Featured Post

WAKENYA WAANDAMANA DHIDI YA RUSHWA YA VIGOGO NYS



NAIROBI, KENYA
Raia wa Kenya wanafanya maandamano makubwa katika miji mikubwa ya nchi hiyo kulaani ufisadi wa mabilioni ya dola katika serikali.
Katika kampeni hiyo inayoendeshwa kupitia mitandao ya kijamii kama vile Facebook na Twitter Wakenya wanasema wamechoshwa na visa vya maafisa wa serikali kuiba pesa zao na kuachiliwa huru.

Maandamano hayo yanafanyika baada ya kukamatwa na kushtakiwa kwa washukiwa 20 kati ya 50 waliokuwa wamekamatwa kutokana na sakata ya ufujaji wa Sh8 bilioni ($78m) kutoka kwa Shirika la Vijana wa Huduma kwa Taifa (NYS) nchini Kenya kufikishwa mahakamani.
Miongoni mwa walioshtakiwa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Masuala ya Vijana na Jinsia Lilian Mbugua Omollo na Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Bw Richard Ndubai.
Aidha, mameneja wa kampuni ambazo zinadaiwa kuhusika katika ufujaji wa pesa hizo walifikishwa kortini Milimani, Nairobi.
Wanakabiliwa na mashtaka mbalimbali yanayohusiana na kutoweka kwa dola milioni 5 kati ya takriban dola milioni 80 zilizopotea katika shirika hilo la NYS.
Licha ya kukamatwa na kushtakiwa kwa baadhi ya watuhumiwa wa wizi wa pesa za umma nchini Kenya, raia wanasema hawana imani kuwa wahusika watakabiliana na mkono wa sheria , kutokana na kwamba washukiwa katika sakata za ufisadi zilizofichuliwa vipindi vilivyopita waliachiliwa.
Serikali ya rais Uhuru Kenyatta imekumbwa na sakata kadhaa katika siku za hivi karibuni katika kile kianachoonekana kushindwa kwa juhudi za kupambana na ufisadi.

Comments