Featured Post

BIASHARA HARAMU YA TANZANITE, ALMASI INAMILIKIWA NA MAGAIDI



Na Daniel Mbega
KUJENGWA ukuta kuzunguka eneo la mgodi wa madini ya vito ya Tanzanite huko Mirerani mkoani Manyara kumezima biashara za magendo ya madini hayo pamoja na almasi ambazo zinadaiwa zimekuwa zikiyanufaisha makundi ya kigaidi duniani.
Ukuta huo wenye urefu wa kilometa 24.5 na kimo cha meta tatu, ulizinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli, Aprili 6, 2018, ukiwa umegharimu takriban shilingi bilioni 6.

Habari za uchunguzi zinaeleza kwamba, kujengwa kwa ukuta huo kulikotanguliwa na Ripoti ya Kamati Maalum ya Bunge ya kuchunguza biashara ya Tanzanite na almasi iliyoongozwa na Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu, ambayo ilibaini madudu mengi.
Ripoti ya Kamati ya Zungu ilieleza kwamba, Serikali ilipoteza mabilioni ya fedha kutokana na ushauri mbovu na usimamizi dhaifu katika mkataba wa kuuza hisa katika kampuni ya almasi mwaka 1994 ambao hazikusaidiwa na pia ubia wa Stamico na TanzaniteOne Mining Limited (TML) ambapo unaelezwa uliharakishwa na Waziri George Simbachawene.
Stamico pia ilionekana kutofuatilia mikataba yote huku baadhi ya watendaji wakibariki ubia huo na kusema ulikuwa ni msaada mkubwa kwa Stamico.
Ilielezwa kuwa hakuna taarifa sahihi kuhusu uzalishaji na uuzaji wa tanzanite ingawa duniani mauzo ni dola trilioni 8.582 katika miaka 12 iliyopita huku takwimu za Tanzania zikionyesha kwamba mauzo ni dola bilioni 454 tu kwa kipindi hicho.
Aidha, Kamati hiyo ilieleza pia kwamba, ni asilimia 20 tu ya uuzaji wa tanzanite unajulikana nchini lakini 80% husafirishwa kwa njia ya panya.

Magendo na ugaidi
Licha ya kamati hiyo kubainisha ufisadi mkubwa, mikataba yenye utata na ukwepaji wa kodi unaohusishwa na baadhi ya vigogo wa serikali, uchunguzi unaonyesha kwamba, asilimia kubwa ya uchimbaji na uuzaji wa tanzanite imekuwa ikipotea kwa njia za magendo, huku mamilioni ya dola yakidaiwa kwenda Mashariki ya Kati kufadhili makundi ya kigaidi.
Uchunguzi unaonyesha kwamba, kwa miaka mingi iliyopita, tanzanite imekuwa ikiuzwa kwa njia za magendo kupitia kwenye maduka mbalimbali ya wafanyabiashara jijini Arusha, ambapo baadhi yao wanatajwa kuwa na 'ushirika' na makundi hayo.
Madini hayo ambayo ni adimu mara 1000 kuliko almasi, yanadaiwa kuwa yamekuwa yakipitishwa kwa nia za panya kuingia nchi jirani ya Kenya, ambako husafishwa na kisha kusafirishwa kupelekwa Arabuni na baadaye Ulaya Magharibi ambako huuzwa kwa bei kubwa huku Tanzania ikikosa mapato.
Wafanyabiashara wa tanzanite, ambao serikali ilitegemea wangeweza kuongeza thamani ya madini hayo, kwa miaka mingi wameshindwa kutekeleza sera ya taifa ya madini.
Wakati Tanzania ikishindwa kuingiza mapato kupitia madini hayo, wafanyabiashara za magendo wamekuwa wakitajirika ambapo mengi kati ya madini hayo huishia kwenye maduka makubwa ya vito nchini Marekani kama Zales, QVC au Tiffany.
Lakini kutoka Mirerani hadi kwenye maduka ya vito Marekani, uchunguzi unaonyesha kwamba, madini hayo hupitia kwenye mikono mingi, ambapo baadhi ya mikono hiyo inawahusisha magaidi wa makundi hatari kama Al Qaeda na mengineyo.
Ingawa Chama cha Wafanyabiashara wa Madini (TMDA) kimekuwa kikikanusha kwamba biashara hiyo haiwahusishi Al Qaeda, lakini uchunguzi unaonyesha kwamba, kwa miaka mingi biashara hiyo imekuwa ikiendeshwa na 'maswahiba' wa Al Qaeda tangu kundi hilo likiongozwa na Osama bin Laden.
Kwa mujibu wa taarifa za uchunguzi, Waislamu wenye imani kali wanaounga mkono jihad, walikuwa wakijishughulisha na biashara hiyo ya tanzanite wakinunua kwa wachimbaji wadogo na madalali, na kuyavusha kwa magendo kupeleka Dubai au Hong Kong.
“Ni kweli, hapa kuna watu wanaowakilisha Al Qaeda. Wewe chunguza tu hapa utaona kuna watu wanaoamini jihad na wanafanya biashara hiyo," aliwahi kukaririwa Musa Abdallah, Mkenya ambaye alikuwa mwanaapolo kwa miaka sita.
Taarifa za kina kuhusu biashara hiyo zimeendelea kuwa siri, kama malengo ya biashara hiyo ya magendo ni kukusanya fedha za kuwahudumia wanamgambo wa makundi ya kigaidi au kuwasaidia magaidi hao kukusanya fedha na kufadhili harakati zao ulimwenguni.

Ulipuaji balozi 1998
William Wechsler, mjumbe wa zamani wa Baraza la Usalama la Marekani aliyeshughulikia masuala ya ugaidi chini ya utawala wa Bill Clinton, anasema hakuna shaka yoyote kwamba Al Qaeda inahusiana na biashara hiyo ya vito, ikiwemo tanzanite, na mapato yamekuwa yakitumika kufadhili harakati zao za kigaidi.
Uhusika wa Al-Qaida katika biashara ya tanzanite kwenye miaka ya 1990 uliwahi kufafanuliwa kwa kina katika kesi moja ambayo iliwatia hatiani washirika wanne wa Bin Laden wakihusishwa na ulipuaji wa Balozi za Marekani Tanzania na Kenya Agosti 7, 1998.
Mkuu wa Madini wa Kanda ya Kaskazini, Alex Magayane, akihojiwa na chombo kimoja cha habari ya kimataifa, alipata kusema kwamba, uwezekano wa makundi ya kigaidi kujihusisha na biashara hiyo ni mkubwa wakiyavusha kutoka Tanzania kuyapeleka Kenya na hatimaye Mashariki ya Kati.
Akiwa amejikita kwenye uchunguzi wa biashara ya tanzanite, Magayane alinukuliwa akisema: “Bila shaka yoyote, ni uhakika wa asilimia 100 kwamba wafanyabiashara hawa Waislamu wana uhusiano na Osama bin Laden.”
Uchunguzi unaonyesha kwamba, huko Mirerani, wachimbaji wadogo ambao ni Waislamu walikuwa wakishinikizwa kuuza tanzanite kwa Waislamu wenzao, huku biashara hiyo ikiendeshwa kwenye Msikiti wa Taqwa kila baada ya Swala ya Magharibi.
Inaelezwa kwamba, katika kipindi hicho, hata kama wafanyabaishara wasio Waislamu wangetoa bei nzuri, lakini wanaapolo wa Kiislamu walilazimishwa kutouza sehemu yoyote bali kwa Waislamu wenye itikadi kali.
Waislamu wafanyabiashara hao waliokuwa wakinunulia msikitini, ambao hawakuwa hata na leseni za biashara bali ni madalali tu, walikuwa wakieleza bayana kwamba biashara hiyo ni lazima isaidie jeshi lao la Kiislamu.
“Sisi Waislamu lazima tuungane kwenye biashara hii tusaidiane wenyewe kwa wenyewe na kukusanya fedha kuulinda Uislamu dhidi ya wale wanaotaka kuubomoa,” anasema Aman Mustafa, dalali wa tanzanite raia wa Kenya ambaye pia alikuwa akifundisha kwenye msikiti huo wa Mirerani, akisema alisomea Sheria katika Uislamu nchini Sudan.
Habari za uchunguzi zinaeleza kwamba, tanzanite iliyosafirishwa kimagendo ilipelekwa Mombasa nchini Kenya, ambako kunaelezwa kuwa ni ngome kubwa ya Al Qaeda pamoja na kundi la Al Shabaab linaloendesha mapambano nchini Somalia.
Kumbukumbu zinaonyesha kwamba, wakati wa kesi za ugaidi na ulipuaji wa Balozi za Marekani wa mwaka 1998, baadhi ya mashahidi na washtakiwa walieleza kwamba walikuwa wakijihusisha na biashara ya tanzanite katikati ya miaka ya 1990.
Vyanzo mbalimbali vya habari vilieleza kwamba, viapo vya mashahidi na watuhumiwa hao vilieleza namna tanzanite ilivyovushwa kupitia Kenya na hatimaye Hong Kong kwa kutumia mojawapo kati ya kampuni mbili za Al Qaeda, iitwayo Tanzanite King au Black Giant, ambayo ilianzishwa na mshtakiwa Wadih el Hage, mfanyabiashara wa vito na katibu mieka wa zamani wa Bin Laden.
Kwa sasa El Hage anatumikia kifungo cha maisha jela kwa kosa la kufadhili magaidi hao wa kujitoa muhanga.
Ingawa uchunguzi unaonyesha kundi la wafanyabiashara kadhaa nchini Tanzania wenye ushirika na Al Qaeda, lakini kwa sasa wanaendelea kufanya biashara zao bila kuingiliwa na mamlaka nyingine kwa kuwa "hakuna ushahidi wa kutosha kuonyesha ushirika wao na magaidi".
Inaonyesha kwamba, kabla ya mwaka 1998, hakuna aliyejua kwamba kulikuwa na biashara ya magendo ya tanzanite iliyohusisha kufadhili makundi ya kigaidi na vyombo vya dola vilijikita zaidi katika kupeleleza matukio na wahalifu, siyo biashara.


Comments