Featured Post

BIMA YA AFYA NA ENEO LA KUTOSHA, CHANGAMOTO KITUO CHA KULEA WATOTO YATIMA CHA MAUNGA NA JUMIA FOOD TANZANIA

Bima ya afya na eneo la kutosha, changamoto kituo cha kulea watoto yatima cha Maunga  
Na Jumia Food Tanzania

Kikiwa kimeanzishwa takribani miaka 10 iliyopita, kituo cha kulea watoto yatima cha Maunga kilichopo Kinondoni jijini Dar es Salaam kinakumbwa na changamoto kadhaa zikiwemo eneo la kutosha kuwalea na kuwahifadhi watoto pamoja na bima ya afya.
Kituo hiki ambacho mpaka hivi sasa kina jumla ya watoto 48 wakiwemo wavulana 26 huku 22 ni wasichana. Watoto hao wanaolelewa na Bi. Zainab Bakari ambaye ndiye mwanzilishi na mlezi wa watoto hao, anawahudumia kwa mahitaji yao yote muhimu yakiwemo malazi, chakula, mavazi, shule, afya na mengineyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kama vile serikali, sekta na watu binafsi kupitia misaada inayopelekwa kituoni hapo.

Akizungumza wakati akipokea msaada wa chakula na mahitaji ya shule kutoka kampuni ya Jumia Food, Bi. Bakari ameelezea kuwa watoto wanazidi kuongezeka kituoni kwake hali inayopelekea kuwa ni changamoto kuwahifadhi na kuwalea katika eneo moja kama inavyotakiwa.
“Kituo hiki nilikianzisha takribani miaka 10 iliyopita nikiwa na watoto wachache hapa kwenye hii nyumba yetu. Na kwa kipindi chote hiko nimekuwa nikipokea watoto na kuwalea hapahapa. Hivyo, kadri miaka inavyozidi kwenda ndivyo ninavyozidi kupokea watoto, wakizidi kukua na mahitaji kuongezeka. Hali hiyo imepelekea suala la kuwalea wote kwa pamoja kuwa ni changamoto kwasababu kituo hiki hakina uzio na kimezungukwa na nyumba za watu wengine,” alielezea Mwanzilishi na Mlezi wa Kituo cha Maunga.  

Jumia Food, kampuni inayojihusisha na huduma ya chakula kwa njia ya mtandao ilikuwa ikiendesha kampeni iliyokwenda kwa jina la “STAND BY ME” katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani. Kampeni hii iliwashirikisha wateja wake kwa kuwataka kuagiza chakula kwa kutumia nenosiri ‘ASANTE’ ili kuchangia mahitaji ya chakula kituoni hapo.
Mpaka kampeni inamalizika jumla ya huduma za chakula zilizofanyika kwa kutumia nenosiri ‘ASANTE’ zilikuwa zaidi ya 200. Hii inamaanisha kwamba idadi hiyo ya wateja wa Jumia Food ndiyo waliounga mkono kampeni hiyo ili kufanikisha watoto wa kituoni hapo kuwa na tabasamu katika msimu huu wa sikukuu za Eid al-Fitr kama watoto wengine.

“Kwa sasa changamoto kubwa ninayokumbana nayo kituoni hapa ni ufinyu wa eneo ambalo nawalea watoto hawa. Eneo ni lilelile tangu nilipofanya uamuzi nyumba hii kuwa kituo cha kulea watoto yatima. Idadi ya watoto inazidi kuongezeka kadri siku zinavyokwenda, kwasababu siwezi kukataa mtoto anayehitaji msaada. Ningependa kutumia fursa hii kuwaomba wadau na serikali kwa ujumla kunisaidia eneo ambalo litajengwa kituo kikubwa cha kutosha tofauti na hapa ili kuwatosheleza hawa nilionao na wengine watakaokuja,” alisema na kuhitimisha Bi. Bakari, “Kwa kuongezea, ningependa kutoa wito kwa wafadhili wajitokeze kunisaidia bima ya afya ili kusaidia pindi pale matibabu yanapohitajika. Matibabu ni gharama, huwa natumia gharama kubwa ili watoto waweze kupatiwa tiba.”
Naye kwa upande wake Meneja wa Maendeleo ya Biashara wa Jumia Food Tanzania, Bi. Sayi Makwaia amesema kuwa, “tumeona ni vema kuleta msaada huu wa mahitaji machache ya chakula na vifaa vya shule kituoni hapa. Waswahili husema, ‘Wema huanzia nyumbani.’ Kampuni yetu ipo jirani na kituo hiki, hivyo ni busara kuwathamini.”

“Maunga inakabiliana na changamoto kadhaa lakini kwa msaada huu wetu mdogo tunaamini utawasaidia kwa kiasi fulani na tunaahidi kuwakumbuka zaidi pale tutakapopata fursa. Ningeziomba pia taasisi na kampuni zingine ambazo zinafanya shughuli zao jirani na kituo kuweza kuwasaidia watoto hawa ili nao waweze kuishi maisha sawa na watoto wengine wenye wazazi na kuwalea,” alimalizia Bi. Makwaia.

Msaada wa mahitaji ya chakula na vifaa vya shule uliotolewa katika kituo cha kulea watoto yatima cha Maunga kutoka Jumia Food kwa niaba ya wateja wake ni pamoja na mchele, unga wa mahindi, maharage, sukari, mafuta ya kupikia, sabuni za kufulia, madaftari, penseli nakadhalika.

Comments