Featured Post

FREEMAN MBOWE ALAZWA BAADA YA KUZIRAI

Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe kulia
Image captionMwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe (kulia)
Mwenyekiti wa chama cha upinzani nchini Tanzania Freeman Mbowe amelazwa katika hospitali ya Muhimbili baada ya kuzirai mapema leo alfajiri.

Mbowe alitarajiwa kuhudhuria kusikizwa kwa kesi yake katika mahakama ya hakimu mkaazi ya Kisutu.
Wakili wake Jeremiah Mtobesya alimwambia hakimu mkaazi wa mahakama ya Kisutu kwamba kiongozi huyo wa upinzani ameugua kwa ghafla .
''Bw Mbowe amelazwa katika hospitali ya Muhimbili'', alisema Mtobesya, kwa mujibu wa gazeti la Citizen..
Idara ya mawasiliano katika hospitali ya Muhimbili pamoja na mkurugenzi wa uhusiano mwema Aminiel Aligaesha wamethibitisha kuwa bwana Mbowe alikuwa amelazwa asubuhi.
''Aliwasilishwa leo alfajiri na familia yake''.
Kulingana na Mtobesya bwana Mbowe ambaye pia ni mbunge wa Hai pia amempoteza nduguye Henry Mbowe ambaye alifariki usiku wa kuamkia siku ya Jumatatu katika hospitali ya Tumaini.
Msemaji wa Chama cha Upinzani Chadema Tumaini Makene ameeleza kwamba taarifa za awali za madaktari zimebaini kwamba bwana Mbowe amekuwa akisumbuliwa na tatizo la uchovu na madaktari wameshauri watu wasimuone kwa sasa ili waweze kumfanyia vipimo vya kina.
Mbowe ameshtakiwa katika mahakama ya Kisutu pamoja na viongozi wengine kwa kufanya maandamano kabla ya kufanyika uchaguzi wa eneo bunge la Kin0ndoni kinyume na sheria, hatua iliowalazimu maafisa wa polisi kupiga risasi juu ili kuwatawanya waandamanji.
Wengine katika kesi hiyo ni katibu mkuu Dkt Vincent Mashinji, naibu katibu mkuu Tanzania bara John Mnyika, naibu katibu mkuu wa Zanzibar Salum Mwalimu na mwenyekiti wa kitaifa wa wanawake Halima Mdee.

Comments