Kelvin Yondan (katikati) akiwa na Hussein Nyika (kushoto) na Kaisi (kulia) leo Jangwani
Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
NAHODHA
wa Yanga SC, Kevin Patrick Yondan ameonyesha dalili atabaki baada ya
leo kufika makao makuu, Jangwani na kufanya mazungumzo na uongozi.
Yondan
ambaye anahusishwa na mpango wa kurejea timu yake ya zamani, Simba SC
asubuhi ya leo alifika makau ya klabu makutano ya mitaa ya Twiga na
Jangwani, Dar es Salaam na kuzungumza na Katibu, Charles Boniface Mkwasa
pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano, Hussein Nyika.
Kabla
ya kuondoka, Yondan akapiga picha ya pamoja na Nyika na mwanachama
maarufu wa klabu hiyo, Kaisi – ingawa bado haijulikani mazungumzo yao
yalihusu nini.
Yondan
amemaliza mkataba wake Yanga SC na inasemekana na kusaini mkataba mpya
kunacheleweshwa na fedha, kwa sababu klabu kwa sasa inakabiliwa na hali
ngumu kiuchumi.
Yondan
hayumo kwenye kikosi cha Yanga kilichoondoka mchana wa leo kwenda Kenya
kwenye michuano ya SportPesa Super Cup kwa sababu ambazo hazijawekwa
wazi.
Kikosi
kilichokwenda Kenya kinaundwa na kipa Mcameroon Youthe Rostand, mzawa
Ramadhani Kabwili, mabeki Hassan Kessy, Mwinyi Hajji Mngwali, Abdallah
Shaibu ‘Ninja’ na Pato Ngonyani.
Viungo
ni Baruan Akilimali, Pius Buswita, Ajib, Maka Edward, Thabani Kamusoko,
Juma Mahadhi, Said Juma ‘Makapu’, Said ‘Ronaldo’ Mussa, Papy Kabamba
Tshishimbi, Yussuf Mhilu na Raphael Daudi, wakati washambuliaji ni
Yohana Oscar Nkomola, Matheo Anthony na Mrundi Amissi Tambwe.
Yanga
watafungua dimba na Kakamega Homeboys Jumatatu, siku moja baada ya
mahasimu wao, Simba SC kumenyana na Kariobangi Sharks Jumapili, mechi
zote zikichezwa Uwanja wa Afraha, Nakuru.
Mabingwa watetezi, Gor Mahia wao pia wataanza na JKU Jumapili, wakati Singida United itaanza na AFC Leopards Jumanne.
Ikumbukwe
bingwa wa michuano hiyo ataondoka kitita cha dola za Kimarekani,
30,000, mshindi wa pili dola 10,000, wa tatu dola 7,500 zitakazoishia
Nusu Fainali dola 5,000 na za Robo Fainali dola 2,500.
Pamoja
na dola 30,000, bingwa wa michuano hiyo kwa mwaka huu atapata fursa ya
kwenda kumenyana na klabu ya Everton Uwanja wa Goodison Park mjini
Walton, Liverpool nchini England.
Mwaka
jana Gor Mahia ilikuwa bingwa wa kwanza wa michuano hiyo baada ya
kuwafunga mahasimu wao, AFC Leopard 2-1 katika fainali kwenye michuano
iliyofanyika Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
BIN ZUBEIRY
Comments
Post a Comment