Featured Post

AFRIKA YATAKA UANDALIZI WA KOMBE LA DUNIA KUZUNGUKA

Musa Bility


MOSCOW, RUSSIA
Marais wa mashirikisho ya soka barani Afrika wameitaka Fifa kurudisha mfumo wa mzunguko ili kuliwezesha kila bara kuandaa awamu moja ya michuano ya Kombe la Dunia.

Hii ni baada ya Morocco kupoteza dhidi ya Marekani kwa kura 134 kwa 65 kwenye kinyang'anyiro cha kumsaka mwenyeji wa fainali za mwaka 2026.
"Njia ya mzunguko itakuwa suluhisho bora," amesema rais wa Chama cha Soka Malawi, Walter Nyamilandu.
Kauli hiyo imeungwa mkono na kiongozi wa Shirikisho la Soka Liberia, Musa Bility.
"Tunafaa kutoa ombi la kurekebishwa utaratibu wa kumsaka muandaaji wa Kombe la Dunia ili kuwezesha kurudishwa kwa mtindo wa bara moja kuliandaa kombe," alisema Bility.
Bility, ambaye pia ni mwanachama wa Bodi ya Makatibu wa Shirilisho la Soka Afrika (CAF), ameitaka Fifa kuangazia njia hiyo akiitaja kuwa Kombe la Dunia ni kufikisha soka kwa wapenzi wake.
Njia hiyo iliyoanzishwa mwaka wa 2001 kabla ya kutupiliwa mbali 2007, imekuwa na manufaa kwa Afrika kwani mwaka wa 2010 Afrika iliandaa kwa mara ya kwanza fainali hizo zilizofanyika nchini Afrika Kusini.
Rais wa zamani wa Fifa, Sepp Blatter, alileta pendekezo hilo baada ya Afrika Kusini kupoteza kura za kuwa mwenyeji mwaka 2006.
Pigo la Morocco dhidi ya Canada, Mexico na Marekani linamaanisha kuwa Bara la Afrika limeandaa Kombe la Dunia mara moja kati ya fainali 23 za michuano hiyo ilihali Mexico pekee imeanda kombe mara tatu.
Ingawa Liberia ni mojawapo ya mataifa yaliyoipa kisogo Morocco, Rais Bility analaumu ukosefu wa njia ya kuyasawazisha mataifa yote.
"Mataifa yote duniani hayako sawa kwa hivyo sheria za kuwezesha mashindano kuandaliwa maeneo tofauti zinahitajika, Morocco isingeweza kuibwaga Marekani kwa namna yoyote ile," alisema Bility.
Matokeo ya kura za kumsaka mwenyeji wa Kombe la Dunia yamewaacha wengi vinywa wazi wajumbe wakiuliza maswali ya ni lini Afrika itaandaa tena Kombe hilo.

Comments