- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
NA ALOYCE NDELEIO
Shughuli nyingi za uchumi zinalenga kupambana na
umaskini, hata hivyo miongoni mwa misingi ya kupambana na umaskini ambayo
mchango wake umejificha ni muunganiko wa bioanuai katika kupunguza umaskini.
Umaskini kwa mtazamo rahisi uliozoeleka, unaelezwa na
unapimwa kuwa ni ukosefu wa kipato au mapato, hata hivyo maana hiyo ni finyu
mno kwani umaskini unaomkabili binadamu ni dhana ambayo inahusisha mambo mengi
ya umaskini uliopo ndani ya nchi zote maskini na tajiri.
Kutokana na hali hiyo umaskini unaweza kuelezwa kuwa ni
ukosefu wa nafasi au fursa zinazomwezesha mtu kuchagua kuishi maisha ambayo
binadamu anaweza kuwa na sababu na kudai kuwa anayaishi na anayathamini.
Kwa mujibu wa vidokezo vya umaskini (HPI) kwa nchi
zinazoendelea inaelezwa kuwa umaskini ni kunyimwa au kukosekana kwa dhana za
maendeleo ya binadamu, kulingana na vidokezo vya maendeleo ya binadamu
(HDI) ambavyo vinajumuisha umri wa kuishi,
uelewa na viwango vizuri vya maisha.
Bioanuai kwa upande wake ni uwiano au kuwianika uliopo
kati ya binadamu na viumbe hai - uwiano ambao unajumuisha uhusiano kati ya
binadamu na mfumo mzima wa ikolojia.
Kwa mujibu wa Azimio la Umoja wa Mataifa juu ya Bioanuai
ni uwiano huo unahusisha aina tofauti za viumbe hai kutoka vyanzo tofauti
ukijumuisha viumbe wanaoishi juu ya ardhi.
Kadhalika hujumuisha viumbe wanaoishi ndani ya maji na mfumo mzima wa maisha ndani ya maji na
sehemu zote ndani ya mfumo wa ikolojia wa maji ambazo ni sehemu yake na kujumuishwa
ndani ya mfumo mzima wa ikolojia.
Uhakika wa chakula
Bioanuai ni msingi imara wa uhakika wa chakula hivyo
kwamba uharibifu wake unaweza kuwa na madhara kwa jamii maskini.
Hiyo ni kutokana na sababu kuwa kiwango kikubwa cha
vyanzo vya vyakula hutokana na vyakula asilia ambavyo hutoka kwenye mfumo wa
ikolojia ambamo ndimo binadamu anaishi.
Hata kwa jamii ambazo si mara kwa mara hutegemea mazao ya
vyakula kutoka eneo husika ambalo inaishi hugeukia vyakula asilia pindi hali ya
uhaba wa chakula inapojitokeza.
Kwa mtazamo mpana bioanuai ni sawa na hifadhi kuu ya
uhakika wa chakula kwa jamii yote ya binadamu kwa sababu wanyama wanaofugwa na
wanyama mwitu huwezesha kuzaliwa au kukua kwa vyanzo vya vinasaba ambavyo ni
muhimu katika uzalishaji wa chakula.
Hali hiyo ndiyo inawezesha kukidhi mahitaji ya chakula
duniani na kuanzisha aina kadhaa za vyakula ambavyo vinaweza au huwa vinaendana
na mazingira halisi ya eneo husika.
Mshikamano wa udongo, udhibiti halisi wa mazingira na
magugu au ndago, lishe ya samaki na mifugo na mtawanyo wa chavua, zote hizi ni
huduma za kilimo zinazotolewa na bioanuai.
Kimsingi ili kuwepo kwa uhakika wa chakula na maendeleo
ya binadamu kwa jumla kunategemea matumizi mazuri na endelevu ya bioanuai.
Uboreshaji wa Afya
Asilimia kubwa ya dawa za kisasa zimepatikana kutokana na
malighafi ambazo zimo au kwa maneno
mengine zimehifadhiwa ndani ya mfumo wa asili wa ikolojia.
Jamii zimeweka matumaini yao na zinategemea kuwa dawa
mbalimbali zitavumbuliwa kutoka kwenye mfumo mzima wa ikolojia kwa ajili ya kukabiliana na magonjwa
yanayotokeza ndani ya mfumo wa bioanuai.
Mahitaji ya afya kwa jamii maskini ulimwenguni hususani
tiba na dawa zinapatikana kwenye vyanzo asilia.
Hivyo uharibifu wa bioanuai humuathiri binadamu moja kwa
moja kutokana na gharama na njia za kawaida za tiba au dawa kuwa zimeingiliwa
na kuharibiwa na shughuli za binadamu.
Mfano hai upo miongoni mwa makabila mengi nchini Tanzania
ambayo hutumia mimea au sehemu ya mimea kwa ajili ya tiba ya mifugo yao.
Miongoni mwa Wandali katika Wilaya za Mbozi na Mbeya
Vijijini mimea kama Maafipila - kwa ajili ya mifugo iliyovimbiwa, Nakavumba - kwa ajili ya kupunguza homa.
Isyogoti - kwa ajili ya tiba za vidonda , Iporotwa - kwa ajili ya ng’ombe aliyevimbiwa, aidha
magome yake yakiwa yametwangwa na kuchanganywa na tumbaku hutumika kama tiba kwa mnyama aliyeng’atwa na
nyoka.
Lowoka- Maji yanayotokana na majani yake hutumika kwa
ajili ya kufunga kuharisha.
Miongoni mwa Wasangu huko Rujewa, Wilaya ya Mbarali mmea
kama Ngayewa- majani yake yakiwa yametwangwa na kuchanganywa na maziwa mtindi
hutumika kama tiba kwa mnyama aliyeng’atwa na mbwa anayehisiwa kuwa na ugonjwa
wa Kichaa cha Mbwa.
Aidha, tiba hiyo hufanyika
mara tu tukio linapotokea na kama ikiwezekana utekelezaji usiwe ni chini ya
siku tatu tangu mnyama ang’atwe.
Miongoni mwa Wachagga kuna Nduo- mizizi ya mmea huu
hutumika kama tiba ya minyoo kwa mbuzi, pia binadamu hutumia kama tiba ya
maumivu ya tumbo, jino, homa na hata kwa kung’atwa na nyoka; aidha majani yake
hutumika kama tiba kwa maumivu ya sikio, jeraha kwa kujikata au kidonda.
Mimea mingine miongoni mwa Wachagga kama Mkuu - maji yanayotokana na majani yake hutumika
kama tiba kwa mnyama anayeharisha.
Msingo- majani yake ni tiba ya ugonjwa wa vidonda vya
midomo na miguu na maji kutoka kwenye majani hayo hutumika kama tiba ya homa ya
East Coast.
Hali kadhalika ipo mimea ambayo ina majina yanayofahamika
kwa lugha ya Kiswahili kama Yasmini ambao majani, mizizi na magome yake
hutwangwa na kutumika kama dawa kwa mnyama aliyeng’atwa na nyoka.
Utupa ni mmea ambao maji yanayotokana na majani yake yana
sumu kali na hutumika kunyunyizia mbogamboga dhidi ya wadudu hususani katika
jamii zinazozingatia kilimo hai.
Matumizi hayo huwa ni mbadala wa viuatilifu vingine
vinavyotokana na kemikali na ambavyo vinaweza kuwa na madhara kwa walaji.
Hata hivyo baadhi ya makundi ya jamii hutumia vibaya mmea
huo katika uvuvi ambao mara nyingine huangamiza hata samaki wadogo.
Iko mimea lukuki ndani ya jamii ambayo ni ya manufaa
katika nyanja ya tiba baadhi ikiwa inafahamika na mingine ikiwa bado
haijafahamika hivyo kuwa ni moja ya hazina ambayo haijaguswa.
Kutokana na hali hiyo maskini ndiyo kundi la kwanza
huathirika zaidi na matokeo hasi ya uharibifu wa mfumo wa ikolojia ambayo
yanajumuisha vitendo vya uchafuzi wa hali ya hewa na maji.
Kadhalika huathiriwa na uhaba au upungufu wa maji na
vyanzo asilia na magonjwa ambayo yanaenea kwa kasi kutokana na uharibifu au
kuingiliwa kwa bioanuai.
Mabadiliko ya vyanzo vya vyakula si tu kwamba ni muhimu
kwa uhakika wa vyakula bali pia uboreshaji wa afya ambayo kwa asilimia zote
hutegemea bioanuai.
Kuongeza mapato utegemezi wa jamii kwenye vyanzo asili
unatofautiana kutoka jamii moja kwenda jamii nyingine hususani miongoni mwa
jamii maskini na nchi maskini kwa jumla.
Sehemu kubwa ya kukua kwa uchumi wa dunia unategemea
uvunaji sahihi na utunzaji wa maliasili.
Jamii maskini ndiyo ya kwanza kuumia kutokana na
uharibifu kwa sababu muunganiko uliopo kati ya maisha yao na bioanuai ni wa
moja kwa moja na vyanzo asilia ndiyo msingi mkuu wa vyanzo vya mapato kwa jamii
hizo.
Utegemezi huu unaweza pia ukawa ni faida kwa kuwa
bioanuai inatoa fursa kwa maendeleo ya bidhaa ambazo ni za kipekee na adimu
ambazo kwa njia moja au nyingine thamani yake ni kubwa.
Hata hivyo faida hizi hivi sasa zinanufaisha baadhi ya
wanajamii wenye nguvu au uwezo ambao wamo ndani ya jamii yenyewe.
Kupunguza majanga
Mafuriko, maporomoko, moto ndani ya misitu na majanga
mengine ya asili yanachochewa katika mtiririko wake na athari au yanapata kasi
kutokana na mmomonyoko wa mfumo wa ikolojia.
Idadi ya watu ambao ni maskini wapo katika lindi la
kuathiriwa na majanga au mazingira ambayo yanaweza kuwaacha wameharibikiwa bila
kuwa na njia ya kuyafikia au kupata mahitaji ya msingi kama malazi, chakula na
maji safi.
Athari nyingine ni pamoja na mabadiliko katika kuwepo kwa
vyanzo asili, chakula na maji - mambo ambayo yanaweza kusababisha mgongano
katika kuzifikia na athari hasi na nyingine
ambazo waathirika wakubwa ni jamii maskini.
Bioanuai inatoa changamoto kwa majanga haya ya asili na
kuhakikisha kuwepo kwa kiwango cha
usalama na tija katika uzalishaji.
Huduma za mfumo wa
ikolojia
Uwezo wa uzalishaji wa watu wanaoishi mijini na vijijini
unaungwa mkono na muingiliano wa huduma za mfumo wa ikolojia ambao ni bidhaa ya
jamii au umma na si kufanywa biashara.
Misitu, maeneo oevu, nyika, ukanda wa pwani na samaki na
mifumo mingine ya ikolojia inatoa maji, kuyasafisha, uboreshaji wa rutuba ya
udongo, udhibiti wa taka, mzunguko wa virutubisho na kuzuia mmomonyoko wa
udongo.
Hali kadhalika juzuia mafuriko na ukame ambao ni muhimu
kwa maisha ya binadamu wote, hususani jamii iliyo maskini ambao huathiriwa
kutokana na uharibifu kwenye huduma hizi.
Thamani za kitamaduni,
kiimani
Kwa jamii nyingi ndani ya maeneo yao bioanuai ndiyo inayounda
misingi ya imani zao za dini, uelewa au taaluma za kitamaduni na asasi za
kijamii.
Mfano hai upo kwa jamii mbalimbali ambazo hutumia na
huamini baadhi ya mimea kama utambulisho wao ikiwa inaunda sehemu ya maisha yao
kama ilivyo kwa mti wa isale miongoni mwa Wachagga.
Mmea huo mbali na kutumiwa kuweka mipaka ya mashamba una matumizi mengi
ambayo yameunganishwa ndani ya mila na tamaduni za kabila hilo.
Jamii za Wamasai licha ya kutumia misitu au mbuga kwa
ajili ya malisho ya wanyama wao pia zina utamaduni tajiri wa kugundua dawa
asilia (miti shamba) ambazo chanzo chake ni mimea mbalimbali mfano
Sichona- ambayo hutumika kusafisha
tumbo. Dawa hiyo asilia hutumika baada ya kuchanganywa na maziwa ya moto.
Pamoja na imani nyingine kufuatana na makazi ya jamii ni
dhahiri kwa njia moja au nyingine kunamfanya binadamu kuwa amefungamana na
mfumo mzima wa ikolojia.
Kutokana na hali hiyo jamii zote maskini na hata jamii
tajiri zimefungamanishwa na mfumo wa ikolojia ambamo ndimo zinaishi na
muunganiko huu unaunda misingi ya pamoja ya utambulisho na utamaduni wa jamii.
CHANZO: TANZANITE
Comments
Post a Comment