
"Bunge letu kama yalivyo mabunge mengine linaendeshwa kwa kanuni zinazoelekeza kila chama chenye wabunge kujitungia kanuni za kusimamia uendeshaji wa shughuli za vyama vyao na wabunge wao.
"Wabunge wa CCM wamejitungia kanuni zinazosimamia na kuongoza shughuli zao bungeni na kukiri kuwa kanuni za wabunge hao ziliandaliwa zaidi ya miaka 20 na zinahitaji kufanyiwa marekebisho kulingana na mahitaji ya wakati walionao," aliongeza.
Hata hivyo, alisema kanuni hizo zipo wazi kuhusu haki, wajibu na mipaka ya wabunge na vilevile zinaelekeza namna serikali inavyotakiwa kuhusiana na wabunge wake na kutimika wajibu wake.
Alisema ndani ya kanuni hizo kuna fursa kamili kwa wabunge wa CCM kutumia haki yao ya uwakilishi na serikali kutetea hoja zake ili kutimiza malengo yake na kwamba msingi mkuu ni kuambiana ukweli, kujenga hoja na nidhamu ya kujituma.
Alisema tofauti za mawazo na maoni zitakuwepo, hivyo itakuwa ni kasoro kubwa kudhani kuwa kutakuwa na chama au serikali ambapo watu wote wanafikiri sawa au wana maoni au kauli sawa kwa kila jambo.
"Tukiwa na watu wa aina hiyo watakuwa ama hawafikiri au si wakweli, na tusiruhusu tofauti za mawazo na maoni kuwa sababu au chanzo cha migawanyiko ndani ya chama au bungeni.
"Isiwe ni nani zaidi bali iwe ni nani ana hoja nzito zaidi na zenye manufaa kwa maendeleo ya taifa letu, ukitaka ushirikiano kutoka kwa mwenzako ni lazima udhihirishe kuwajali na kuonyesha kuwa nao pia wana uelewa na wana umuhimu," alisema.
Alisema jambo la msingi ni kujenga utayari wa kila upande kujitahidi kuelewa, kutafakari na kuheshimu hoja za upande mwingine na kwamba CCM imeendelea kukubalika na kuheshimika kwa kudumisha demokrasia inayoheshimu mijadala ya kina katika kufikia maamuzi.
Kwa upande mwingine, alishauri kamati ni chombo kinachoweka pamoja wabunge na serikali yao, hivyo ni vyema ujengwe utamaduni wa kamati kukutana kwa ratiba.
"Isikutane kwa sababu tu ya kujadili mambo ya dharura, kamati ni jukwaa la kujadiliana, kushauriana, kuambizana ukweli, kukosoana na kujenga mshikamano wa dhati," alisema na kuongeza kuwa hiyo itapunguza kuwepo kwa mifarakano, kushutumiana na kutiliana mashaka.
Alieleza kuwa, kwa nyakati mbili tofauti akiwa Katibu Mkuu aliwahi kumwomba Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli, astaafu nafasi hiyo lakini alimkatalia.
Alisema walipoitisha kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM mwezi Mei aliona amepata fursa nyingine ya kuwasilisha maombi yake ya kupumzika.
Aidha, Kinana alimpa neno Dkt. Bashiru kuwa hana shaka naye hata kidogo na kwamba atapata ushirikiano kutoka kwa viongozi wengine wa CCM na msaada wao kwa kiwango cha juu.
Alisema chama hicho kimekuwa na makatibu wakuu wengi na kila mmoja aliondoka kwa wakati wake na kueleza kuwa wakati wake wa kuondoka na kumwachia mtu mwingine umefika.


Comments