Featured Post

CASTER SEMENYA KWENDA KORTINI KUTETEA JINSIA



JOHANNESBURG, AFRIKA KUSINI
BINGWA wa Olimpiki wa mbio za meta 800, Caster Semenya, anatarajia kwenda mahakamani kwa lengo la kudai "haki" dhidi ya sheria zinazoathiri wanariadha wa kike wenye kiwango cha juu cha homoni za kiume.

Shirikisho la Riadha Ulimwenguni (IAAF) limeelekeza kuwa wanariadha wa kike wenye viwango vya juu vya homoni za kiume wanapaswa kuchuana na wanaume badala ya wanawake, ama wabadili michezo, vinginevyo wawe katika matibabu maalum.
Semenya (27) atafungua kesi katika Mahakama ya Usuluhisho wa Michezo, pia amenukuliwa akilalamika: "Si haki, ninataka kuendelea kwenye riadha kama ilivyo kawaida yangu, vile nilivyozaliwa."
Anasema yeye ni Mokgadi Caster Semenya, anakiri kuwa yeye ni mwanamke tena mwenye kasi zaidi michezoni.
Uamuzi huo, ambao unatarajiwa kuanza kutumika Novemba Mosi, 2018, unawahusu wanariadha wanawake wanaokimbia kuanzia meta 400 hadi 1,500.
Semenya, mshindi mara mbili wa michuano ya Olimpiki na mshindi mara tatu wa dunia katika riadha, siku za hivi karibuni amejikuta katika wakati mgumu pale alipopewa ushauri wa kwenye kufanyiwa uchunguzi na kiongozi mkuu wa riadha ulimwenguni kisha ajulikane yeye ni wa jinsi gani, ingawa mpaka sasa haijatanabahishwa hadharani dhidi ya jinsi yake.
Viwango vya juu vya homoni husababisha umbo la mwanamke kushupaa na kuonesha misuli, kuwa na nguvu nyingi, na kiwango cha juu cha chembe chembe nyekundu za damu kinyume na ilivyozoeleka na huathiri kikomo cha uvumilivu.
Mwanasheria Norton Rose Fulbright atamuongoza Semenya katika suala zima la sheria, na inatarajiwa kufunguliwa huko Lausanne mwanzoni mwa wiki ijayo.
Imearifiwa kuwa, Semenya kama walivyo wanariadha wengine, anapaswa kuchuana upande wa riadha kama alivyozaliwa bila kumbagua ama kulazimishwa kubadilisha mwili wake kwa njia yoyote ya matibabu.


Comments