- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Wakati wa kumuomboleza mwanaharakati aliyepigana dhidi ya ubaguzi wa rangi Afrika Kusini, Winnie Mandela, siku moja, kundi la waumini walioonekana kulewa walizua kionja.
Walikuwa wakilia na kuimba "Mama, Mama". Walijitetea kwamba nao pia walikuwa na haki ya kumuomboleza mtu waliyemuenzi sana.
Kiongozi wao alikuwa amevalia mavazi ya kidini.
Hakuwa mwingine ila Papa Makiti kiongozi wa kanisa jipya nchini Afrika Kusini ambalo limekuwa likiwashangaza wengi.
Kanisa hilo linalofahamika kwa jina Gobola (yaani nipe Ulevi ninywe kidogo kwa Lugha ya Kitswana, moja ya lugha rasmi nchini humo) lina mwaka mmoja hivi tangu lianzishwe.
Mwasisi wa kanisa hilo ni Father Tsietsi D Makiti, 53, ambaye kwa sasa anajiita Papa Makiti. Hujieleza kama papa wa kwanza mweusi kutoka bara la Afrika.
Alilianzisha kanisa hilo katika baa moja, na kanisa hilo hufanya ibada zake katika baa na vilabu.
Aliambia mwandishi wetu wa Afrika Kusini Omar Mutasa kwamba kanisa la Gobola na ulevi, vyote ni vya Mungu na ni wajibu wake kuwapa nasaha bora walevi wote waliofukuzwa kwenye makanisa mengine.
Kanisa kuu la Gobola limo ndani ya baa inaitwa Freddie's Tarvern na mwenye baa hiyo Askofu Freddie Mathebula ndiye naibu wa Papa Makiti, husaidia kuongoza mahubiri na ibada wakati mwingine.
Tangu kuanzishwa kwake, kanisa hilo limekuwa likipata umaarufu na inakadiriwa kwamba kwa sasa lina waumini kati ya 500 na 2,000, ingawa idadi yenyewe ni vigumu kuithibitisha.
'Huu ni ukumbi kwa watu kuja pamoja kwa jina la Mungu bila kuaibishwa kwa kuwa walevi," anasema.
'Pombe si mbaya, watu ndio wabaya'
Mwezi Machi mwaka huu, wakati akitawazwa kuwa papa, aliandika katika Facebook: "Ni kwa nini watu wanalichukia kanisa la Gabola, kana kwamba ndilo lililoleta pombe duniani, na kuanzia wakati huo kwamba pombe ikawepo?
"Ninataka kukariri kwamba hakuna chochote kibaya kuhusu pombe au unywaji pombe, iwapo mtu ana tatizo akiwa mlevi, ni mtu huyo mwenye tatizo si pombe, msiilaumu pombe.
"Mnasema kwamba pombe husababisha vita, ajali, watu kupigana nyumbani na uzinzi, si kweli hata kidogo. Mambo haya yote huwatokea hata watu wasiokunywa pombe…wapita njia hugongwa na magari, baadhi (ya madereva) huwa si walevi, watu kupigana na mizozo mingine hivi vyote vipo hata katika makanisa yasiyotumia pombe kama kanisa la Gabola."
Kanisa la Gobola lina watu wa tabaka mbali mbali wanaume kwa wanawake na ndani yake kuna vyeo sawa na ilivyo kwenye makanisa na madhehebu mengine.
Mfano wamo mapasta, makasisi na maaskofu lakini hakuna kadinali.
Kila siku ya Jumapili ndipo wasaidizi wa Papa Makiti wanapovalia rasmi mavazi yao ya upadri.
Tulipomwuliza Papa Makiti idadi ya baraza la wasaidizi wake hao alisema wapo wengi tu na kila jumapili yeye huwatawaza wanachama wa kanisa la Gobola kuwa makasisi na mapadri na kuwavalisha majoho meusi.
Lakini mwenyewe anasema siyo hoja kujuwa wapi walikosomea mafunzo ya dini ya Kikristo kuweza kupewa vyeo hivyo jambo ambalo Baraza kuu la makanisa Afrika Kusini huwa linalisisitiza kwamba ni muhimu katika kanisa lolote lile.
Baraza hilo lenye makao yake mjini Johannesburg halikubaliani kabisa na mafundisho ya kanisa la Gobola na limesema kwamba ni njia moja ya kuwapotosha wafasi wa dini ya Kikristo.
Papa TD Makiti naye amekua akiwalaumu viongozi wa baraza la makanisa kusini mwa Afrika kuwa hawana mamlaka ya kumshutumu wala kumhukumu kwa anayoyafanya.
Amesema mwenye uwezo wa kumhukumu ni Mwenyezi Mungu peke yake, na kwamba ni dhambi kubwa kwa hao wanaomtuhumu na adhabu yao watakwenda motoni.
Sherehe ya ubatizo
Wakati Papa Makiti akisema hayo, wakati tukimhoji, wafuasi wake wanamshangilia kwa vifijo na nderemu na kusema 'Haleluya kanisa la walevi lidumu'.
Kwa mujibu wa katiba ya Afrika Kusini, kila mtu ana haki ya kuabudu anavyotaka na ndipo kila kukicha nchini Afrika Kusini kunaibuka makanisa mapya kama uyoga ili mradi mtu mhusika asiingilie dini za watu wengine.
Sherehe inayo wafurahisha wengi katika kanisa la Gobola ni Papa TD Makiti anapoanza kuwabatiza wanachama wapya wa Kanisa la Gobola.
Huwa anawapaka kileo usoni mwao huku akiwausia siku zote walitetee kanisa la Gobola. Mapadri na wahubiri wa kanisa hilo pia hutawazwa kwa kutumia kileo, kila mmoja kwa kileo akipendacho.
Miongoni mwa wanachama wapya wa Kanisa la Gobola (ambalo wakati mwingine huandikwa Khabula) ni Bi Lydia mke wa Papa Makiti.
Yeye alikataa kunywa ulevi isipokuwa soda ya Coca Cola.
Wanachama wa Kanisa la Gobola wote ni wachangamfu, wacheshi na wenye maneno mengi mazuri na mabaya na siyo rahisi kiongozi wao Papa Makiti kuwanyamazisha wanapoanza kupiga gumzo na kupiga kelele ndani ya baa hiyo iliogeuzwa kuwa Kanisa kuweza kuwaleta pamoja walevi wote kuwa na msimamo mmoja.
Wakati mwengine imekuwa ikimlazimu Pope Makiti hata kuwapiga makofi kama watoto wadogo na kuwambia wanyamaze huku akiamrisha hata wengine watolewe nje ya Kanisa la Gobola kutokana na utovu wa adabu.
Kuwatia adabu waumini
Mmoja ya wanachama wa Kanisa la Gobola alikuwa akipiga makelele na kusema ovyo ovyo baada ya kunywa kileo kwa wingi, ndipo Pope Makiti akamzaba makofi na kuamrisha atolewe nje ya Kanisa.
Mwandishi wetu Omar Mutasa alimfuata nje kusemezana naye.
Mwumini huyo alisema inashangaza kumuona papa mzima, mtu wa Mungu anapiga watu makofi bila sababu.
"Tangu lini papa wapige watu makofi kanisani? Papa Makiti amenivunjia heshima na uhuru wangu wa kuabudu na njia peke ni kumshitaki polisi Papa Makiti kwa kosa la kumpiga makofi mtu mzima," alilalamika.
Hatukufuatilia kubaini iwapo alifika kwa polisi, lakini ikizingatiwa kwamba alisema hayo akiwa amelewa, msomaji unaweza kujiamulia mwenyewe yaliyotokea baadaye.
Papa Makiti anasema Kanisa la Gobola halitaki kutegemea sana misaada kutoka kwa wahisani na ndio mana wanawahimiza wanachama wao kununua pombe kwa wingi, kutoka duka lao lililopo ndani ya kanisa na hivyo kulifanya kanisa la Gobola kulipa kodi ya serikali.
Katika kanisa hilo, watu huwa hawatoi sadaka, mapato hutoka kwa mauzo ya bia na vileo vingine.
Kwa upande mwengine Kanisa la Gobola halina tofauti na makanisa mapya yanayoanzishwa Afrika Kusini kila kukicha kama kitega uchumi, viongozi wao kutajirika sana na wengine kumiliki hata ndege za kibinafsi.
Wana pia nyimbo zao walizotunga wenyewe, miongoni mwake Gabola Mpepe unaosema 'Ninapoonja kidogo, huwa na lewa lewa, hii haina maana kwamba huwa sifuati njia iliyonyooka'.
Papa TD Makiti anasema yeye bado ni mwanajeshi wa jeshi la Afrika Kusini (SANDF) akiwa na cheo cha Kapteni na alikuwa Jamhuri ya DRC akihudumu katika jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa.
Anasema akiwa huko ndipo alipowasaidia wanawake wa DRC kwa kuwajengea Kanisa waweze kuhishimu na kuzingatia dini ya Kikristo ili kuacha biashara ya kuuza miili yao (ngono).
Juhudi zetu za kutaka kuthibitisha iwapo Papa Makiti bado ni mwanajeshi, amefukuzwa jeshi au alistaafu hazikufua dafu.
'Walevi wote ni wanachama'
Kwa sasa Kanisa la Gobola lipo na linatarajiwa kuendelea kuwepo na wengi wa wanywaji pombe, bia na vileo vikali ukizungumza nao kuhusu kanisa hilo wanakwambia ni mpango mzuri walevi nao wajihisi wana kundi la kuwatetea.
Kanisa la Gobola linasema kila mlevi nchini Afrika Kusini ni mwanachama wa kanisa hilo na wala haina haja ya kujua kuna idadi ya walevi wangapi walio nchini humo.
Wote wanakaribishwa kwa mikono miwili ya Papa Makiti mkono wa kulia ukiwa na chupa ya kileo na mkono wa kushoto ukiwa na kitabu cha Biblia.
Ili kuwa mwanachama kamili lazima Papa Makiti akubatize kwa pombe unayoipenda zaidi, inaweza kuwa Johnnie Walker Red Label, Guinness, Smirnoff na kama ingekuwa Afrika Mashariki pengine Serengeti, Castle, Tusker au hata Konyagi.
"Iwapo wewe hunywa bia, basi unabatizwa kwa bia," Papa Makiti anasema.
"Vile vile kwa wale wanaokunywa cider na vileo vingine."
CHANZO: BBC/SWAHILI
Comments
Post a Comment