Featured Post

FAHAMU MAMBO AMBAYO WANAWAKE SAUDI ARABIA HAWAWEZI KUYAFANYA



RIYADH, SAUDI ARABIA
WANAWAKE hatimaye wataweza kuendesha magari nchini Saudi Arabia baada ya marufuku kuondolewa tarehe 24 mwezi Juni, lakini mapambano bado hayajaisha.
Awali viongozi wa Saudi walisema wanawake hawawezi kuendesha magari kwa kuwa jamii 'ilikataa'.

Sheria na taratibu zinazoongozwa na wanaume zinaendelea kuathiri maisha yao ya kila siku.Yafuatayo ni mambo matano ambayo wanawake hawawezi kuyafanya wenyewe nchini mwao.
Katika miezi ya karibuni, Saudi Arabia ilishika vichwa vya habari kutokana na mabadiliko kadhaa yaliyofanywa nchini humo ambayo yanawapa uhuru wanawake.
Wanawake waliweza kuhudhuria mchezo wa mpira wa miguu kwa mara ya kwanza.
Wanawake waliruhusiwa kufanya kazi za jeshi na intelijensia.
Wanawake walishiriki mashindano ya baiskeli.
Na hivi karibuni wataweza kuendesha magari baada ya marufuku kuondolewa.
Ingawa nchi hiyo imetoa leseni ya kuendesha magari kwa wanawake- Kundi la wanaharakati wanawake ambao walifanya kampeni kutaka usawa wa kijinsia walikamatwa mwezi uliopita kwa shutuma za kuvuruga hali ya usalama.
Bado jamii inatawaliwa na wanaume.
Hapa, ni mambo matano ambayo wanawake bado hawaruhusiwi kufanya.

1. Kufungua akaunti benki bila mwanamume
Wanawake nchini Saudi Arabia hawawezi kufungua akaunti benki bila ruhusa ya walezi au waangalizi wa kiume.
Mfumo huo umekuwa ukikosolewa vikali na watetezi wa haki za binaadamu ambao wamesema wanawake wanashindwa kufanya maamuzi wenyewe.

2. Kupata Pasi ya kusafiria, au hata kusafiri nje ya nchi
Huu ni mfano mwingine wa mfumodume.
Wanawake wa Saudia wanalazimika kuwa na ridhaa ya kiongozi wa kiume mfano katika familia ili kupata pasi ya kusafiria au kuondoka nchini.
Mfumo huu pia umekuwa ukipewa nafasi kwenye maeneo mengine ya maisha ya wanawake mfano masomo, kazi na hata kwenye kupata baadhi ya huduma za kiafya.
Kiongozi anaweza kuwa baba wa mwanamke, kaka au ndugu wa kiume-kwa mwanamke mjane wakati mwingine mtoto wa kiume anaweza kuombwa ridhaa.

3. Kuolewa au kutalikiana
Ruhusa kutoka kwa kiongozi wa kiume inahitajika kwa ajili ya kuolewa au kutalikiana.
Ni vigumu kwa wanawake kuwapata watoto aliowazaa akiwa kwenye ndoa, kama watoto hao wanaumri wa zaidi ya miaka saba kwa watoto wa kiume na miaka tisa kwa watoto wa kike.
Walezi hao pia wako huru kukataa kutoa ridhaa kwa wanawake.
Wanawake wamelalamika kwa haki zao kukiukwa, wakilazimishwa kutoa mishahara yao kwa wanaume, wakizuiwa kuolewa au kulazimishwa kuolewa.

4. Kunywa kahawa na wanaume mgahawani
Migahawa yote inayowahudumia wanawake na wanaume hugawanyika katika sehemu mbili.
Hivyo, sehemu ya familia na watu wasio na familia (ambao uchukuliwa kuwa wanaume).
Wanawake wote wanapaswa kukaa sehemu ya familia.

5. Kuvaa unachotaka
Wanawake nchini Saudi Arabia wanalazimika kuvaa mavazi ya kufunika nywele mpaka vidole vya miguu wawapo hadharani.
Hadharani hauna haja ya kufunika uso, lakini unapaswa kuvaa kufunika kichwa mpaka vidole vya miguu. Vazi hili huitwa Abaya.
Wanawake ambao hawafuati sheria hii huadhibiwa na viongozi wa kidini
Ni kwenye maeneo machache sana ya maduka makubwa ambayo wanawake wanaweza kuvua abaya.
Mwanzoni mwa mwaka huu, kiongozi wa kidini alisema ''wanawake hawana haja ya kuvaa abaya''-kauli ambayo inaweza kuwa msingi wa sheria za Saudi siku za usoni.
Wanawake wasio wa Saudi wanaweza kuwa huru.
Kisheria wanaruhusiwa kuvaa mavazi ya kiliberali, na kama si Waislamu, wanaruhusiwa kutofunika nywele zao.


Comments